Hassan Athuman Fatiu akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)
MWANASHERIA kutoka Kampuni ya Fatiu Advocate & Co. ya Jijini Dar es Salaam, Hassan Athumani Fatiu amejitosa rasmi kuomba kugombea ubunge katika jimbo la Shinyanga mjini.

Fatiu ametangaza nia hiyo mjini Shinyanga na tayari amechukua rasmi fomu kwa ajili ya kugombea ubunge katika hilo kwsa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo anasema uamuzi wake huo umesukuwa na nia ya dhati ya kutaka kuwatumika wakazi wa Shinyanga mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga, Fatiu alisema kwa miaka mingi Jimbo la Shinyanga halijawahi kupata mbunge mwenye nia na uzalendo wa dhati wa kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo hali ambayo imechangia wakazi wake waendelee kuishi katika maisha duni.

Hassan Athuman Fatiu (anayecheka) akiwa pamoja na waandishi wa habari wakati akitangaza rasmi kuchukua kwake fomu za kugombea ubunge katika jimbo la Shinyanga mjini.
Alisema pamoja na kwamba anatoka katika moja ya familia duni zilizopo katika kata ya Katingali manispaa ya Shinyanga akiwa ni mmoja wa watoto wa muuza kahawa maarufu mjini humo lakini anaamini elimu aliyonayo itamwezesha kuwatumika vyema wakazi wa Shinyanga.

Fatiu ambaye kwa sasa ni mmoja wa wakazi wa Kitangili waliofanikisha kata hiyo kuweza kupata umeme kutoka Shirika la Ugavi wa umeme nchini TANESCO anasema maendeleo yoyote ya kweli yanapaswa kuletwa na watu wenye moyo wa uzalendo wa kweli.

Alisema ili maendeleo ya kweli yaweze kupatikana katika eneo lolote lile ni muhimu pawepo viongozi wenye moyo wa kizalendo na wenye nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi badala ya kutanguliza mbele maslahi binafsi.

 “Uzoefu unatuonesha kwamba watu wengi wa ngazi ya chini hawana watu wa kuwasemea huko juu kwa dhati, na hata kama wanapokuwepo basi hawana ule uzalendo wa dhati na nia thabiti, hii ndiyo sababu iliyonisukuma kuomba kugombea ubunge katika jimbo letu,”

“Jimbo la Shinyanga halijawahi kupata mzalendo wa kweli, halijapata mzalendo wa dhati mwenye nia ya kuwatumikia wananchi, mimi nimeweza kuisaidia kata yangu ya kitangili nikiwa siyo diwani wala kiongozi wa ngazi yoyote bali kiongozi wa kikundi kidogo tu cha kijamii, sasa nataka niongeze wigo,” alieleza.

"Nina dhamira ya dhati ya kugombea ubunge kwenye jimbo hili la Shinyanga mjini,"
Fatiu alisema iwapo chama chake cha CCM kitampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu anaamini ataibuka na ushindi mkubwa dhidi ya wagombea kutoka vyama vya upinzani.

Alisema anagombea ubunge akitokea katika familia duni kabisa na hana ufahali wowote wa kifedha bali na ufahari wa kizalendo na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Shinyanga ndiyo uliomsukuma kugombea nafasi hiyo ya ubunge.

“Ninao uwezo kutokana na ujana wangu na elimu yangu niliyonayo, hivyo naamini nitawatumikia vizuri wananchi watakaonichagua, na kwa sasa siwezi kutaja vipaumbele vyangu kwa vile itategemea ilani ya uchaguzi ya chama changu itakuwa imeelekeza vipaumbele vipi,”

“Hata hivyo moja ya vipaumbele vyangu binafsi kama mbunge nitakavyopigania ni suala la kupiga vita mauaji ya kikatili ya vikongwe na walemavu wa ngozi na nitatumia ofisi yangu ya uanasheria kumaliza migogoro ya ardhi katika jimbo langu ambayo pia ni moja ya chanzo cha mauaji ya kikatili,” alieleza Fatiu.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top