Mwenyekiti wa CCM kata ya Ndala akimnadi mgombea udiwani wa CCM kata ya Ndala, Abel Kaholwe katika mkutano wa kampeni kwa wakazi wa kata ya Ndama Manispaa ya Shinyanga. |
Hata mimi Push - Up nazimudu eti, tazama hapa!!! ndivyo anavyoelekea kueleza mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM katika kata ya Ndala Shinyanga. |
WAKAZI wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga
wameombwa Oktoba 25, mwaka huu wahakikishe wanatumia vizuri kura zao kwa
kumchagua diwani mwenye uwezo atakayeshughulikia kero zao badala ya kumchagua mtu
anayetaka sifa na maslahi binafsi.
Ushauri huo umetolewa na mmoja wa wajumbe wa timu
ya kampeni za kuwanadi wagombea wa CCM katika jimbo la Shinyanga mjini, Zuhura
Waziri katika mkutano wa kampeni za kuwanadi wagombea wa chama hicho
uliofanyika kwenye viwanja vya kanisa la Angilakana kata ya Ndala mjini humo.
Waziri alisema suala la maendeleo katika eneo lolote
lile linahitaji mtu muadilifu na mchapa kazi kama alivyo mgombea wa CCM, Abel
Kaholwe ambaye mbali ya kuwa kijana lakini pia anao uzoefu wa kutosha wa
kushughulikia matatizo ya wananchi.
“Ndugu zangu wakazi wa kata ya Ndala, tunaelekea
kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, ni vizuri tukazitumia vizuri kura
zetu kwa kumchagua mgombea wetu wa CCM, ni kijana na mchapa kazi, msirudie makosa
ya mwaka 2010 kwa kuchagua diwani kutoka upinzani,”
“Ninyi wenyewe ni mashahidi kutokana na kudorora kwa
maendeleo katika kata yenu, yapo mambo mengi yameshindikana kutekelezwa
kutokana na udhaifu wa diwani mliyekuwa mmemchagua, kwa hali hiyo tunawaomba
msirudie tena kosa la kulamba sumu, litawacheleweshea maendeleo,” alieleza
Waziri.
Kwa upande wake mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM
katika kata hiyo ya Ndala, Abel Kaholwe aliwaomba wakazi wa kata hiyo wampe kura
za kishindi ili aweze kuwa diwani wao na apate fursa ya kushughulikia kero
nyingi zilizopo katika kata hiyo.
“Tunaingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wakazi wa
kata ya Ndala tukiwa na agenda tatu muhimu, ipo kero ya kupandishwa ovyo kwa
kodi za majengo, ukosefu wa huduma za afya na ubovu wa miundombinu ya barabara
na kutokupimwa kwa viwanja vya makazi,
“Yote haya katika kipindi cha nyuma yalishindwa
kutekelezwa kutokana na udhaifu wa diwani tuliyekuwa naye, huyu kipindi kirefu
alishughulikia matatizo yake badala ya wananchi, nakuombeni tusirudie kosa,
nipeni kura zenu niweze kuwatumikia,” alieleza Kaholwe.
Kwa upande wake mmoja wa wagombea wa udiwani viti
maalumu, Mariamu Nyangaka aliwataka wakazi wa kata hiyo kuhakikisha wanatunza
shahada zao za kupigia kura na wasikubali kurubuniwa na watu wanaopita pita
mitaani wakitaka kuzinunua na kwamba kura zao zina thamani zaidi ya fedha
watakazopewa.
Post a Comment