Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA Taifa, Halima Mdee akihutubia mamia ya wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake.


Maelfu ya wakazi wa Mji wa Shinyanga na vitongoji vyake wakimsikiliza mwenyekiti wa Taifa wa BAWACHA, Halima Mdee katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Mahakama ya Mwanzo mjini Shinyanga.aption
Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Halima Mdee akipokea kadi ya CCM kutoka kwa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Tawi la Jikolile kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, Robert Ng'welo baada ya kada huyo kuamua kujiunga na CHADEMA juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga. Kulia aliyekaa chini mwenye miwani ni kada mwingine wa CCM, Joseph Rweyemamu ambaye pia alijiunga na CHADEMA on

MWENYEKITI wa Taifa wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee amewataka wakazi wa Shinyanga waache kulalamika na kupiga kelele wakituhumu kuibiwa kura za ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2010 ambapo alitoa wito wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kwenye upigaji kura.

Mdee alitoa wito huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga kwenye viwanja vya Mahakama ya Mwanzo ikiwa ni moja ya harakati za chama chake kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuikataa katiba pendekezwa iliyopitishwa hivi karibuni kutokana na kutupilia mbali sehemu kubwa na maoni yaliyotolewa na wananchi.

Huku akishangiliwa Mdee alisema anashangazwa na kauli za wananchi wa Shinyanga kudai katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 waliibiwa kura za ubunge jimbo la Shinyanga mjini na kwamba aliyekuwa ameshinda katika uchaguzi huo ni mgombea wa CHADEMA, hayati Philipo Shelembi na ushindi wa mbunge wa CCM aliyepo ulitokana na kura kuchakachuliwa.

Alisema hata kama ushindi wao ulichakachuliwa hiyo ilisababishwa na uzembe na woga wao wa kutokubali kulinda kura zao na wengine wakishindwa kwenda vituoni kupiga kura kutokana na kutokujiandikisha kwa wingi na kwamba ili kuishinda CCM inahitajika nguvu kubwa kama walivyofanya wapiga kura wa jimbo lake la Kawe jijini Dar es Salaam.

“Ndugu zangu wana wa Shinyanga, acheni kukaa mkilalamika kwamba 2010 mliibiwa kura zenu, ni ninyi wenyewe hamkukaza buti sawasawa, kama mngekuwa imara hakuna kura hata moja ambayo ingepotea, kama ni suala la CCM kuiba kura, basi wangekuwa na uwezo huo katika jimbo langu ambako serikali yote ndiyo makazi yake kuanzia Ikulu ya Magogoni hadi usalama wa Taifa,”

“Vijana wa Kawe walisimama kidete wakakaza buti zao, hakuna ujanja wowote uliofanyika, leo hii ninapoongea Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa watu wa Jimbo langu, mawaziri na viongozi wakuu mbalimbali wa serikali mimi ndiyo mbunge wao, tulikaza buti kwelikweli bila kulegeza, kuing’oa CCM madarakani kunahitaji juhudi si mchezo,” alieleza Mdee.

Kutokana na hali hiyo aliwaomba vijana na wanachama wote wa CHADEMA kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na daftari la kudumu mwakani na kwamba kila mmoja wao ahakikishe anakwenda kupiga kura bila kukosa na wazilinde kura zao ili zisiibwe.

Katika hatua nyingine Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano huo kilipata pigo baada ya kuwapoteza makada wake wawili waliojiunga na CHADEMA  wakidai kuvutiwa na hotuba iliyotolewa na mwenyekiti huyo wa BAWACHA Taifa aliyesema lengo la CHADEMA ni kuhakikisha nchi inapata ukombozi wa pili utakaowawezesha watanzania kufaidi raslimali zilizopo nchini.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya makada hao kukatisha hotuba ya Mdee walipoingia katikati ya uwanja wakiinua mikono juu kwa madai wanataka kuokoka hali iliyowashangaza wananchi katika mkutano huo huku wakifuatwa na Red Bridged waliowafuata kwa lengo la kutaka kuwatoa hata hivyo waliposema wanataka kujiunga na CHADEMA walishangiliwa kwa nguvu na wananchi.

Makada walioamua kuhama CCM na kujiunga na CHADEMA ni pamoja na aliyekuwa katibu mwenezi wa CCM Tawi la Jikolile kata ya Ndembezi, Robert Ng’welo na Joseph Rweyemamu aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kolandoto ambao wote kwa pamoja na walimkabidhi Mdee kadi zao za CCM na kupewa za CHADEMA.

Kwa upande wake Mdee aliwapongeza makada hao kwa kuuona ukweli na kuwataka wana CCM wengine wenye nia nzuri na Taifa leo kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA ili waunganishe nguvu kupitia Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA) kuing’oa CCM madarakani ambayo daima imeshindwa kuwaletea maisha mazuri.


Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top