Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TAMWA kutoka wilayani Sengerema mkoani Mwanza akiwasilisha maoni ya kundi lake mbele ya waandishi wengine.
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo ya waandishi wa habari, Fredrick Katulanda akisisitiza jambo mbele ya waandishi.
 
Mshiriki wa Mafunzo kutoka Radio Fadeco Karagwe akichangia mada katika mafunzo ya waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
WAANDISHI wa habari nchini wamekumbuswa wajibu wao wa kuwaelimisha wananchi juu ya mambo muhimu ya kisheria wanayopaswa kuyazingatia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa uvunjifu wa amani.


Ushauri huo umetolewa mjini Mwanza na Leonida Kanyuma kutoka Chama cha wanahabari wanawake nchini (TAMWA) katika mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya kanda ya Ziwa yakihusu mchango wa vyombo vya habari na uchaguzi mkuu.

Kanyama alisema waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zinazohusiana na mambo ya uchaguzi ikiwemo kuwaelimisha juu ya sheria mbalimbali za uchaguzi zilizopo kama zilivyoandaliwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).

Alisema yapo mambo mengi yanayohusiana na mchakato wa uchaguzi mkuu nchini unaoendelea hivi sasa ambayo wananchi hawayaelewi kiundani na hivyo kuhitajika mchango wa vyombo vya habari ili waweze kuyaelewa.

Hata hivyo alisema pamoja na jukumu la waandishi kuielimisha jamii lakini bado wanapaswa kuhakikisha kile wanachokifikisha kwao ni habari sahihi isiyokuwa na upotoshaji wa aina yoyote au yenye mlengo wa kulalia upande mmoja wa chama cha siasa.

“Tumekutana hapa leo kwa lengo moja tu la kukumbushana juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, uchaguzi mkuu ni jambo muhimu katika mstakabali wa taifa lolote lile duniani, hivyo kuna kila sababu za kuhakikisha unafanyika katika hali ya amani na utulivu,”

“Waandishi wa habari tunalo jukumu kubwa la kuwasaidia wananchi waweze kuelewa masuala mbalimbali wanayopaswa kuyaelewa katika kipindi hiki cha uchaguzi, ikiwemo siku ya upigaji kura, na ni vizuri tukaandika habari sahihi kutoka mamlaka husika ili tusiipotoshe jamii,”

Akitoa mfano alisema hivi sasa kuna kauli tata inayohusiana na suala la siku ya kupiga kura ambapo wananchi wanatakiwa kurejea nyumbani lakini hata hivyo wapo baadhi ya wanasiasa wanawataka wapiga kura wakimaliza kupiga kura wakae umbali wa mita 200 ili walinde kura.

“Kuna kauli zinachanganya, NEC na baadhi ya viongozi wa serikali wanawataka wananchi wakipiga kura waondoke vituoni na kwenda nyumbani, wanasiasa wanasema mkipiga kura kaeni umbali wa mita 200 mlinde kura zenu, sasa mwandishi ni jukumu lako kutafuta sheria hasa inazungumziaje suala hili,” alieleza Kanyama.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Mara na Mwanza ambayo yanaratibiwa na TAMWA kwa lengo la kuwasaidia waandishi kuelewa umuhimu wa kuandika habari sahihi zinazohusiana na masuala ya uchaguzi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top