Mbunge
wa Mpanda Mjini, Said Arfi ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza
mjini Mpanda katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya
Msingi Kashaulili, jana Arfi aliwaeleza wananchi wa Mpanda kuwa uanachama wake
ndani ya Chadema utakoma mara tu baada ya kuvunjwa Bunge Julai 9.
Pia,
alitumia mkutano huu kuwaaga wananchi wa jimbo hilo akisema hatagombea tena
nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 10.
Arfi
alifafanua kuwa hayuko tayari kugombea jimbo hilo kupitia chama chochote cha
siasa na kauli hiyo imelenga kuondoa uvumi uliokuwa umeenea kwamba alikuwa na
nia ya kugombea kupia ama ACT – Wazalendo au CCM.
Alisema
amekuwa akishangazwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanachana
na wapenzi wa Chadema kuwa hajafanya lolote kwenye chama hicho.
Alisema
kama kuna mtu anayekifahamu vizuri chama hicho ni yeye, hivyo haoni sababu za
watu kumbeza.
Alisema
alikuwa ameamua kukaa kimya na kuwa akiamua ‘atamwaga mboga’ ili watu wafahamu
upungufu ulioko ndani ya chama hicho.
Alisema
hagombei katika jimbo hilo na kama kweli chama hicho kina nguvu, basi
kilitetee, akisisitiza kuwa ana uhakika jimbo hilo litakwenda CCM kwa kuwa
wananchi wa Mpanda Mjini walikuwa na mapenzi na mtu siyo chama.
Arfi
aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema kabla kujiuzulu wadhifa huo,
aliwahi kuhusishwa kusuka mpango wa kumwezesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kupita bila kupingwa katika kinyang’anyiro uchaguzi wa mwaka 2010 katika Jimbo
la Katavi kwa kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoka majina yao.
Hata
hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo, hali ambayo pia ilisababisha
kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake na kusababisha kujiuzulu nafasi
yake ya umakamu mwenyekiti.
Baadhi
ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walionyesha kushtushwa na kauli ya
mbunge huyo kujiondoa Chadema lakini wakasema ametimiza haki yake ya kikatiba
kuchagua sehemu iliyo sahihi kwake.
Mmoja
wa wananchi hao, Abdallah Hussein alisema: “Arfi amekuwa mvumilivu sana ndani
ya Chadema lakini anayo ya moyoni sasa kwa muda mrefu amekaa kimya aliogopa ya
Zitto Kabwe yasimtokee, sasa ameweka bayana msimamo wake acha tuheshimu mawazo
yake.”
Chanzo: Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment