Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga akimkaribisha Naibu waziri Luhaga Mpina mkoani Shinyanga ambapo pia alisoma taarifa fupi ya mkoa.

NAIBU waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina amewapongeza viongozi wa serikali wilayani Shinyanga kwa jinsi wanavyosimamia kikamilifu suala la usafi na utunzaji wa mazingira na kuufanya mji wa Shinyanga kuonekana katika hali ya usafi.


Naibu waziri Luhaga Mpina akikagua ghuba eneo la Soko la Nguzo nane Manispaa ya Shinyanga.

Naibu waziri Mpina akizungumza na sehemu ya wafanyabiashara wa Soko la Nguzo nane - Shinyanga, kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro.







Naibu waziri Mpina akikagua maeneo ya  Soko la Nguzo Nane wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya mazingira katika manispaa ya Shinyanga





Hapa ni katika machinjio ya Shinyanga mjini.
Mpina alitoa pongezi hizo juzi baada ya kumaliza ziara siku mbili ya kuutembelea mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kukagua hali ya usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ikiwemo viwanda vikubwa vinavyomilikiwa na wawekezaji wa kigeni.

Alisema baada ya kutembelea maeneo ya mji wa Shinyanga ameridhishwa na hali ya usafi aliyoiona na kuwapongeza viongozi wake chini ya usimamizi wa mkuu wa wilaya hiyo, Josephine Matiro ambapo alisema viongozi wa maeneo mengine wanapaswa kwenda kujifunza katika wilaya hiyo.

Alisema katika ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya mji huo ikiwemo machinjio ya manispaa, maghuba na madampo kunakohifadhiwa taka ngumu amekuta hali ya usafi inaridhisha tofauti na maeneo ya wilaya nyingine alizokwisha zitembelea.

“Kwa kweli nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wa serikali kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhusu suala zima la usafi, nimeridhishwa na hali ya usafi na utunzaji wa mazingira katika wilaya yenu, pamoja na mapungufu ya hapa na pale lakini ukweli mji wenu ni msafi, hata maeneo ya machinjio ni tofauti na kwingine,”

“Lakini pia wenzetu mmekwenda mbali zaidi, maana mmenieleza tayari mmejiwekea utaratibu na kukubaliana kufanya usafi kila jumamosi ya kila wiki badala ya mwezi mara moja kama tulivyokubaliana kitaifa, na tayari mmesema mnazo sheria ndogo zinazohusiana na suala la usafi na utunzaji wa mazingira, hongereni sana,” alieleza Mpina.


Naibu waziri Mpina akipata maelezo kutoka kwa bwana afya wa Manispaa, (hayupo pichani) katika eneo la dambo linalotumika kutupia taka zinazokusanywa kutoka katika maguba.

Kwa upande mwingine Mpina alisisitiza suala la upandaji wa miti ili kukabiliana na hali ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameanza kujitokeza katika maeneo mengi na kusababisha majanga ikiwemo ukame na mafuriko na baadhi ya maeneo kugeuka kuwa jangwa.

Mpina alisema hata ndani ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020 inaelekeza suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira lengo ni kutaka kuirudisha nchi katika hali nzuri na kupunguza hewa chafu (carbon dioxide) inayotishia kuenea katika maeneo mengi.

“Nawaombeni sasa tuhamishie nguvu zetu katika suala zima la upandaji miti, tupande miti kama wendawazimu, mikoa ya Shinyanga, Dodoma, Singida na Simiyu ina uhaba mkubwa wa miti kutokana na wananchi wake kuikata ovyo, tusifanye mchezo, asilimia 61 ya maeneo ya nchi yetu yapo katika hatari ya kugeuka jangwa,” alieleza Mpina.


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro aliyekuwa amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga alisema hali ya usafi katika wilaya yake imechangiwa zaidi na mwitikio wa wananchi waliokubali kufanya usafi katika maeneo yao kila Jumamosi na kwamba hivi sasa watahimiza pia suala la upandaji miti.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top