SIKU chache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa wa
wizara ya sheria na katiba nchini, waziri mpya wa wizara hiyo, Profesa
Palamagamba Kabudi ameshauriwa aangalie uwezekano wa kumshauri Rais Dkt. John
Magufuli kuruhusu kuendelea kwa mchakato wa uandikwaji wa katiba mpya nchini.
Ushauri huo umetolewa na mwenyekiti wa Taasisi ya
Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari mjini Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni siku chache baada ya Rais Dkt.
Magufuli kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake la mawaziri.
Mgeja ambaye taasisi yake inajishughulisha na masuala
ya uelimishaji jamii kuhusu utawala bora na haki za kibinadamu hapa nchini
alisema, moja ya mambo ambayo Profesa Kabudi anapaswa kuyapa kipaumbele ni
suala la kuendeleza mchakato wa upatikanaji katiba mpya hapa nchini.
Akifafanua Mgeja alisema Katiba mpya ndiyo itakayokuwa
ufumbuzi wa uimarishaji wa demokrasia hapa nchini na itakoyotoa haki za msingi
kwa raia tofauti na katiba iliyopo hivi sasa ambayo ikitumika vibaya inaweza
kusababisha viongozi walioko madarakani kuongoza kama wafalme.
“Suala la katiba mpya katika nchi ye yote ulimwenguni
siyo la watu wachache au kikundi fulani, ni suala la wananchi wenyewe, hivyo
serikali zote zilizopo madarakani zinapaswa kuheshimu matakwa na maoni ya
wananchi wake si vinginevyo,”
“Kwa hali hii basi, mara baada ya ndugu yetu Profesa
kukabidhiwa mikoba ya wizara ya sheria na katiba, agenda yake ya kwanza ya
kufanyia kazi iwe ni kuanzisha mchakato utakaoendeleza uandikwaji na kuwezesha
kupatikana kwa katiba mpya, maana tayari mamilioni ya fedha za walipa kodi
yalitumika katika mchakato wa awali,” alieleza Mgeja.
Mgeja
alisema anamtambua Profesha Kabudi ni msomi aliyebobea katika masuala ya sheria
hivyo ni vizuri sasa akaonesha uzoefu wake katika masuala ya sheria na amshauri
Rais Dkt. Magufuli kwa umakini kuhusu matakwa ya wananchi wa Tanzania wenye kiu
kubwa ya kupatikana kwa Katiba mpya.
Alisema
ni vizuri suala la katiba mpya likaanza kushughulikiwa hivi sasa kwa vile
linavyocheleweshwa ndivyo siku zinavyokwenda mbele kuelekea uchaguzi mkuu
mwingine mwaka 2020 utakaotanguliwa na ule wa serikali za mitaa utakaofanyika
mwaka 2019.
“Ukiangalia
muda wa kuwepo madarakani kwa serikali hii ya awamu ya tano unazidi kuyoyoma
kila siku, ki uhalisia tumebakiza mwaka mmoja pekee wa shughuli nyingine za
kawaida, yaani mwaka 2018, hivyo ni vyema mchakato wa upatikanaji wa katiba
mpya ukaanza hivi sasa ili kutoa nafasi ya chaguzi hizo za 2019 na 2020,”
“Bahati
nzuri mtu aliyepokea kijiti kutoka kwa ndugu yetu Mwakyembe, alikuwa miongoni
mwa wajumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na katiba mpya
iliyokuwa ikiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, sasa atumie fursa hiyo kuendeleza
mchakto pale ulipokuwa umeishia,” alieleza Mgeja.
Wajumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kutoka kwa wananchi wakati huo wakiwa katika moja ya vikao vya kukusanya maoni. |
Aliendelea
kueleza kuwa mashaka yake ni kuona iwapo mchakato huo utacheleweshwa kuanza
hivi sasa, baada ya mwaka 2018 viongozi walioko madarakani watakuwa na
visingizio vingi wakidai muda wa kufanya mabadiliko ya katiba haupo tena na
badala yake nguvu zote kuelekezwa kwenye mchakato wa uchaguzi.
Alisema
watanzania wengi wana hamu ya kusikia lini mchakato wa upatikanaji wa katiba
mpya hapa nchini utaanza na kwamba wanaona kuwepo kwa wingu zito huku baadhi ya
viongozi wakiamini suala la katiba mpya siyo kipaumbele chao ama cha Taifa kwa
hivi sasa.
“Iwapo
suala hili litashindikana ni wazi itakuwa ni “Jipu” jingine nchini na
linahitaji kutumbuliwa kutokana na kusababisha hasara kubwa kwa watanzania
ikizingatiwa fedha nyingi zilizotumika kwenye ukusanyaji wa maoni kutoka kwa
wananchi na Bunge maalumu la Katiba lililoongozwa na hayati Samwel Sitta,”
alieleza Mgeja.
Post a Comment