BAADHI YA MADIWANI WA UDP NA CCM WALIOHAMIA CHADEMA WAKONESHA KADI ZAO ZA CHADEMA
Siku moja baada ya Madiwani 10 CCM, pamoja na UDP kutimkia  Chadema katika wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, jana Chama hicho kimepokea madiwani wengine 9 kutoka  chama cha United Democratic Party (UDP) katika jimbo la Itilima mkoani hapa.


Madiwani hao walidai kuwa sababu za kujiunga na chama cha democrasia na maendeleo (CHADEMA) ni kutokana na chama chao za zamani UDP  kukosa kiongozi makini ambaye anaweza kukisimamia chama hicho.

Madiwani hao wakiongea katika mkutano wa chadema uliofanyika katika kijiji cha Luguru wilayani Itilima walisema kuwa chama hicho kimekosa mvuto wa kisiasa wakuweza kushindana na vyama vingine vya siasa pamoja na kutokuwa na uongozi mzuri wa chama hicho.

Mmoja wa madiwani waliotoka UDP na kuhamia chadema Nicodemas Athumani alisema kuwa amefikia uamuzi huo wa kuhama chama ni kutokana na chama hicho kuwa hakina viongozi makini ambao wanaweza kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho.

“Tumeamua kuhama chama kutokana na kukosa viongozi ambao wanasimamia maslahi ya chama hata ukiangalia tulikosa hata wagombea kwenye serikali ya mitaa wananchama wote walikataa kugombea na matokeo yake chama kilishindwa kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi huo”Alisema Athumani.

Waliorudisha kadi na kujiunga na chadema ni pamoja na Mbuke Mlyandengu viti maalumu kata ya Nhobora(udp),Luli Tabulo viti maalumu kata ya Luguru(udp),James Kidayi diwani wa kata ya Chinamili (udp),Ntundu ntemi diwani kata ya Mbita (UDP).

Wengine ni Nicodemus Athumani diwani wa kata ya Mhunze (UDP),Kilinga Mayani diwani wa kata ya Ikindilo (UDP),Kinda Nindwa diwani wa kata ya Ndoleleji (UDP),Tano Butamane diwani wa kata ya Mwamtani (UDP)pamoja na Jackson Scania diwani wa kata ya Kinang’weli (CCM).

Akiwakabidhi kadi madiwani hao katibu wa chadema wilaya ya Itilima Gimbi Masaba alisema kuwa wanachama waliopo katika chama cha mapinduzi msiwachukie bali tuwapende kwani ipo siku na wao watahamia na kujiunga na jeshi la ukombozi.

Gimbi alisema wananchi wanatakiwa kufanya siasa za amani ambazo zinalenga kuleta mahusiano baina ya wanachama wa vyama vyote ili kuweza kuepuka siasa za chuki baina ya wakeleketwa wa vyama vya siasa.

“Tunawapokea wananchama hawa ambao wametoka chama cha UDP  na kujiunga na gari la ukombozi ila tusiwachukie wanachama waliopo katika vyama vingine na tutaendelea kuwapokea na wao wasione aibu waje kujiunga na jeshi la ukombozi la chadema”Alisema Samba.

Kwa upande wake Mtangaza nia wa ubunge jimbo hilo Martin Magile aliwataka wananchi na wanachama wa chadema kuwaunga mkono waliotangaza nia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweza kuleta umoja na nguvu ili kuwashinda chama cha mapinduzi.

Alisema kuwa lazima tuwe wamoja katika kuleta mapinduzi kutoka kwa mafisadi wa ccm na kwamba tumekuwa tukinyanyswa na ccm kwani fursa zote wanazichukua zote na kwamba wanahitaji mabadiliko ili rasilimali za nchi ziweze kunufaisha kila mtamzania.

Jumla ya madiwani 18 UDP katika majimbo mawili ya Itilima na Bariadi Magharibi wamehama chama hicho na kuhamia chedema na kukiweka katika njia panda chama hicho kwa kukosa madiwani katika kata hizo.

Chanzo: Simiyu Yetu blog.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top