Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Alhaj Saad Kusilawe akitangaza kwa waandishi wa habari matokeo ya kura za maoni kwa nafasi za ubunge.
 
WABUNGE wote wa zamani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomaliza muda wao mkoani Shinyanga ukimuondoa James Lembeli aliyehamia CHADEMA wameibuka na ushindi mkubwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM zilizofanyika nchini kote juzi.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Shinyanga na Katibu wa CCM mkoani humo, Alhaji Saad Kusilawe majimbo yote ya uchaguzi mkoani humo yalikamalisha mchakato wa kura za maoni na hapakuwa na tatizo lolote kubwa lililojitokeza katika maeneo mengi.
 
Stephen Masele, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini akielezea furaha yake kwa wana habari muda mfupi baada ya kutangazwa kuongoza katika kura za maoni jimboni mwake.
Kusilawe alisema katika jimbo la Shinyanga mjini, mbunge anayemaliza muda wake, Stephen Masele aliibuka mshindi baada ya kupata kura 7,900 sawa na asilimia 81.8 ya kura zote halali 9,649 zilizopigwa katika vituo vyote akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Siha, Dkt. Charles Mlingwa aliyepata kura 669.
 
Wagombea wengine katika jimbo hilo na kura walizopata katika mabano walikuwa, Dkt. Abdalah Seni (391), Erasto Kwilasa (232), Hassan Fatiu (164), Mussa Jonas (116), Khatibu Kazungu (69), Willy Mzava (65) na Tara Omar Nzeimana (43).
 
Jimbo la Ushetu aliyeshinda ni Elias Kwandikwa aliyepata kura 11,554 akifuatiwa na Isaya Simon kura 5,241 na Erhard Mlyansi ambaye ni wakili wa kujitegemea jijini Dar es Salaam aliyejikusanyia kura 2007.
 
Mfanyabiashara maarufu nchini, Jumanne Kishimba ameongoza  katika jimbo la Kahama baada ya kupata kura  9,754 akifuatiwa na Sweetbert Nkuba (1,389), Julius Masubo (303), Adam Ngalawa (1460, John Tunge (89), Deogratias Sazia (268), Eliackim Machunda, Michael Bundala (321), Godwin Kitonka (461), Kapela Busungu (142) Luhende Gerald (118) na Charles Marere (94).
 
Katika Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige pia ameongoza kwa kura 11,575 ambapo mpinzani wake wa karibu Emmanuel Kipole alipata kura 1,197, Nicholaus Magangila (668), John Sukili (294), Wankia Lukumba (142), Maganza Mashala (597) na John Rufunga (294).
 
Ahmed Salum aliongoza katika jimbo la Solwa  kwa kupata kura 17,485, aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Amos Mshandete alipata kura 2,028, Kafile Paulo (637), Renatus Chokala (357), Luhumbi Kaswende (361), Hosea Somi (255), Cyprian Miyedu (1,586) na Luhende Richard (1,273),.
 
Katika jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi amepata kura 13,441, ambapo wagombea wengine katika jimbo hilo, Bonda William (6,143), Kishiwa Kapale (500), Heke Jidindulu (359), Limbe Maurice (393) na Timothy Ndanya (193), matokeo ya kata nane katika jimbo hilo yalikuwa hayajapatikana mpaka jana mchana.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top