Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoani Shinyanga, Lydia Kwesigabo akiwasilisha mada kwa washiriki juu ya Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 |
Washiriki wa warsha wakifuatilia kwa makini mada zinazowasilishwa, wa kwanza mwenye miwani ni katibu wa TAS mkoani Shinyanga, Lazaro Anaeli. |
CHAMA cha Watu wenye Ualbino (TAS) mkoani Shinyanga
kimeiomba serikali kutekeleza agizo lake lililotolewa mwaka 2012 likielekeza
watu wenye ulemavu kupatiwa bure huduma za matibabu katika zahanati, vituo vya
afya na hospitali za serikali.
Ombi hilo limetolewa na washiriki wa warsha ya
siku moja iliyoandaliwa kwa ajili ya kubadilishana mawazo kati ya watu wenye
ualbino, wazazi na walezi wao juu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo
sambamba na kuelimishana juu ya haki wanazostahili kupatiwa.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo kutoka wilayani
Kishapu, Joseph Masanja alihoji kitendo cha baadhi ya watoa huduma katika
zahanati na hospitali za serikali kuwataka walemavu kuchangia huduma za
matibabu wakati kuna waraka wa serikali unaoagiza watibiwe bure.
Masanja alisema walemavu wengi hawana uwezo hivyo
wanashindwa kuchangia huduma na mara nyingi baadhi yao huondoka vituoni bila ya
kupatiwa matibabu kutokana na kutokuwa na fedha.
Mbali ya matibabu pia walielezea masikitiko yao ya
kukatiliwa kuajiriwa katika maeneo mengi kinyume na maelekezo yaliyotolewa na
serikali ikielekeza eneo lolote la kazi asilimia tatu ya wafanyakazi wake wawe
ni watu wenye walemavu hata hivyo waajiri hawatekelezi agizo hilo hata kama
walemavu wanakidhi vigezo vya kazi iliyotangazwa.
Kwa upande wake Ofisa Mipango kutoka TAS makao makuu,
Severin Edward alikiri kuwepo kwa agizo la walemavu kutibiwa bure lililotolewa
kwa waraka wenye Kumb. Na. AB.24/280/01 wa Julai 13, 2012 na kusainiwa na
aliyekuwa katibu mkuu wa TAMISEMI wakati huo, H. A. Kattanga.
Washiriki wakiwa makini katika kufuatilia mada zinazowasilishwa. |
“Waraka huo ulisambazwa kwa makatibu tawala wote wa
mikoa nchini ukiwa na kichwa cha habari; Kusimamia masuala mbalimbali
yanayohusiana na watu wenye ulemavu ambapo waliagiza kuhakikisha walemavu
wanapokwenda kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo
chini ya serikali hawatozwi huduma za matibabu,” alieleza Edward.
Aliendelea kufafanua kuwa mbali ya waraka huo wa
serikali pia Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa kimataifa wa
Haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD) na hata sheria namba tisa ya mwaka 2010 ya
watu wenye ulemavu na Sera ya afya ya Taifa vinaelekeza walemavu kutibiwa bure.
Washiriki wa warsha hiyo iliyohudhuriwa pia na
mshiriki mwenye ualbino kutoka nchini Uganda, Edith Nabalanga wameiomba
serikali ihakikishe itoe msimamo wake ili kuwezesha sera na sheria mbalimbali
zinazotungwa hapa nchini zinatekelezwa na kuondoa kupishana kwa matamko
yanayotolewa.
Maofisa wa polisi kutoka kitengo cha dawati la jinsi walikuwa ni miongoni mwa washiriki wa warsha hiyo. |
Ofisa Habari kutoka TAS Makao Makuu, Josephat Tonner akisisitiza jambo kwa washiriki. |
Hata hivyo kwa upande wake Ofisa Habari kutoka TAS
Makao Makuu, Josephat Tonner aliwahadharisha washiriki hao kuhusiana na suala
la kutegemea kusaidiwa katika kila jambo hata kwa mambo wanayoyaweza na
kuwataka waache tabia ya kujinyanyapaa wao wenyewe na badala yake washirikiane
na jamii katika masuala ya kimaendeleo.
Post a Comment