Jengo la Zahanati linaloombwa na wanakijiji cha Mweseme kutoka uongozi wa Kanisa la Anglikana. |
Jiwe la msingi liliwekwa na Rais wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi |
Baadhi ya vifaa vilivyomo katika vyumba vilivyotelekezwa baada ya kufungwa kwa zahanati hiyo mwaka 2009. |
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro (kushoto) na diwani wa kata ya Solwa, Awadhi Aboud wakikagua jengo linaloombwa na wanakijiji ili liendelee kutumika kutoa huduma za Zahanati ya kijiji. |
MKUU wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro
ametoa siku 28 kwa viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Kanisa la
Anglikana na wa Serikali ya Kijiji cha Mwiseme wilayani humo kumaliza mgogoro
uliopo kati yao kuhusiana na Zahanati iliyofungwa ili iweze kuanza kazi.
Matiro ametoa agizo hilo baada ya kupokea
malalamiko ya wakazi wa kijiji cha Mwiseme waliolalamikia kitendo cha kijiji
chao kukosa huduma za Zahanati tangu mwaka 2009 baada ya uongozi wa Kanisa la
Anglikana kuamua kuamua kuifunga zahanati hiyo kwa madai ya kuachana na utoaji
wa huduma hiyo.
Wakisoma risala yao mbele ya mkuu huyo wa
wilaya wanakijiji hao walidai kitendo cha kukosa huduma za zahanati kijijini
hapo, kimesababisha walazimike kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu
katika vijiji jirani ambako kuna umbali mrefu.
Hata hivyo walisema tatizo kubwa limekuwa
likijitokeza pale inapotokea shida ya akinamama wajawazito wanaotaka kujifungua
kulazimika kukimbizwa hospitali zilizopo mbali na kijiji chao ambapo baadhi ya
wanaopata shida wakati wa kujifungua huwa katika hatari ya kupoteza maisha.
Akifafanua kuhusiana na kufungwa kwa zahanati
iliyokuwa ikitoa huduma hapo awali, diwani wa kata ya Solwa, Awadhi Aboud
alisema mwaka 1993 wanakijiji cha Mwiseme walikubali kutoa eneo la ardhi lenye
ukubwa wa ekari zaidi ya 40 kwa uongozi wa kanisa la Anglikana kwa ajili ya
ujenzi wa zahanati pamoja na majengo mengine ya shughuli za kijamii.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro akiwahutubia wanakijiji baada ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili. |
Wanakijiji wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga |
Risala ya wanakijiji ikisomwa mbele ya mkuu wa wilaya. |
Mwanakijiji cha Mwiseme akielezea kero katika mkutano wa mkuu wa wilaya. |
Aboud alisema pamoja na kutoa eneo hilo pia
wanakijiji walishiriki kwa kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo kwa lengo la
kuondoa tatizo la kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika
vijiji jirani ambapo walikamilisha
ujenzi na jengo hilo lilizinduliwa rasmi na Rais wa awamu pili, Alhaj Ali
Hassan Mwinyi mwaka 1993.
Hata hivyo alisema Zahanati hiyo ilifungwa baada ya uongozi wa kanisa la Anglikana kushindwa kutimiza masharti ya uendeshaji wake na hivyo wizara ya afya iliagiza ifungwe na hivyo wanakijiji kukosa eneo la kupatiwa huduma za matibabu.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya tatizo ni kwamba
baada ya wenzetu kusitisha huduma za uendeshaji wa zahanati hii mnamo mwaka
2009, wamekataa katakata kuruhusu jengo lao kuendelea kutumika tena kwa ajili
ya kutoa huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hiki,"
"Kwa niaba ya wananchi hawa tunaomba utusaidie
kutuombea kwa viongozi wa kanisa hili ili wakubali kutukabidhi jengo hili na liendelee kutumika kutoa huduma kama ilivyokuwa zamani chini ya usimamizi wa serikali ya kijiji na uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,” alieleza diwani Awadhi.
Diwani wa kata ya Solwa Awadhi Aboud akitoa maelezo mbele ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga. |
Kwa upande wake mkuu wa wilaya alielezea
masikitiko yake kuona wanakijiji wakitaabika kutokana na ukosefu wa zahanati wakati
lipo jengo lililokamilika kwa kila eneo kwa ajili ya utoaji wa huduma za tiba
na lingeondoa usumbufu wa wanakijiji kufuata huduma za matibabu maeneo mengine
nje ya kijiji hicho.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa wilaya aliwaagiza
viongozi wa serikali ya kijiji, halmashauri ya wilaya na wale wa kanisa la
Anglikana kukaa chini na kukamilisha taratibu walizokuwa wamepanga
kuzikamilisha kwa lengo la kurejesha jengo hilo mikononi mwa wananchi na liweze
kutumika kwa kutoa huduma za zahanati.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya amewashauri
wakazi wa kijiji cha Mwiseme kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ambao
utamuwezesha mkuu wa kaya na wategemezi wake sita kupatiwa huduma za matibabu
kwa gharama ya shilingi 10,000 kwa kipindi cha mwaka mzima.
Aidha alisema fedha itakayokusanywa chini ya
mfuko wa bima ya afya itasaidia pia kununulia dawa na vifaa tiba katika
zahanati hiyo ambapo serikali kwa upande wake itakuwa ikichangia asilimia 50 ya
fedha zitakazokuwa zimechangwa na wahusika wa mfuko huo.
Wakati huohuo mkuu wa wilaya ya Shinyanga
amewaagiza viongozi wa serikali ya kijiji cha Mwesemi na walioko katika kamati
ya TASAF III ya kijiji kuangalia uwezekano wa kumsaidia mlemavu mkazi wa kijiji
hicho, Gideon Shija aliyemfuata na kulalamika akidai aliondolewa kwenye mpango
huo wakati yeye ni mlengwa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akimsikiliza mmoja wa walemavu katika kijiji cha Mwiseme, Gideon Shija aliyelalamikia kuenguliwa kwenye Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III). |
Matiro alisema ni vizuri wahusika wanaosimamia
utaratibu wa kuandikisha watu wanaostahili kupatiwa ruzuku hiyo chini ya Mpango
wa kunusuru kaya maskini wakawa makini wanapoteua wanufaika wa mpango huo
badala ya kuandikisha watu wenye uwezo na wasio na sifa.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mkuu huyo alijikuta
akikwama kuendelea na mikutano ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi katika
kijiji cha Manghu kata ya Salawe baada ya kukuta uongozi wa serikali ya kijiji
hicho haukualika wananchi kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa hadhara na
hivyo kulazimika kukatisha ziara yake.
Post a Comment