Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum.

Baadhi ya familia za wachimbaji wadogo walioko katika kitongoji cha Mahiga kata ya Mwakitolyo wakimsikiliza mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum kufuatia agizo la mkuu wa mkoa kuwataka waondoke katika eneo hilo.

MBUNGE wa Jimbo la Solwa mkoani Shinyanga, Ahmed Salum amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali kutafisiri isivyo maagizo yanayotolewa na Rais Dkt. John Magufuli hali inayoweza kusababisha wananchi kuichukua serikali yao iliyopo madarakani hivi sasa.

Kauli ya mbunge huyo inafuatia agizo lililotolewa hivi karibuni na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab  Telack kuwataka wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu yaliyopo katika kitongoji cha Mahiga kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga kuondoka katika maeneo hayo ndani ya siku saba ili kumpisha mwekezaji kutoka nje.


Wachimbaji wadogo katika kitongoji cha Mahiga wakimsikiliza mbunge wa Jimbo la Solwa.




Baadhi ya dhana za kazi zinazotumiwa na wachimbaji wadogo.

Akizungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano wa dharula uliofanyika juzi katika kitongoji cha Mahiga, mbunge Salum alielezea kusikitishwa na agizo hilo la mkuu wa mkoa kwa vile linapingana na maelekezo yaliyotolewa na rais alipozuia wachimbaji wadogo kutofukuzwa katika maeneo yao kwa kisingizio cha kuwapisha wawekezaji wa kigeni.

Mbunge Salum amewataka wachimbaji hao kutotekeleza agizo la kuondoka katika eneo hilo na badala yake waendelee na shughuli zao kama kawaida na kama ni kukamatwa basi yeye ndiye atakayekuwa mtu wa kwanza kukamatwa kwa niaba ya wapiga kura wake na kwamba moja ya malengo ya serikali ya awamu ya tano ni kuwakomboa wanyonge.

Akifafanua kuhusu agizo la mkuu wa mkoa alisema, baadhi ya watendaji wa serikali wamekuwa wakitafisiri vibaya maagizo yanayotolewa na Rais aidha kwa nidhamu ya woga au kutaka kujipendekeza kwa viongozi wakuu ndani ya serikali hali inayoweza kusababisha wananchi kuichukia serikali iliyopo madarakani.

“Ukweli ndugu zangu nimesikitishwa na hatua ya mkuu wetu wa mkoa kuwataka ndani ya siku saba muwe muondoke katika eneo hili kwa madai eti lipo chini ya mwekezaji, nilishitushwa na agizo hili la mtendaji wetu mkuu katika ngazi ya mkoa kiuhalisia linapingana na agizo la Rais wetu, sasa nasema msiondoke na endeleeni kufanya kazi zenu kama kawaida,”

“Nilimpigia simu na kumuuliza kapata wapi agizo hilo, Je, Rais Magufuli ametengua agizo lake alilolitoa hivi karibuni, au limetolewa na mtu gani mwingine? Alinijibu hana maelekezo yoyote ya Rais, bali anazingatia sheria kwa vile eneo hili lipo chini ya leseni ya mwekezaji, mimi nasema huku nikupingana na rais wake, hivyo nasisitiza msiondoke,” alieleza.

Mbunge Ahmed Salum akisisitiza jambo mbele ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika kata ya Mwakitolyo.

Aliendelea kufafanua mbali ya kuwasiliana na mkuu wa mkoa, pia aliwasiliana na Naibu waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani iwapo ofisi yake imetoa maagizo ya kuwataka wachimbaji wadogo kuondoka katika eneo hilo ambapo alikana na kueleza hakuna maelekezo yoyote ya rais kutengua kauli yake ya awali.

“Sisi tulivyomuelewa Rais ni kwamba wachimbaji wote wadogo walioko katika eneo la kata ya Mwakitolyo wasibughudhiwe, hakusema eti wanaohusika ni wale wa eneo la Nyaligongo kwani Mwakitolyo ni moja ikijumuisha pia kitongoji hiki cha Mahiga,”

“Nafikiri ingekuwa busara kwa mkuu wa mkoa kabla ya kutoa agizo hili huku akitumia askari wa FFU kuwatisha wananchi angewasiliana kwanza na mwajiri wake, ambaye ni Rais ili ampatie ufafanuzi wa kina badala ya kukurupuka kama alivyofanya, sasa endeleeni na kazi mpaka pale Rais atakapokuwa ametoa ufafanuzi wa kina,” alieleza Salum.

Kwa upande mwingine mbunge huyo ametoa wito kwa wachimbaji wote wadogo kujiunga katika vikundi vidogo vidogo ili waweze kusajiliwa na watambulike kisheria ambapo yeye binafsi tayari ameanza kushughulikia mchakato wa kuwapatia hatimiliki ikiwemo leseni za uchimbaji ili wafanye shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje aliwapongeza wachimbaji wadogo wote katika kata ya Mwakitolyo kwa jinsi walivyounga mkono agizo la serikali la kuchangia fedha kwa ajili ya utengenezaji wa madawati na ujenzi wa maabara kinyume na mwekezaji ambaye hajafanya lolote ndani ya kipindi cha miaka 10.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika kitongoji cha Mahiga kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga.


“Kwa niaba ya halmashauri yenu ya wilaya nichukue nafasi hii kukupongezeni kwa michango yenu yote mliyoitoa iliyofanikisha kazi ya utengenezaji wa madawati na ujenzi wa maabara katika shule zilizopo katika kata yenu, ukweli mlifanya kazi nzuri na halmashauri haijawahi kupokea mchango wowote kutoka kwa mwekezaji anayedaiwa kumiliki eneo hili,”

“Kwa hali hiyo na mimi naungana na mbunge wetu kusema endeleeni kufanya kazi na msiondoke hapa mpaka utakapopatikana ufafanuzi wa mheshimiwa Rais juu ya agizo lake, haiwezekani mtu mmoja ambaye hajafanya lolote hapa kwa zaidi ya miaka 10 yeye abaki na ninyi muondolewe, hapana, kikubwa lipeni ushuru mnaotakiwa kulipa,” alieleza Mboje.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga vijijini, Mwenzetu Mgeja aliwapa pole wachimbaji hao kutokana na “timbwilitimbwili” walizozipata na kuwashukuru kwa utulivu waliouonesha mpaka hivi sasa hali iliyotoa nafasi kwa mgogoro wao kushughulikiwa kwa utaratibu.

“Ndugu zangu kwanza nakupeni pole kwa haya yaliyowakuta, na ninawashukuru kwa utulivu mliouonesha mpaka hivi sasa, sisi viongozi wenu wa chama tunasema daima tupo kwa ajili ya watanzania wanyonge na tutahakikisha haki inatendeka na si vinginevyo, tulieni na msibabaike mpaka pale ufumbuzi utakapokuwa umepatikana,” alieleza Mgeja.

Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alitoa agizo la kuwataka wachimbaji wadogo walioko katika kitongoji cha Mahiga kuondoka katika eneo hilo kwa madai lipo chini ya leseni ya mwekezaji kampuni ya Henan Afro Asian Geo Engineering kutoka nchini China ambaye ndiye mwenye haki ya uchimbaji.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini, kanda ya kati Magharibi, Mhandisi Hamisi Kamando alisema pamoja na agizo lililotolewa na Rais kuzuia wachimbaji wadogo kutobughudhiwa katika maeneo yao, lakini wao watendaji ndiyo wanaotafsiri maagizo anayoyatoa na kuyatekeleza kwa kuzingatia sheria za nchi.

"Ni kweli Rais alisema wachimbaji walioko kata ya Mwakitolyo wasibughudhiwe, hakutaja eneo rasmi, sisi tulivyoelewa ni eneo lililokuwa na leseni ya Pangea Minerals namba PL 5044/2008, na siyo maeneo mengine, hivyo hawa walioko pale Mahiga wanatakiwa kuondoka mara moja.  Eleweni Rais anapotoa maagizo, sisi watendaji wake ndiyo hutafsiri maagizo hayo kwa mujibu wa sheria zilizopo," alieleza Kamando.






Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top