Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga, James Lembeli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa CHADEMA wilayani Kahama.
Mbunge wa Kahama, James Lembeli ameiweka njiapanda CCM baada ya kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.


Uamuzi wa Lembeli umekuja wakati wanachama kutoka sehemu mbalimbali wakitangaza uamuzi wao wa kujiengua CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema ambayo imesomba asilimia kubwa ya wahamaji hao.

Lembeli alisema taarifa hizo ni uvumi uliozagaa jimboni kwake, lakini hajajiunga na chama chochote.

“Ni uvumi tu na uvumi wenyewe umechangiwa na swali nililoulizwa leo na wananchi kwamba ‘mbona toka mchakato wa kuchukua fomu umeanza hatujakuona’ na mimi nikawajibu kuwa ‘sitachukua fomu’,” alisema.

Lembeli alisema amechukua uamuzi huo kutokana na rafu inayoendelea jimboni humo na maneno ya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi kuwa hatakiwi na vigogo ndani ya CCM.

Lembeli, mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema sababu za kutotakiwa huko zinatokana na dhana potofu ya baadhi ya viongozi kwamba michango yake ndani na nje ya Bunge inaivua nguo Serikali.

“Tangu mchakato wa uchukuaji wa fomu umeanza baadhi ya wanachama wengi tu wameitwa kwenye vikao visivyo halali karibu kata zote wakiwa na kadi zao na kuorodheshwa na kupewa maagizo ya kunikataa kwenye kura ya maoni na wengine wanapewa Sh5,000,” alisema mwandishi huyo wa habari.

Lembeli alidai kuwa mbaya zaidi ni kwamba zipo kadi mpya za CCM zinazotolewa kiholela bila kufuata utaratibu na licha ya kulalamikia hali hiyo hakuna hatua zilizochukuliwa.

Alisema kutokana na yote hayo, aliwahi kusema kwenye mkutano wa hadhara kuwa kuna njama hizo, lakini badala ya CCM kufanyia kazi madai hayo, wakamuita mbele ya Kamati ya Maadili.

“Kwenye kamati ya maadili nilituhumiwa kuwa nakidhalilisha chama na kutakiwa niwataje nani walioniambia sitakiwi. Niliwajibu, tena kwa maandishi na kuwapa orodha, lakini mpaka leo kimya ina maana mimi bado ni mtuhumiwa,” alidai.

“Mimi siyo mtoto mdogo. Naelewa nini kinaendelea na ndiyo maana nimesema sitachukua fomu ya kugombea ubunge kwa mazingira haya. Bado sijatangaza kuhama CCM”.

Wakati Lembeli akisisitiza suala la kuhama kwake ni fununu tu, habari nyingine zilidai huenda akagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema kutokana na kutokubaliana na mchakato huo anaodai ni batili.

Chanzo: Mwananchi.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top