EDWARD NGOYAYI LOWASSA KUGOMBEA URAIS KWA TIKETI YA CHADEMA.
Sehemu ya wageni waalikwa kwenye mkutano mkuu wa CHADEMA Taifa.
MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA, FREEMAN MBOWE AKIHUTUBIA MKUTANO MKUU WA CHADEMA
Mkutano Mkuu wa CHADEMA umempitisha Edward Lowassa kuwa Mgombea Urais na mgombea mwenza Duni Haji, hatimaye kuwa wagombea wa UKAWA.

CHADEMA imewapokea rasmi na kuwakabidhi kadi viongozi kadhaa mashuhuri waliokuwa CCM na ambao wamejiunga na CHADEMA.

Wamekabidhi kadi viongozi wanne wanaowakilisha makundi kadhaa yaliyojiorodhesha kujiunga CHADEMA.  Kadi ya kwanza imetolewa kwa Mgana Msindai Mwenyekiti wa Wenyeviti wa mikoa wa CCM akiwakilisha wenyeviti kadhaa walioomba kujiunga CHADEMA.

Kadi ya pili amekabidhiwa Makongoro Mahanga Naibu Waziri wa Kazi na Ajira kwa niaba ya mawaziri na manaibu waziri kadhaa walioomba kujiunga na jeshi la ukombozi.

Kadi ya tatu imetolewa kwa Mbunge wa Arumeru Magharibi Ole Madeye akiwakilisha wabunge wengi walioomba kujiunga CHADEMA.  Kadi ya nne imetolewa kwa Katibu wa fedha na Uchumi CCM Isaya Simon Bukakiye,Kahama ambaye anawakilisha viongozi wa wilaya kwa mamia ambao mpaka sasa wameorodhesha majina yao ili wasimame wahesabiwe!

Zinafuatia salaam kutoka kwa wawakilishi mbalimbali,vyama rafiki na wageni wengine...

Kati ya hotuba zilizosisimua ukumbini ni za James Mbatia Mwenyekiti mwenza wa Ukawa pamoja na mwenzie Dr Emmanuel Makaidi.

Makamo wa Rais Zanzibar alitoa hotuba makini na thabiti kabisa hususan kuuimarisha muungano na kuwarejeshea wananchi katiba yao kupitia mapendekezo ya Tume ya Warioba.

Mgombea mwenza Juma Duni Haji alishangiliwa mno na wajumbe hasa alipoeleza jinsi alivyochukua maamuzi magumu kwa kujivua nyadhifa zote SMZ na ndani ya CUF ili ajiunge Chadema kuwa mgombea mwenza.

Mgombea Urais Kamanda mpambanaji na mtetezi wa Wanyonge Mzee wa maamuzi magumu Edward Ngoyai Lowassa ametoa hotuba fupi yenye mambo mazito.

Lowassa amesema mwananchi yeyote asiwe na hofu itakuwaje baada ya UKAWA kuingia madarakani.Amesema ataanza mara moja mchakamchaka wa maendeleo.

Lowassa amemwagia sifa kemkem Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na viongozi wote kwa jinsi walivyokijenga chama hicho na pia amewasifu viongozi wote wa UKAWA kwa kujitoa kufanikisha yote na kumuunga mkono

Lowassa ameahidi kufanya kampeni ya kistaarabu isiyo na matusi wala fujo na ameahidi kufika kila jimbo la uchaguzi kunadi wabunge na madiwani.

Lowassa amemalizia kusema kwake hata siku moja hakuna msamiati wa kushindwa na ameahidi ushindi mkubwa UKAWA Oktoba 25.

Lowassa alikatishwa mara kwa mara hotuba yake kwa wajumbe waliokuwa wanamshangilia kupita kiasi.

Nje ya viwanja vya mlimani city kulikuwa na screen kubwa iliyokuwa inaonyesha kila kilichokuwa kinaendelea ndani na kulikuwa na umati mkubwa wa watu uliokuwa unapiga makelele ya shangwe kila walipoona Lowassa alipokuwa anatamka neno.

Mwenyekiti wa Chama Freeman Mbowe amekaribishwa kufunga mkutano mkuu na amesema kikao cha Kamati Kuu kitaendelea kwa siku tatu kupitisha majina ya wagombea ubunge.

Amewaasa wagombea wote kukubaliana na maamuzi ya chama hasa pale watakapotakiwa kupisha baadhi ya majimbo kwa wenzao wa UKAWA.

Mwisho kabisa Askofu Josephat Gwajima amemalizia kwa maombi maalum.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top