Mgombea mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (CCM), Bi. Samia Suluhu Hassan. |
MGOMBEA
Mwenza wa CCM, Bi. Samia Suluhu Hassan amewaomba wakazi wa majimbo manne ya
uchaguzi jijini Dar es Salaam waendelee kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM)
kwa vile ndiyo chama pekee chenye uwezo wa kuwaletea mabadiliko ya kweli.
Bi.
Hassan aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara ya
kampeni za kumnadi mgombea urais wa CCM, Dkt. John Magufuli uliyofanyika katika
majimbo ya Kibamba, Ubungo, Kinondoni na Kawe.
Akiwa
katika jimbo jipya la Kibamba, aliwataka wakazi wa jimbo hilo kuhakikisha
hawarejei kosa walilolifanya mwaka 2010 kwa kumchagua mbunge anayetokana na
upinzani, John Mnyika (CHADEMA) kwa vile tayari wamejionea uwezo wake mdogo wa
kuwatumikia.
Alieleza
kushangazwa kwake na madai ya wagombea wa upinzani ambao kila siku
wanawashinikiza watanzania kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi ili wao
waweze kuleta mabadiliko na kwamba uwezo huo hawana na hawajawahi kuongoza nchi
hata siku moja kwamba mabadiliko wanayoyataka wao ni yale ya kuleta machafuko.
“Ndugu
zangu wakazi wa jimbo jipya la Kibamba, CCM tunapita kwenu kukuombeni kura zenu
hapo Oktoba 25, mwaka huu, tunafanya hivi kwa vile tunawathamini, kikubwa
tunachowaomba tupeni kura za kishindo kwa kumchangua mgombea urais wetu, Dkt.
John Magufuli,”
“Lakini
niwatahadharishe na kauli za wenzetu hawa wanaojiita UKAWA, wanapita wakiwaomba
mfanye mabadiliko, waulizeni wanataka mabadiliko gani, maana tayari CCM
imeshafanya mabadiliko makubwa katika nchi yetu, mfano mzuri ni mabadiliko ya
kutoka mfumo wa chama kimoja na kuwa wa vyama vingi,”
“Niwahakikishie
mabadiliko ya kweli yataendelea kuletwa na serikali ya CCM ndiyo yenye uzoefu,
ninyi wenyewe ni mashahidi, linganisheni hali ya barabara zetu miaka 10 nyuma
na zilivyo hivi leo, nyingi zimejengwa kwa kiwango cha lami, na hata kwenye
bajeti zetu, tumeanza kubadilika, tumepunguza kutegemea wahisani,” alieleza Bi.
Hassan.
Kwa
upande wa jimbo la Ubungo, Bi. Hassan aliwahakikishia wakazi wa jimbo hilo
iwapo serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. Magufuli itafanikiwa kuingia
madarakani moja ya vipaumbele vyake vya kwanza ni kujenga hospitali kubwa ya
kisasa katika jimbo hilo.
Kuhusu
tatizo la ajira kwa vijana, alisema serikali ya awamu ya tano itafanya kila
linalowezekana ili kumaliza tatizo la ajira kwa vijana kwa kufufua viwanda
vilivyofungwa na kujenga vipya ili kuwezesha vijana kupata ajira na pia
kuwezesha akinamama na vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu ili kuinua
mitaji yao.
“CCM
hivi sasa imejipanga vizuri katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa ajira,
moja ya mipango yetu ni kujenga viwanda vingi na kuvifufua vilivyofungwa ili
vijana wetu wapate ajira, lakini pia tutafungua mfuko maalumu wenye kiasi cha
shilingi milioni 10 utakaokuwa dhamana ya mikopo kwa vijana na akinamama,”
alieleza Bi. Hassan.
Aidha
kuhusu
kero ya uhaba wa maji katika jiji la Dar es Salaam, alisema Chama cha
Mapinduzi kinalielewa vyema tatizo hilo na hivi sasa kinafanya kila
linalowezekana kuhakikisha kero hiyo inatatuliwa na jiji la Dar es
Salaam kwa kuongeza
upatikanaji wake kutoka asilimia 75 ya sasa na kufikia asilimia 95.
Kwa
upande wake Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela
Kairuki aliwaeleza wakazi wa kijiji cha Mloganzila waliokubali kuyahama maeneo
yao kupisha ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa ili kuipunguzia mzigo hospitali
ya Muhimbili kwamba serikali ya CCM imekubali pamoja na kulipwa fidia zao
lakini pia watalipwa kifuta jasho kingine.
Mgombea
mwenza huyo leo hii anaendelea na ziara ya mikutano ya kampeni katika wilaya ya
Ilala jijini Dar es Salaam ambako ataendelea kumnadi mgombea urais wa CCM, Dkt.
Magufuli, wabunge na madiwani wote wa CCM ambapo kwa jana aliweza kuhutubia
mikutano minne ya kampeni.
Naye
mgombea ubunge katika jimbo la Ubungo, Didas Masaburi alisema iwapo
atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha anavisaidia vikundi
vya akina na mikopo (SACCOS) viweze kuimarka zaidi ambapo atatoa kiasi
cha shilingi milioni 10 kwa kila SACCOS iliyopo katika jimbo lake.
Post a Comment