Hizi ndizo fomu rasmi za kuomba kugombea ubunge wa Jimbo la Solwa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). |
Mgombea ubunge Jimbo la Solwa wilayani Shinyanga, Amos Mshandete akipokea rasmi fomu zake kutoka kwa katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga vijijini, Margareth Cosmas. |
WANACHAMA
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge
katika uchaguzi mkuu ujao wameshauriwa kutowekeana vinyongo wala uadui kwa vile
kila mmoja ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi ili mradi ametimiza sifa zinazotakiwa.
Ushauri huo umetolewa juzi na aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Shinyanga na diwani wa kata ya Ilola kwa tiketi ya CCM, Amos Malugu Mshandete
alipokuwa akichukua rasmi fomu kwa ajili ya kugombea ubunge katika jimbo la
Solwa wilayani humo.
Mshandete
alisema mara kwa mara kinapofika kipindi cha uchaguzi mkuu baadhi ya wanachama
wa CCM huwekeana uadui usio na sababu baada ya baadhi yao kujitokeza kuomba
kugombea nafasi za udiwani ama ubunge katika maeneo yao hali inayochangia
makundi na kuanza kuchafuana.
Pokea rasmi fomu hizi, ukazijaze kwa usahihi na kuzirejesha ifikapo Julai 19, mwaka huu saa 10 kamili jioni. |
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga vijijini, Margareth Cosmas akitoa maelezo muhimu kwa mgombea Mshandete yatakayomuwezesha kujaza fomu zake kwa usahihi. |
Akifafanua
Mshandete alisema kwa kawaida ndani ya CCM wanachama huwa
hawapingani bali ni kujipanga kuangalia ni mwana CCM yupi anayeweza
kuipeperusha vyema bendera ya CCM katika nafasi ya udiwani, ubunge na urais na
hiyo ni haki ya kila mwanachama.
“Ni
vizuri wana CCM katika kipindi hiki cha mchakato wa kura za maoni tukadumisha
umoja na mshikamano wetu kwa kila mmoja kujiona ana haki sawa na mwenzake
katika kugombea nafasi yoyote ya uongozi anayoihitaji na kazi ya kuamua nani
awe mgombea rasmi waachiwe wanachama wenyewe,”
“Binafsi
baada
ya kukaa na kutafakari kazi zangu nilizozitekeleza kwa upande huu wa
udiwani kwenye kata yangu na halmashauri nzima ya Shinyanga nikiwa
mwenyekiti wa halmashauri, nimeona wazi sasa ni wakati muafaka wa
kujikita
katika nafasi ya ubunge ili niweze kuwatumika zaidi wananchi wangu,”
alieleza
Mshandete.
Alisema
hatua yake ya kuamua kugombea ubunge katika jimbo la Solwa imetokana na kuombwa
na wapiga kura wa jimbo hilo kwa kipindi kirefu na wao ndiyo wanaoelewa sababu
za kumuomba agombee hivyo ameona akubali ombi hilo na iwapo atachaguliwa
ni wazi hatawaangusha.
Aliendelea
kueleza katika kipindi chake cha miaka 10 akiwa diwani wa kata ya Ilola na
miaka mitano ya uenyekiti wa halmashauri ya wilaya kwa kiasi kikubwa
amejitahidi kutekeleza kikamilifu ahadi zote alizozitoa kwa wapiga kura wake
kama ilivyoainishwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mpambe wa mgombea Mshandete akikabidhi ada ya kuchukulia fomu kiasi cha shilingi 100,000. |
“Katika
miaka 10 ya udiwani wangu naamini nimefanya mambo mengi katika
sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara ambapo kwa upande wa maji
hivi karibuni kata yangu itaanza kupata huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria, na
shule zote tatu za msingi tumekamilisha ujenzi wa nyumba za walimu siyo chini ya nne,”
“Kwa
upande wa afya nimekamilisha ujenzi wa zahanati mbili na hivi sasa tupo katika
kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya, naamini nikipata fursa ya kuwa mbunge
nitafanya mengi, muhimu wana CCM tuhakikishe uchaguzi hautugawi, kazi ya nani
atachaguliwa tuwaachie waajiri wetu ambao ni wananchi,” alieleza.
Wanachama
wengine wa CCM waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge
katika jimbo hilo la Solwa mbali ya Mshandete ni pamoja na mbunge
anayemaliza muda wake, Ahmed Salumu, Kafile Paulo, Renatus Chokala na
Mhandisi Luhumbi Kaswende.
Post a Comment