VIONGOZI WAKUU WA UKAWA KATIKA MOJA YA VIKAO VYAO
Hatma ya chama cha NCCR-Mageuzi kuwa ndani ya Ukawa itajulikana Jumamosi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu Taifa, ambacho pamoja na mambo mengine, kitajadili taarifa za kutoridhishwa na mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.


Kikao hicho cha Jumamosi kitakutanisha viongozi wa NCCR-Mageuzi wa mikoa ambao watatoa mwongozo na hatma ya chama hicho ndani ya Ukawa, ambayo ni kifupi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi.

Vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chadema viliunda Ukawa wakati wa Bunge la Katiba vikipinga mwenendo wa vikao vya chombo hicho cha kutunga Katiba, na baadaye viongozi kusaini makubaliano ya kushirikiana kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kusimamisha mgombea mmoja kwenye nafasi za urais, ubunge na madiwani.

Tayari kamati inayoshughulikia utekelezaji wa azimio hilo imeshakutana na kukubaliana kugawana majimbo kwa asilimia 95, kwa mujibu wa viongozi wa Ukawa, lakini kumekuwapo na hali ya sintofahamu kwenye asilimia iliyosalia, hali kadhalika changamoto ya kikatiba katika kupata mgombea mwenza na waziri mkuu.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa miongoni mwa sababu za NCCR kutaka kujiondoa Ukawa ni kupewa majimbo machache ya uchaguzi kinyume na matarajio yao.

“Hoja nyingine ni kutoandaliwa kwa kanuni za kuongoza umoja huo mpaka sasa na hadi sasa majimbo 13 hawajafikiwa mwafaka,” alisema mpashaji habari wetu.

“Wanachama walitarajia kupata kati ya asilimia 10 na 15 ya majimbo yote, lakini mpaka sasa tumepata asilimia 3.4 tu kati ya majimbo 239 na hakuna matumaini ya kupata zaidi ya hapo kwa hivyo kuna wasiwasi wa wanachama kuazimia kujitoa.”

Hata hivyo, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipoulizwa kuhusu masuala hayo, pamoja na kukiri kuwapo kwa kikao Jumamosi, alikanusha madai ya chama hicho kutaka kujitoa Ukawa.

Alisema kikao hicho kitajadili hali ya kisiasa nchini na Uchaguzi Mkuu, lakini akasema suala la mgombea urais bado linajadiliwa ndani ya Ukawa.

Akizungumzia suala hilo Mbatia alisema, “Siyo kweli, hakuna mtu yeyote NCCR mwenye fikra ya kujitoa ndani ya Ukawa. Halmashauri Kuu haijaitishwa kwa ajili ya kujadili kujitoa Ukawa. 

Sisi ni waasisi wa Ukawa na NCCR ni chama cha maridhiano pia ni chachu ya kuleta mabadiliko ya Katiba tangu mwaka 1991 na kitajadili hali ya kisiasa nchini na uchaguzi wa ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Kuhusu mgawanyo wa majimbo, Mbatia alisema: “Kwenye makubaliano yoyote duniani kuna kupata na kupoteza. Ukawa si ya NCCR, Chadema, CUF wala NLD, ni mali ya Watanzania.”

Alisema Watanzania wanataka kuona Ukawa ikipiga hatua na viongozi wa vyama hivyo wanaweza wasiwepo lakini umoja huo ukaendelea kuwapo kwa kuwa ni injini ya kuwaunganisha, na NCCR haina ubavu wa kujitoa.

Kuhusu mgawanyo wa nyadhifa nyingine ndani ya umoja huo, Mbatia alisema: “Tutatekeleza matakwa yote ya kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na sheria ya uchaguzi na tutashiriki uchaguzi ipasavyo. Hayo ni mambo madogo ambayo tutayakamilisha hivi karibuni na kuueleza umma wa Watanzania.”

“Unaona CCM wanavyosuguana au Chadema wanavyosuguana. Hebu fikiria chama kimoja kina katiba yake na bado kinasuguana sasa Ukawa ina vyama vinne, misuguano ni lazima itakuwapo, tena mikubwa zaidi. Kinachotakiwa hapa ni hekima, amani na umoja ili tujenge maeleweno ya pamoja kwa maslahi ya Watanzania wote.”

SOURCE: Mwananchi News Papers
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top