Hawa wamepanga kwenda kuonana na Mheshimiwa Edward Lowassa. |
Wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa
Kimaasai (Malaigwanan) kutoka Wilaya ya Monduli wamemuomba waziri mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa kubaki na kuendelea kuwa kada wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwa sababu ndicho kilichomlea na anakijua.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini
Monduli kwa niaba ya Malaigwanan, Mzee Joseph Mesopiro kutoka Kata ya Sepeko
wilayani humo alisema viongozi wa mila wanakusudia kutuma ujumbe maalumu kwa
Lowassa kumshauri asihame CCM kama baadhi ya watu aliowaita wapambe
wanavyomshauri.
“Sote Monduli tumesononeka kwa jinsi vikao vya
chama vilivyomtendea mbunge wetu. Bado tunampenda kama ambavyo tunakipenda
chama chetu. Tunaamini ataendelea kubaki CCM na kupigania ushindi wa chama
katika uchaguzi ujao,” alisema Mzee Mesopiro.
Alizungumza hayo wakati wa hafla ya kuchukua
fomu na kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Monduli, mwanasiasa wa
siku nyingi Loata Sanare.
Kwa upande wake Laigwanan Julius Laizer kutoka
Kata ya Moita, alisema licha ya mizengwe iliyotawala vikao vya uteuzi vya CCM
vilivyomalizika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha ufa
miongoni mwa viongozi na wanachama, bado anaamini chama hicho kitaendelea
kubaki imara hata kama baadhi ya watu watakihama.
“Kama viongozi tuliolelewa na kukuzwa na CCM,
tunaamini chama hiki kitaendelea kuwa imara na hatuko tayari kukubali ushawishi
wowote wa kututaka tuhamie upinzani,” alisema Laizer.
Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Lepurko wilayani
Monduli, Njoput Alami alibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa
kisingizio Lowassa kukatwa akiziita ni kelele za wapambe wanaohofia kukosa
fursa walizozitarajia iwapo Lowassa angeteuliwa kuwa mgombea wa CCM.
Akizungumzia taarifa za wanaCCM wilayani
Monduli kughadhabika na kutishia kukihama chama hicho kutokana na Lowassa
kukatwa, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro alikiri baadhi ya
wanachama kuchana kadi na kuchoma bendera za chama hicho, lakini akasema ni
idadi ndogo ikilinganishwa na wanachama waliopo wilayani humo.
“Kuna taarifa za kadi na bendera za CCM
kuchomwa moto katika baadhi ya maeneo kama Migungani, Mto wa Mbu, Makuyuni na
Nalaarani. Tunaendelea kukusanya taarifa sahihi na kufanya tathmini ya matukio
hayo,” alisema Kimaro.
Chanzo: Mwananchi
News
Post a Comment