Meneja Tawi la CRDB Shinyanga, Said Pamui akitoa taarifa kwa mgeni rasmi juu ya mpango wa kuwakopesha pikipiki kwa masharti nafuu vijana wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki (bodaboda) kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro.
BENKI ya CRDB Tawi la Shinyanga imezindua mpango maalumu wa utoaji mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana waendesha pikipiki za kusafirisha abiria (bodaboda) manispaa ya Shinyanga ili kuwasaidia waweze kujiajiri wenyewe.


Mpango huo unatarajiwa kuwakomboa vijana wengi wanaofanya biashara hiyo hivi sasa kwa kutegemea pikipiki za kukodi kutoka kwa watu wengine na kulazimika kuwapelekea wamiliki sehemu kubwa ya mapato wanayopata kwa siku.

Akitoa taarifa juu ya uanzishwaji wa mpango huo wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi vijana wanne wa awali waliokopeshwa mkopo wa pikipiki aina ya SANLG, meneja wa Tawi la CRDB Shinyanga, Saidi Pamui alisema ni matumaini ya benki yake mikopo hiyo itakuwa ni mkombozi kwa vijana wanaofanya biashara ya bodaboda.

“Tulipokea maombi kutoka kwa viongozi wa kikundi cha Umoja wa wamiliki na madereva wa pikipiki za kukodisha manispaa ya Shinyanga (SHIMODU) wakitaka tuwasaidie kuwapatia fedha kwa ajili ya kununulia pikipiki zao wenyewe badala ya kufanya kazi kwa kutumia za kukodi kutoka kwa watu wengine,”

“Katika maombi yao walisema wamekuwa wakifanya biashara hiyo lakini hawaoni faida wanayoipata kutokana na kulazimika kuwakabidhi wamiliki wa pikipiki wanazokodi sehemu kubwa ya kipato wanachokipata kwa siku, tulikaa na tukatafakari, tukaona tuanzishe utaratibu wa kuwakopesha kwa masharti nafuu,” alieleza Pamui.


Meneja Pamui akitoa hotuba yake mbele ya mgeni rasmi, mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa Umoja wa wamiliki na madereva wa pikipiki za kukodisha manispaa ya Shinyanga (SHIMODU, Mwito Mniko na Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Alfred Nkomoi.
Hata hivyo pamoja na kukubali kuanzisha mpango huo, Pamui alisisitiza umuhimu wa vijana kabla ya kuanza kuendesha pikipiki kwanza wapitie chuo cha ufundi VETA kwa lengo la kujifundisha udereva na kuzielewa vizuri sheria za usalama barabarani ili kazi yao iwe na ufanisi mzuri na endelevu.

“Leo (juzi) tunakabidhi pikipiki nne ambazo ni mkopo wenye thamani ya shilingi milioni tisa, zimelipiwa kila kitu ikiwemo bima ya ajali na bima ya maisha, hivyo kijana akitoka nayo hapa anaingia kazini moja kwa moja,"

"Riba ya mkopo huu wa pikipiki ni asilimia 18  kwa miezi 12, yaani mwaka mmoja na marejesho ya mwezi ni shilingi 177,000, tunaamini wote watazingatia masharti ya mkopo huu, na wataurejesha kwa wakati, kwa vile mapato ya siku waliyopaswa kupeleka kwa mmiliki sasa yatakuwa ni marejesho ya mkopo,” alieleza Pamui.

Mwenyekiti wa SHIMODU, Mwita Mniko akitoa hotuba ya shukrani kwa uongozi wa CRDB kwa kukubali kutoa mikopo ya pikipiki yenye masharti nafuu kwa wanachama wake.

Awali katika taarifa yake mwenyekiti wa SHIMODU, Mwita Mniko aliushukuru uongozi wa CRDB Tawi la Shinyanga kwa kukubali ombi lao na kwamba hatua hiyo itawasaidia vijana wengi walioko katika biashara ya bodaboda kujikomboa kutoka katika utumwa wa kuwatumikia watu wengine.

Hata hivyo aliomba serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo mjini Shinyanga kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili waweze kupata fedha za kutosha zitakazotumika kama dhamana ya mkopo kwa kundi la vijana wengine zaidi ya 65 ambao ni wanachama wa SHIMODU wanaohitaji pia kupatiwa mkopo wa pikipiki.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, mkuu wetu wa wilaya, Josephine Matiro, kwa niaba ya wanachama wa SHIMODU naomba niwashukuru wenzetu wa CRDB kwa kutushika mkono sisi vijana waendesha pikipiki, ukweli ni kwamba mkopo huu ni mkombozi kwetu, hata hivyo wahitaji bado ni wengi, na chama hakina fedha za dhamana ya mkopo,”

“Moja ya masharti ya mkopo huu ni chama kuweka dhamana ya shilingi 200,000 kwa kila mkopaji, chama chetu bado ni kidogo, wahitaji ni wengi, hivyo kwa hawa wanne wa leo tayari tumeweka dhamana ya shilingi 800,000 kwa hali hii tunaomba serikali au wadau wengine watuchangie ili kutunisha mfuko wetu,” alieleza Mniko.


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akikabidhi rasmi pikipiki nne aina ya SNGL kwa vijana wa kwanza kutoka kikundi cha SHIMODU waliokopeshwa pikipiki kwa masharti nafuu.




Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mbali ya kuipongeza benki ya CRDB kwa kuanzisha mpango huo alisema hatua ya mpango huo mbali ya kuwaondoa katika dimbwi la utumwa kutokana na kukodi pikipiki za watu wengine lakini pia unaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Tunawapongeza wenzetu wa CRDB kwa kubuni utaratibu huu mzuri, hawa ni wadau wakubwa wa maendeleo hapa nchini, mpango waliouanzisha utawapunguzia vijana wetu adha ya kukopa mitaani kwa riba kubwa au kutumikishwa na watu wengine kwa kipato kidogo,”

“Ni matumaini yangu kuwa vijana mtaitumia vizuri fursa hii kwa kukopa na kulipa madeni yenu kwa wakati kama mlivyokubaliana, lakini pia niwaombe mzingatie sheria za usalama barabarani katika kufanya kazi zenu za kila siku, pamoja na kulipa kodi mbalimbali za serikali, na msibebe abiria zaidi ya wale wanaohurusiwa kisheria,” alieleza Matiro.

Kwa upande mwingine mkuu huyo wa wilaya alisisitiza umuhimu wa vijana kujiunga kwenye vikundi kama walivyojiunga vijana hao wa bodaboda ambao wameanzisha kikundi chao cha Umoja wa wamiliki na madereva wa pikipiki za kukodisha (SHIMODU) ili iwe rahisi kwao kusaidiwa na serikali ama taasisi nyingine za kifedha.




Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top