Naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina akiwasili katika kiwanda cha kutengeneza ngozi cha kampuni ya Xing Hua kilichopo eneo la Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga. |
NAIBU Waziri
ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Luhaga Mpina ameagiza kufungwa kwa kiwanda
cha kusindika ngozi cha Xing Hua kilichopo manispaa ya Shinyanga baada ya
kubainika kinachafua mazingira.
Mbali ya
kufungwa kwa kiwanda hicho pia wamiliki wake wametakiwa kulipa faini ya
shilingi milioni 25 ndani ya kipindi cha siku 14 huku wakipewa siku saba
kufukia taka ngumu zilizokuwa zikitupwa ovyo na kusababisha harufu mbaya
kuzagaa maeneo ya jirani na kiwanda.
Kufungwa kwa
kiwanda hicho kunatokana na ziara iliyofanywa juzi na Naibu waziri Mpina
akiongozana watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) wakiwemo viongozi wa serikali mkoani Shinyanga na kukuta makosa kadhaa
ya uchafuzi wa mazingira kiwandani hapo.
Mratibu
kutoka NEMC kanda ya Ziwa, Anna Masasi akisoma taarifa ya makosa yaliyobainika
katika ukaguzi uliofanyika alisema ni pamoja na umwagwaji ovyo ya maji
yanayotoka kiwandani kutokana na mabwawa yanayotumika kuhifadhia maji hayo
kutowekewa vizuizi vya kitaalamu kuzuia yasiingie ardhini.
Hata hivyo
Masasi alisema wamiliki wa kiwanda hicho walifanya ujanja kwa kuidanganya
serikali baada ya kubainika kibali walichopewa kilikuwa ni kujenga kiwanda cha
kuchinja na kusindika nyama lakini badala yake wamejenga kiwanda cha
kutengeneza ngozi kinyume na kibali chao kinavyoeleza.
Naibu waziri Mpina akikagua maeneo mbalimbali ya kiwanda kujionea hali ya mazingira ilivyo, nyuma yake ni mmoja wa wamikili wa kiwanda hicho, Mr. Wang Kum. |
“Tumebaini
makosa kadhaa katika ukaguzi wetu, mojawapo ni eneo la kuhifadhia maji machafu
yanayotoka kiwandani kutokuwa katika hali inayoridhisha kutokana na mabwawa
yaliyochimbwa kuhifadhia maji hayo kutokuwekewa kinga za kuzuia maji kuingia
ardhini,”
“Lakini pia
tumeona wenyewe eneo wanalotupa taka ngumu, ikiwemo mabaki ya ngozi na vipande
vya nyamanyama ni baya na taka zinazagaa ovyo na hivyo kusababisha usumbufu kwa
majirani wanaoishi karibu na kiwanda huku eneo lote likigumbikwa na harufu
mbaya,” alieleza Masasi.
Kutokana na
hali hiyo, Naibu waziri Mpina alitoa agizo la kufungwa kiwanda hicho kuanzia
juzi ambapo alitoa siku saba wamiliki wa kiwanda wawe wamefanya utaratibu wa
kuchimba shimo na kufukia taka zote ngumu chini ya usimamizi wa wataalamu wa
mifugo na kilimo kutoka manispaa ya Shinyanga.
Akipata maelezo ya jinsi miundombinu ya kusafirisha mabaki ya maji machafu kutoka kiwandani na yanavyohifadhiwa. |
“Hawa
wenzetu tuwaombe wasituelewe vibaya tunapochukua maamuzi haya, tuliwakaribisha
kwa nia nzuri ili tusaidiane nao katika kukuza uchumi wetu, lakini baadhi yao
wanaonekana kwenda kinyume na suala la utunzaji wa mazingira katika viwanda
vyao, hatutaruhusu hali hii iendelee kutokea, sheria lazima ziheshimiwe,”
“Tunakifunga
kiwanda hiki kuanzia leo (juzi) na ninatoa siku saba wawe wamefanya utaratibu
wa kuchimba shimo ili kufukia taka zote tulizokuta zinazagaa ovyo na kutoa
harufu mbaya, kazi hii ifanyike chini ya usimamizi wa wataalamu wetu, na hizi
shilingi milioni 25 zilipwe ndani ya siku 14,” alieleza Mpina.
Mkuu wa
wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro aliyemwakilisha mkuu wa mkoa Ally Rufunga
alimshukuru waziri Mpina kwa hatua alizochukua na kueleza kuwa uongozi wa mkoa
mara kwa mara ulikuwa ukitoa maelekezo kwa wamiliki wa kiwanda hicho kuhusu
suala zima la utunzaji mazingira lakini mara zote walikaidi.
“Tunakushukuru
Naibu waziri kwa maagizo uliyoyatoa leo hii, hawa wenzetu kwa kipindi kirefu
wamekuwa wakikaidi maagizo yote wanayopewa na uongozi wa mkoa, wanadai
wanaowasikiliza ni watu wa EPZ, lakini hata uzalishaji wa kiwanda ni wa
kusuasua, muda mwingi hakifanyi kazi,” alieleza Matiro.
Post a Comment