Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, Graham Crew (kushoto) akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga, mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi 374,608,900 kwa ajili ya Halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita ikiwa ni ada ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha miezi sita (July - Dec. 2016) Kulia anayeshuhudia ni katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela. |
MBUNGE wa Jimbo la Msalala wilayani Kahama mkoa
wa Shinyanga, Ezekiel Maige ameupongeza uongozi wa Mgodi wa dhahabu wa
Bulyanhulu kwa kuilipa Halmashauri ya Msalala ada ya ushuru wa huduma kwa
mujibu wa sheria.
Maige ametoa pongezi hizo katika hafla fupi ya
makabidhiano ya hundi yenye thamani ya shilingi milioni 760 kwa halmashauri ya
Msalala na shilingi milioni 374 kwa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani
Geita.
Akikabidhi hundi hizo, Meneja Mkuu wa mgodi wa
dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya Acacia, Graham Crew alisema
malipo hayo ni moja ya utekelezaji wa sheria inayowataka wawekezaji kulipa ada
ya ushuru wa huduma kwa halmashauri utakaosaidia kusukuma maendeleo ya jamii.
Akifafanua Crew alisema hadi kufikia mwishoni
mwa mwaka 2016, mgodi huo umelipa kiasi cha shilingi bilioni 4.8 tangu mwaka
2014 kampuni ya Acacia ilipoanza kutoa malipo ya ushuru wa huduma wa asilimia
0.3 ya mapato ghafi kwa halmashauri ya husika.
“Fedha hii tunayoikabidhi leo hii ni malipo ya
awamu ya pili ya ada ya ushuru wa huduma ambayo tumeanza kulipa tangu mwaka
2014, ni utekelezaji wa sheria inayotutaka kulipia ushuru wa huduma asilimia
0.3 ya mapato yetu ghafi tunayopata katika halmashauri husika,”
“Mpaka hivi sasa tumeisha lipa ushuru huu kiasi
cha shilingi bilioni 4.8 kwa halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga na
Nyang’hwale kwa mkoa wa Geita, kwa awamu hii ya pili kwa mwaka 2016, tumelipa
shilingi milioni 760 kwa halmashauri ya Msalala na shilingi bilioni 374 kwa
Nyang’hwale,” alieleza Crew.
Sehemu ya mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu. |
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Msalala,
Ezekiel Maige pamoja na kupongeza kitendo cha mgodi huo kulipa ushuru stahiki
kwa mujibu wa sheria, aliuomba uongozi wa mgodi kuwabana wakandarasi wadogo
wanaopewa kazi na mgodi ili na wao waweze kulipa ada hiyo ya ushuru wa huduma.
Maige alisema pamoja na mgodi wa Bulyanhulu
kutekeleza sheria, bado makampuni mengi ya ukandarasi yanayopewa kazi
mbalimbali mgodini hayazilipi halmashauri husika ushuru huo na kwamba viongozi
wa halmashauri hawana uwezo wa kuyabaini makampuni hayo bali kwa msaada wa
uongozi wa mgodi.
“Pamoja na kuwapongezeni kwa utekelezaji wa
sheria hii, lakini bado tuna safari ndefu, wananchi wetu bado wana kiu kubwa ya
kuona jinsi gani wananufaika na raslimali zilizopo katika maeneo yao, hivyo
tunaomba tusaidiane kuyabana makampuni mnayoyapa kazi ili na yenyewe yatulipe
ushuru huu,” alieleza Maige.
Naye meneja mkuu wa mahusiano kati ya kampuni
na serikali, Asa Mwaipopo alisema malipo yaliyolipwa na mgodi wa Bulyanhulu ni
moja wa wajibu wake katika kutekeleza sheria zilizopo nchini kuhusiana na
masuala ya uwekezaji.
Mwaipopo alisema pamekuwepo na mafanikio mazuri
katika utekelezaji wa shughuli za uzalishaji wa mgodi hali iliyochangiwa na
mahusiano mazuri yaliyopo kati ya uongozi wa mgodi, serikali na jamii yenyewe.
“Sisi tunaamini iwapo hali hii ya mahusiano
mazuri itaendelea, ni wazi tutaongeza uzalishaji zaidi na hivyo kuwezesha
kupatikana kwa fedha nyingi kwa upande huu wa ada ya ushuru wa huduma tunaolipa
kila mwaka, tunaomba ushirikiano uliopo uendelezwe kwa pande zote husika,”
alieleza Mwaipopo.
Post a Comment