Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Rais
Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kuwahimiza waumini wao kuwachagua
wanasiasa wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu au hata kuukaribia.
Amewataka
kuepuka makundi ya kisiasa na wasiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu
katika kutafuta madaraka kwa thamani yoyote na wawakemee wale wanaotaka kupata
madaraka kwa gharama yoyote.
Alisema
hayo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 125 tangu kuingia kwa
injili katika ukanda wa Pwani ya Tanga na Milima ya Usambara uliofanyika katika
Viwanja vya Mbuyukenda jijini hapa.
“Wanasiasa
wanaotaka madaraka kwa njia yoyote ile, muwanyanyapae, wakatalieni kwa macho
makavu, hawa si watu wema watatufikisha pabaya,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
hayo baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya
Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga kumweleza kwamba akiwa mkuu wa nchi anao
wajibu wa kuhakikisha Taifa linavuka kwa amani na usalama katika kipindi hiki
kigumu cha uchaguzi.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema katika kipindi hiki, viongozi
wa madhehebu ya dini wasijiingize katika makundi ya wanasiasa kwa sababu mambo
yakiharibika itakuwa hakuna pa kukimbilia.
Aliwataka
viongozi wa dini watumie nyumba za ibada kuliombea Taifa livuke salama katika
kipindi hiki kigumu badala ya kuwapangia vyama au viongozi wa kuwachagua.
“Tunawategemea
kuwahimiza na kuwakumbusha kutumia haki na wajibu wao vizuri, muwahimize na
kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu; Kwanza,
kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi
wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma
mbele gurudumu la maendeleo na kujali masilahi mapana ya jamii husika na nchi
yetu.”
“Viongozi
wa dini muwe kama mimi, nina wagombea wa urais 42, kama nitaonyesha kuwa upande
wa mgombea yeyote kati yao, basi nitakuwa nimeharibu mchakato mzima wa
uchaguzi.
“Tusiwape
mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee
kukemea matumizi mabaya ya fedha, rushwa, hila, ghiliba na hujuma katika
uchaguzi. Tunapaswa kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani
ya vyama vya siasa na baadaye wakati wa uchaguzi,” alisema.
Alisema
hiki ni kipindi nyeti na kwamba, viongozi wa dini pamoja na Watanzania kwa
ujumla wanapaswa kufahamu kuwa Tanzania haina kinga ya milele ya amani na
utulivu, kama itavurugwa haitakuwa lulu ya Afrika tena kama ilivyo sifa yake.
“Tuwakemee
wanasiasa wapenda madaraka kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha
kununua ushindi au ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua
wapinzani wao na kujijenga kisiasa. Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza
kwani mchezo wao ni mauti yetu. Wakatalieni kwa macho makavu na kwa kweli
muwanyanyapae,” alisema.
Rais
Kikwete ambaye wiki hii atakuwa na kibarua cha kuongoza vikao vya kuwachuja
wagombea kupitia CCM, alisema hawapaswi kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka
maadili na kuchochea mifarakano katika Taifa.
“Hawa
si watu wema, watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi yetu. Kamwe tusiruhusu
wachezee dini zetu ambazo ni mhimili muhimu sana wa amani yetu,” alisema.
Alisema
tofauti na ukabila ambao pamoja na ubaya wake, unaweza kuhusisha eneo dogo,
dini zinahusisha nchi nzima.
“Hakuna
mtu, dini wala eneo litakalonusurika. Tutapoteza ile sifa yetu ya kihistoria ya
kuwa lulu na mfano wa amani katika Afrika. Tusikubali kumchukiza Mungu akatukasirikia
na kutuadhibu kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee. Kwa
kweli mambo yakiharibika, hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote, bali sisi
wenyewe. Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu, bali itakuwa ni makosa yetu
wenyewe.”
Aliwaomba
viongozi wa dini: “Limeni mraba wenu vizuri nasi tulime wetu. Msiwape nafasi
viongozi wa siasa na hata wa dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza masilahi
yao ya kisiasa na hasa kupandikiza chuki katika jamii. Msiwe sehemu ya makundi
ya wagombea au vyama vya siasa. Mnatakiwa msiwe na upande, muwe juu ya pande
zote. Hapo ndipo mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya Taifa iwapo
kutatokea matatizo.”
Chanzo: Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment