Mlengwa wa Mpango wa TASAF III akielekezwa jinsi ya kuweka saini ya dole gumba kabla ya kukabidhiwa fedha zake. |
BAADHI ya
walengwa wanaonufaika na Mpango wa kuzinusuru kaya maskini nchini kupitia Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu wameipongeza serikali kwa uamuzi
wake wa kuanzisha mpango huo utakaowezesha kupunguza kiwango cha umaskini
miongoni mwa watanzania.
Wakizungumza
na waandishi wa habari wakati wa ugawaji wa fedha kwa walengwa
kwa awamu ya pili walengwa hao katika vijiji vya Itwangi na Kidanda kata ya
Itwangi wilayani Shinyanga walielezea jinsi walivyoanza kunufaika na mpango huo
ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Walisema
mpango wa TASAF III utawawezesha wengi wao kuondokana na umaskini wa kipato kwa
kutumia fedha kidogo wanazopatiwa kila baada ya miezi miwili ambazo sehemu yake
huitumia kwa kununulia mahitaji muhimu ikiwemo chakula na nyingine kufanya
shughuli za ujasiriamali mdogo.
Sehemu ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini kutoka kata ya Itwangi Shinyanga wakisubiri kupokea ruzuku zao. |
Kwa upande
wake Bi. Sofia Mwanzalima mkazi wa kitongoji cha Imenya kata ya Itwangi alisema
fedha aliyopokea katika awamu ya kwanza ilimuwezesha kununulia kuku wawili
ambao anatagemea watakapoanza kutaga mayai na kutotoa wataongezeka na
kumwezesha kuwa mfugaji wa kuku.
“Ninaishukuru
serikali kwa kutuanzishia mpango huu, kwa kweli kama tukiutumia vizuri utaweza
kutukomboa katika dimbwi hili la umaskini, pale mwanzo nilinunua kuku wawili,
na leo hii sehemu ya fedha hii niliyopokea nitanunulia chakula na nataka
niongeze kuku mwingine, wakiwa wengi nitauza na kununua mbuzi,” alieleza Bi.
Mwanzalima.
Walengwa
wengine Pecos Mazoya mkazi wa kitongoji cha Igomelo, Bakari Kizozo kutoka
kitongoji cha Wella na Stella Kibushi kutoka kijiji cha Itwangi walielezea
jinsi walivyoanza kunufaika na mpango huo na kwamba wanaamini ndani ya kipindi
cha miezi sita kiwango cha umaskini walichonacho hivi sasa kitapungua kwa kiasi
kikubwa.
Mlengwa wa ruzuku yenye masharti akipokea ruzuku yake, wanaokabidhi ni wajumbe wa kamati ya ugawaji wa fedha waliochaguliwa na wanakijiji wenyewe. |
Kwa upande
wake mmoja wa maofisa wa TASAF katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,
Happiness Shayo aliwaomba walengwa wote walioteuliwa katika awamu ya kwanza ya
mpango huo kuhakikisha wanatumia vizuri fedha wanazopatiwa badala ya
kuzielekeza kwenye matumizi ya anasa.
“Serikali
imeamua kuanzisha mpango huu kwa nia njema kabisa, lengo kuu ni kutaka
kuwakomboa wananchi wake wanaoishi katika mazingira hatarishi ya umaskini wa
kipato, kwa hali hiyo ni vizuri tukazitumia fedha hizi kwa malengo
yaliyokusudiwa, msizitumie kwa mambo ya anasa,”
“Tujitahidi
fedha hii itukomboe ili baada ya miaka mitatu iwe mmepiga hatua, kumbukeni
baada yenu kuna wengine watafuata, lakini pia kwa wale wenye ruzuku ya
masharti, hakikisheni mnatimiza masharti yenu, pelekeni watoto kliniki na kwa
wale wanaopaswa kwenda shule waende shule, vinginevyo mtafutiwa ruzuku,”
alieleza Shayo.
Shayo
alisema hivi sasa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga inaendelea na ugawaji wa
fedha kwa walengwa ikiwa ni awamu ya pili ambapo awamu ya tatu inatarajiwa
kufanyika mwishoni mwa Novemba 2015 na kwamba jumla ya kaya maskini 9,458
zinatarajiwa kunufaika na mpango huo wilayani humo.
Post a Comment