Mtuhumiwa Neema Japhet (23) akipanda ndani ya gari la polisi tayari kwa kupelekwa kituo cha polisi mjini Shinyanga.
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mkazi wa kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga, Neema Japhet (23) akituhumiwa kwa kosa la kujifungua mtoto kisha kumtupa katika choo cha kanisa la AIC –Tanzania Kitangiri.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Elias Mwita alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumanne ya Januari 24, 2017 saa 3.00 asubuhi kufuatia taarifa zilizotolewa na wananchi waliomtilia shaka baada ya kubaini hakuwa na ujauzito aliokuwa nao hapo awali.

Akifafanua Kamanda Mwita alisema Januari 20, huko katika kanisa la AIC Tanzania Kitangiri, wananchi walibaini kutupwa chooni kwa mtoto mwenye umri wa siku moja ambapo juhudi zilifanyika na kufanikiwa kumuopoa akiwa hai na kukimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza katika kujaribu kuokoa uhai wake.

Mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi akijaribu kuwazuia wananchi wenye hasira kuinga ndani ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kitangiri kwa lengo la kumshambulia mtuhumiwa anayedaiwa kutupa chooni kichanga chake muda mfupi baada ya kujifungua.
Hata hivyo alisema kichanga hicho kilifariki asubuhi siku ya pili kilipokuwa kikiendelea kupatiwa matibabu  na mwili wake ulichukuliwa na viongozi wa kanisa la AIC Kitangiri walioandaa taratibu za mazishi na kukizika.

Akifafanua alisema baada ya kukamatwa na kuhojiwa alikiri na kudai hakufanya kitendo hicho kwa makusudi na kwamba ilitokea kwa bahati mbaya wakati alipokwenda katika chooni kwa lengo la kujisaidia ambapo mtoto alitoka na kutumbikia chooni.  Hata hivyo alishindwa kueleza kwa nini hakutoa taarifa kwa viongozi.




Juu mtuhumiwa Neema Japhet akiwa chini ya ulinzi ndani ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kitangiri , chini wananchi wakibanana kwenye dirisha kumchungulia na kutaka kumfahamu mtuhumiwa huyo.

Baadhi ya wananchi wakionesha furaha yao baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa kutupa mtoto chooni.

Gari la Polisi Shinyanga likijiandaa kumpakia mtuhumiwa kumpeleka katika kituo kikuu cha Polisi mjini Shinyanga.

Mchungaji wa kanisa la AIC Kitangiri, David Kazimoto alisema baada ya tukio la kuokotwa kwa kichanga katika choo cha kanisa lake walitoa wito kwa waumini wote wa kanisa kufanya uchunguzi na kupeleleza kwa kina ili waweze kumbaini mtu aliyefanya kitendo hicho kiovu.
 
“Tulisikitishwa na kitendo kilichofanywa na ndugu yetu huyu, kile kichanga tulikiokoa ndani ya shimo la choo, lakini kutokana na hali aliyokuwa nayo hakuweza kuishi pamoja na juhudi za madaktari, tulitoa wito kwa waumini wetu wafanye upelelezi kuweza kumbaini mtuhumiwa, kweli walifanikiwa na leo hii (juzi) wamemkamata,” alieleza mchungaji Kazimoto.
 
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top