Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Alhaj Saad Kusilawe akifungua rasmi kikao cha siku moja cha Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Shinyanga. |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani
Shinyanga kimewapongeza viongozi na watendaji wa Jumuiya zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kipindi cha
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwezesha CCM kupata ushindi wa kishindo kwa kunyakua
majimbo yote sita ya uchaguzi mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa na katibu wa
CCM mkoani Shinyanga, Alhaji Saad Kusilawe alipokuwa akifungua kikao cha siku
moja cha Baraza Kuu la Jumuiya ya wazazi la mkoa ikiwa ni moja ya vikao vyake vya kikatiba.
Alhaji Kusilawe alisema juhudi kubwa
iliyofanywa na viongozi na watendaji mbalimbali wa Jumuiya za chama katika kuwanadi wagombea
wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ziliwezesha ushindi kwa wagombea wa CCM.
Katibu wa CCM mkoa akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la wazazi mkoani Shinyanga. |
Wajumbe wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi. |
“Ndugu zangu naomba nitumie fursa hii leo
(jana) kuwashukuru viongozi na wanachama wote wa Jumuiya zetu kwa kazi nzuri
mliyoifanya kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu hapa nchini na kukiwezesha
chama chetu kupata ushindi wa kishindo hasa ngazi ya majimbo ya ubunge,”
“Kwa hapa kwetu Jumuiya ya wazazi mlikuwa
mstari wa mbele kwenye kazi hiyo, mlifuatiwa na wanawake (UWT) na vijana
(UVCCM), ukweli mchango wenu ulionekana na ilionesha wazi jumuiya yenu
sasa imeanza kuimarika ikilinganishwa na siku za nyuma, tunakushukuruni sana kwa
kazi hiyo,” alieleza Alhaji Kusilawe.
Akifafanua
alisema jumuiya za CCM ni
nguzo muhimu ndani ya chama na kwamba moja ya kazi zake ni kurahisisha
kufikiwa kwa urahisi kwa jamii mitaani ambako ndiko yaliko makundi ya
makubwa ya vijana, wanawake na wazee na hivyo kuwaeleza
kwa ufasaha mipango na sera mbalimbali za chama.
“Kwa hali hiyo basi niwaombe viongozi wa
Jumuiya hii ya wazazi hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu kwa kufanya kazi
usiku na mchana kuhakikisha jumuiya inaendelea kuimarika zaidi, na tangu sasa anzeni
kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ili kuiwezesha jumuiya ijitegemee,”
“Tokeni ofisini nendeni kwa wanachama
huko mitaani, kahimizeni suala la uhai wa chama, hasa katika suala la ulipaji
wa ada, waelezeni wanachama wa CCM na jumuiya zake kuwa mwanachama hai ni yule
anayelipa ada zake kwa mujibu wa katiba, lakini pia wahimizeni waanzishe miradi
kwa ajili ya jumuiya yao,” alieleza.
Kikao kinaendelea kulia ni Katibu wa wazazi mkoa, Gulisha Mfanga. |
Katibu wa mkoa akitoa maneno ya utangulizi kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao. |
Kikao kinaendelea. |
Katika hatua nyingine Alhaji Kusilawe
ametoa wito kwa wanachama wa CCM na Jumuiya zake kuanza maandalizi mapema kwa
ajili ya uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani katika kata ya Isagenhe wilayani
Kahama mkoani Shinyanga unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwakani.
Alisema CCM lazima ihakikishe kata hiyo
inaendelea kubaki mikononi mwake baada ya kifo cha aliyekuwa diwani wake, marehemu Andrea Shimo na
kwamba kila kiongozi wa chama au wa jumuiya aelekeze nguvu zake kwenye kata
hiyo pale kampeni zitakapozinduliwa rasmi.
“Tusiudharau uchaguzi huu eti ni uchaguzi
mdogo, lazima tuanze maandalizi mapema na tujipange vizuri ili tuweze kupata
ushindi na kuikamata tena kata hiyo, kumbukeni vyama vyote vya siasa vitaweka
wagombea wake, sasa sisi tusimame imara kuhakikisha kata hiyo haipotei,”
alieleza Alhaji Kusilawe.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya
wazazi mkoani Shinyanga, Willy Mzava alimuhakikishia Alhaji Kusilawe kwamba
Jumuiya hiyo itaendelea kusimama imara muda wote katika kunadi sera za chama ili CCM
iendelee kuwa imara ikikamata dola ambapo alitoa wito kwa wajumbe kujiandaa vizuri kwa uchaguzi
wa ndani ya chama mapema mwakani.
Post a Comment