Mwenyekiti wa kamati, Mary Nagu akiongozana na wajumbe wake kukagua eneo la mradi wa ujenzi wa tangi la maji katika mji wa Mhunze, kushoto ni kaimu mkurugenzi wa KASHWASA, Lawrance Wasala. |
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA)
imepongezwa kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha huduma ya maji kutoka mradi
wa Ziwa Victoria inasambazwa na kuwafikia wananchi wengi mkoani Shinyanga na mkoa
jirani wa Tabora.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo iliyokuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Shinyanga kutembelea na kukagua utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji inayotekelezwa na KASHWASA.
Wakizungumza katika kikao cha majumuisho baada
ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na KASHWASA, wabunge hao walielezea
kuridhishwa na kazi nzuri inayofanyika ya usambazaji wa maji katika wilaya za
Shinyanga na Kishapu hali ambayo imewezesha wananchi wengi kupata maji kwa
urahisi.
Wabunge hao walisema kazi inayofanywa na
KASHWASA inaonesha jinsi gani serikali ya awamu ya tano inavyotekeleza kwa
vitendo ahadi ilizozitoa kwa wananchi kuhusiana na suala zima la kuwaondolea
kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili katika maeneo yao.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya wajumbe wake,
mwenyekiti wa Kamati, Mary Nagu alisema kamati yake imeridhishwa na kazi
zinazotekelezwa na KASHWASA ambazo zitawezesha wananchi wengi hivi sasa kupata
huduma ya maji ya uhakika tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.
“Kwa kweli mimi na wenzangu tumeridhishwa na
kazi nzuri inayofanywa na wenzetu wa KASHWASA, ni wazi wanatekeleza kikamilifu
maelekezo ya serikali, na sisi wabunge hatuna budi pia kuipongeza serikali kwa
jinsi inavyotekelezwa kwa vitendo suala la usambazaji wa maji kwa wananchi wetu
hasa walioko maeneo ya vijijini,”
“Mradi huu wa maji kutoka Ziwa victoria ni
mradi uliobuniwa miaka mingi iliyopita, awali ulikumbana na vikwazo vingi
serikali ilipotaka kuutekeleza, nakumbuka tangu mimi nikiwa waziri wa HESAWA
iliyokuwa ikishughulikia uchimbaji wa visima vifupi, tulipendekeza kujengwa kwa
mradi huu, hatimaye umekamilika na unafanya kazi,” alieleza Nagu.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa
upanuzi wa mtandao wa usafirishaji maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika mji
wa Kishapu kupitia mji mdogo wa Maganzo na mgodi wa Almasi wa Mwadui, Kaimu
mkurugenzi wa KASHWASA, Mhandisi Laurence Wasala alisema mradi huo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 14.46.
“Kutokana na hali ya upatikanaji wa fedha
kutoka serikalini na makubaliano kati ya KASHWASA na mgodi wa Almasi wa Mwadui,
mradi ulipangwa kutekelezwa katika awamu mbili, awamu ya kwanza ilihusu ujenzi
wa bomba kutoka Old Shinyanga hadi mgodi wa Almasi Mwadui,”
“Hii ilifanyika kutokana na makubaliano ya
kisheria yaliyofikiwa kati ya KASHWASA na uongozi wa mgodi wa Almasi wa Mwadui,
awamu hii ilipangwa kukamilika ndani ya muda wa miezi mitano tangu kuanza kwa
utekelezaji, mradi mzima unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi 14.46
bilioni, sawa na dola za kimarekani 6.62 milioni,” alieleza Wasala.
Mbali ya mradi wa usambazaji maji wilayani
Kishapu pia KASHWASA itapeleka maji katika manispaa ya Tabora na miji midogo ya
Igunga, Nzega, Kagongwa, Isaka na Tinde ambapo mradi huo umepangwa kuanza
kutekelezwa mwezi Mei, 2017.
Baadhi ya miradi iliyotembelewa na kamati hiyo ya
bunge ni pamoja na kuangalia ujenzi wa tangi kubwa linalojengwa katika mji wa
Kishapu litakalokuwa na meta za ujazo 1,200 ambapo kazi hiyo imekamilika kwa
asilimia 70 mpaka hivi sasa.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge, Mary Nagu akiteremka kutoka juu ya tangi linalojengwa wilayani Kishapu kwa ajili ya kusambaza maji katika mji wa Mhunze na vijiji vya jirani. |
Wajumbe wa kamati ya bunge ya kudumu wakisikiliza maelezo kuhusiana na mradi wa usambazaji maji katika kijiji cha Bunambiyu wilayani Kishapu. |
Pia wajumbe walitembelea kuangalia en.eo ambalo
mtandao wa bomba kutoka chanzo cha maji katika kijiji cha Ihelele wilayani
Misungwi mkoani Mwanza kinapounganishwa kupeleka maji katika mji wa Shinyanga
na wilaya ya Kishapu ambapo pia walitembelea mradi wa maji katika kijiji cha
Bunambiyu wilayani Kishapu.
Post a Comment