Mmoja wa wahanga wa viboko vya walinzi wa Jadi (Sungusungu), John Kitumbo mkazi wa kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilayani Shinyanga akionesha majeraha aliyoyapata baada ya kucharazwa viboko. |
Mkazi wa kijiji cha Welezo ambaye alijeruhiwa kwa kipingo cha sungusungu. |
KATIKA
hali isiyotarajiwa wakazi kadhaa wa kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilayani
Shinyanga wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao huku wengine wakipoteza
fahamu baada kushambuliwa kwa vipigo vya fimbo na kundi la walinzi wa jadi
sungusungu zaidi ya 800.
Tukio
hilo lisilokuwa la kawaida limetokea Desemba 10, mwaka huu saa 4.00 asubuhi
huko katika kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilayani Shinyanga baada ya kutokea
vurugu zilizosababisha mapigano kati ya wanakijiji na walinzi wa jadi kutoka vijiji
jirani vinavyozunguka kijiji hicho.
Kufuatia
tukio hilo wanakijiji wa wamemkataa mwenyekiti wao wa serikali ya kijiji Salumu
Shabani mbele ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro anayetuhumiwa kula
njama za kuwaalika sungusungu hao waliowadhalilisha kwa kuwacharaza viboko huku
wakipewa adhabu za kupiga pushapu bila kujali wanawake wenye ujauzito.
Wakizungumza
katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Josephine Matiro, wanakiji hao walidai chanzo cha wao kuadhibiwa na kujeruhiwa
baada ya kucharazwa viboko huku wengine wakipoteza fahamu kuwashinikiza
viongozi wao kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji.
Pia
walisema viongozi wao wa sungusungu kijijini hapo walishindwa kutekeleza agizo
la mkutano mkuu wa kijiji ulioagiza wanakijiji wagawane mpunga ambao hukusanywa
kutoka kwa watu wanaolipishwa adhabu ya “mchenya” baada ya kufanya makosa
madogo madogo kijijini.
Wakifafanua
walisema hivi karibuni walifanya mkutano mkuu wa kijiji ambapo moja ya maazimio
yaliyotolewa ni viongozi wa serikali ya kijiji na walinzi wa jadi kuandaa
taarifa ya mapato na matumizi ikiwemo kupanga utaratibu wa jinsi wanakijiji
watakavyogawiwa mpunga uliokwisha kusanywa zaidi ya magunia 150.
Wananchi wakitoa malalamiko yao mbele ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro baada ya kucharazwa viboko na sungusungu. |
Kaimu mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, Janeth Kulobone aliyechaguliwa baada ya kuenguliwa kwa mwenyekiti wa zamani Salumu Shabani. |
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Welezo, Salumu Shabani ambaye amekataliwa na wananchi wake. |
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro. |
Hata
hivyo siku iliyopangwa viongozi hao hawakuweza kujitokeza katika mkutano
uliokuwa umeitishwa na badala yake waliendesha vikao vya ndani wakishirikiana
na viongozi wa walinzi wa jadi (sungusungu) kitu ambacho wanakijiji
hawakukiafiki na hivyo kuchukua hatua ya kuukataa uongozi mzima wa sungsungu.
“Baada
ya kubaini viongozi wetu wanatuzungusha na hawataki kutekeleza maazimio ya mkutano
mkuu, wanakijiji waliamua kuwavua madaraka viongozi wa sungusungu, hali ambayo
wenzetu hawakuiafiki, na hivyo walikula njama na viongozi wa sungusungu ngazi
ya kata na tarafa ili kutukomoa,”
“Tulipowavua
madaraka viongozi wa sungusungu, Sungusungu ngazi ya kata na tarafa walipitisha
azimio la kijiji chetu kutengwa, tulitengwa na baada ya muda tukaombwa
tuchangie shilingi 5,000 kila kaya ili tuondolewe adhabu tuliyopewa, kiasi cha shilingi milioni moja na laki tatu kilikusanywa, tulinunua
ng’ombe sita na mbuzi kadhaa kwa ajili ya kazi hiyo,” alieleza John Kitumbo.
Kitumbo
aliendelea kufafanua kuwa baada ya kukamilisha mahitaji yote kwa ajili ya
shughuli za kutawadhwa upya kuwa sungusungu, mkutano uliitishwa na viongozi wa
jadi kutoka ngazi ya kata, tarafa na wilaya ndiyo waliohusika kusimamia kazi
hiyo kwa lengo la kijiji chao kuondolewa adhabu ya kutengwa.
Hata
hivyo siku ya kufanyika kwa shughuli iliyokuwa imekusudiwa, walishangaa kuona
viongozi wao wakiibuka na agenda tofauti na iliyokuwa imepangwa kufanyika
ambapo kikao hicho kiligeuka cha kuwataja watu wahalifu, wizi na wakata mapanga
vikongwe.
“Ajabu
siku ya mkutano rasmi tulishangaa kugeuziwa kibao, tukiwa tunajiandaa
kutawadhwa upya, ghafla kamanda wa sungusungu wa wilaya, Kulwa Masanja alianza
kuita majina ya watu na kuwataka wajitokeze mbele ya mkutano ambapo walielezwa
wao ni wahalifu na wanatakiwa kujikomboa kwa shilingi 200,000 kila mmoja,”
“Suala
la kutaja majina ya wahalifu haikuwa agenda yetu siku hiyo, baadhi ya watu
waliotuhumiwa na kutajwa waliitwa mbele kisha walichapwa viboko na kutakiwa
kuondoka mkutanoni vinginevyo walipe
shilingi 200,000 ili wajikomboke, mmoja alilipa lakini mtu wa nne aligoma,
akapigwa fimbo, aligoma na kumkwida shati mpigaji, hapo ndipo vurugu
zilipoanzia,” alieleza Janeth Kulubone.
Kutokana
na hali hiyo mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alitoa agizo la
kusimamishwa uongozi mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Welezo, Salumu Shabani na kuagiza
kufanyika uchunguzi dhidi ya tuhuma zote anazotuhumiwa na kuivunja kamati nzima
ya sungusungu ya kijiji ambapo wanakijiji walichagua kamati mpya.
“Nimesikiliza
maelezo yenu kwa kina, nimebaini chanzo cha vurugu hizi ni viongozi wenu
kukiuka maadili ya uongozi, sasa na mimi naunga mkono azimio lenu la kumkataa
mwenyekiti wa serikali ya kijiji, asimame na uchunguzi wa tuhuma zake ufanyike,
na hapahapa chagueni mwenyekiti wa muda, na kamati mpya ya sungusungu,” alieleza
Matiro.
Mkuu huyo aliongeza kueleza, “.....Wananchi wamenyanyaswa, wameumizwa kwa sababu ya viongozi wa
sungusungu na serikali ya kijiji, sasa tunawaondoa wote, hii nchi ni ya amani, haiwezekani
watu wachache waharibu amani yetu, sungusungu kazi yenu siyo kunyanyasa wananchi
hii iwe mara ya mwisho, eleweni sehemu yoyote yenye vurugu hapawezi kuwa na maendeleo.”
Aidha Matiro amekemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji kufuja mali za wananchi na pale wanapotakiwa kusoma taarifa ya mapato na matumizi hushindwa kufanya hivyo wakiogopa kuumbuliwa na kueleza kuanzia sasa ofisi yake itafuatilia viongozi wote wasiopenda kutekeleza taratibu za kazi na kuwachukulia hatua.
Askari wa Jeshi la Polisi akigawa karatasi kwa ajili ya kupiga kura za siri kufichua watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu. |
Katika hatua nyingine wanakijiji hao waliamua kupiga kura za siri ili kuwataja watu wanaotuhumiwa kwa vitendo vya uhalifu mbalimbali ikiwemo mauaji ya vikongwe na kumuomba mkuu wa wilaya kutoyatambua majina ya awali yaliyokuwa yameandaliwa na viongozi wa sungusungu wakishirikiana na mwenyekiti wa serikali ya kijiji.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Welezo, Salumu Shabani akiondoka eneo la mkutano baada ya kukataliwa na wanakijiji. |
Post a Comment