Mheshimiwa Mpina akisaini kitabu cha wageni katika ofisi za CCM wilayani Meatu muda mfupi kabla ya kuzungumza na mamia ya wana CCM waliojitokeza kumdhamini. |
Jamani nilikuwa sitanii, bali nimedhamiria kweli kukabidhiwa kijiti na Rais Jakaya Kikwete, fomu hizi hapa!!! |
Mheshimiwa Luhaga Mpina akiingia katika ukumbi wa mikutano wa CCM wilayani Meatu, Simiyu, mkono wake wa kulia akionesha mkoba wenye fomu za kuomba kugombea urais. |
KADA WA CCM
KUTOKA WILAYA YA MEATU MKOANI SIMIYU, LUHAGA MPINA AFUNGA ZOEZI LA KUSAKA
WADHAMINI KWA KISHINDO.
·
Apata Baraka za
wazazi wawili,
Baba na Mama Luhaga Mpina wakitambulishwa mbele ya wadhamini wa Mpina. |
·
Mwenyekiti wa
CCM wilaya ampongeza, uamuzi wake umeitangaza wilaya ya Meatu kitaifa na hadi
mataifa ya nje.
·
Adhaminiwa na
wana CCM 945.
Meatu Simiyu.
MMOJA wa makada wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) anayeomba kuteuliwa na chama chake kupeperusha
bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Luhaga Mpina amekamilisha rasmi zoezi la kutafuta wadhamini 450
katika mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Tanzania Zanzibar.
Mpina ambaye pia
ni mbunge wa Jimbo la Kisesa amehitimisha zoezi hilo Juni 27, mwaka huu mjini
Mwanhuzi wilayani Meatu mkoa wa Simiyu ambako alipata wadhamini 945
waliojitokeza kumuunga mkono katika adhima yake ya kuomba kuteuliwa kugombea
nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini,
Oktoba 25, mwaka huu.
Katika hafla fupi
ya kukamilisha idadi ya wadhamini wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa
na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika katika viwanja vya Ofisi
ya CCM mjini Mwanhuzi iliyohudhuriwa na mamia ya wana CCM wilayani Meatu,
Luhaga alieleza furaha yake isiyo na kifani kwa jinsi wana CCM wenzake
walivyojitokeza kumuunga mkono.
Alisema mbali ya
wana CCM wa Meatu ambako ndiko alikozaliwa lakini pia alipata mapokezi makubwa
na yenye kutia moyo katika safari yake aliyoikusudia katika mikoa mingine 16
aliyotembelea kutafuta wadhamini wa kumdhamini na kwamba kila alikokwenda wana
CCM walionesha dhahiri kumuunga mkono huku wengi wao wakisema awamu ya rais wa
tano ni lazima iongozwe na rais kijana, mfano wake Mpina.
Miongoni mwa
walioshiriki katika hafla hiyo ni wazazi wawili, Baba na Mama wa Mheshimiwa
Mpina, ambao kutokana na furaha waliyosema walisema hawakuwa na la kueleza na
kwamba wanaamini mtoto waliyemzaa si wakwao peke yao bali ni wa watu wa Meatu
nzima, na kwamba kupata kwake nafasi hiyo ya urais itakuwa si sifa yao wazazi
peke yao bali kwa wana Meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
Mama mzazi wa Mheshimiwa Mpina (mwenye kitambaa kichwani) akifuatilia kwa makini hotuba ya mwanae katika ukumbi wa CCM wilaya Meatu, Simiyu. |
Awali akimkaribisha
kuzungumza na wana CCM waliojiotokeza kumdhamini, mwenyekiti wa CCM wilayani
Meatu, Juma Mwiburi alimshukuru Mpina kwa uamuzi wake sahihi wa kuamua kuwania
kuteuliwa ili aweze kugombea nafasi hiyo kubwa ndani ya nchi na chama chake na
kwamba kutokana na ujasiri wake anaamini ataimudu vyema.
“Kwa uwezo wako
ninavyokuelewa na umahiri
wako, mwenyezi mungu atakubaliki, kwa sababu
tutakubaliki kuanzia sisi kuanzia leo tunakuombea kwa mwenyezi mungu mradi jina
lifike tu mbele ya mkutano mkuu, tayari umeisha kuwa rais,”
“Naelewa huna
ubaguzi, na moyo wako nauelewa, na uchapa kazi wako, naamini mzee Mpina
hakukosea, ni baraka zako, na mama amesema si yeye peke yake aliyekuzaa bali
wote tumekuzaa, sasa tunakuombea kwa mwenyezi mungu safari hii ni ndefu, lakini
kwa maombi tunayoomba wilaya nzima ya Meatu na mkoa mzima wa Simiyu,
tunakuombea na kukutakia kila la kheri,” alieleza Mwiburi.
Kwa upande wake
katibu wa CCM wilayani Meatu, Jonathan Mabiya alisema jumla ya wana CCM 945,
kati yao 900 waliotoka ngazi ya kata, na 45 kutoka ofisi ya wilaya walijitokeza
kumdhamini mheshimiwa Mpina, na kwamba fomu zote zilizowekwa saini na wadhamini
hao na kugongwa mhuri wa CCM na mkurugenzi wa uchaguzi wilayani humo ambaye ni
yeye zimekamilika kikamilifu.
“Mheshimiwa Mpina
tunakuombea kwa mwenyezi mungu akutangulie katika safari yako ya urejeshaji wa
fomu hizo makao makuu ya Chama mkoani Dodoma, nikuhakikishie wanachama wote
waliojitokeza kukudhamini ni wanachama safi na hai wa Chama cha Mapinduzi, wanazo
kadi na wamelipia ada zao, ni hai kabisa, tunaamini kazi hii tumeifanya kwa
umakini, ni wazi mkoa wa Simiyu tumeuwakilisha vizuri,” alieleza Mabiya.
NAKUSHUKURUNI SANA!! SANA!! KWA KUNIUNGA MKONO. |
Mheshimiwa Mpina akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wadhamini wake. |
Akizungumza na
wana CCM waliojitokeza kumdhamini na wanachama wengine kwa ujumla, Mpina
alisema uamuzi wake wa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya
Muungano aliuchukua baada ya kujipima na kuona anaweza kuiongoza nchi ya
Tanzania, na chama chake cha CCM akiwa mwenyekiti wa CCM wa Taifa.
Mpina alisema
mbali ya kuamini anaweza kuongoza nafasi hiyo kubwa katika taifa la Tanzania,
lakini pia ni haki yake ya kikatiba na ni katika kutekeleza kwa vitendo
demokrasia na hatua hiyo ni kutimiza ahadi yake ya awali kwa wakazi wa wilaya
ya Meatu aliyoitoa Mei 31, mwaka huu kwamba atagombea nafasi hiyo ya urais, na
kweli ametimiza ahadi hiyo.
“Ndugu zangu
nataka niwathibitishie kwamba ile ahadi yangu niliyoitoa Mei 31, mwaka huu
nimeenda kutekeleza na ndiyo mkoba huu mnaouona ninao hapa ambao nilikabidhiwa
pale CCM makao makuu, Dodoma, ukiwa na fomu ya kuomba uteuzi na zile za
wadhamini wanaohitajika kunidhamini,”
“Lakini niwaeleza
ukweli katika mikoa yote 17 niliyotembelea kutafuta wadhamini, kabla ya
kukaribishwa kuzungumza na wadhamini wangu, watu waliokuwa wakiulizana, mbona
mgombea urais hatumuoni hapa, hii ni kutoka na umbile la mwili wangu kuwa dogo,”
“Na hata pale nilipokuwa
nikisimama watu walionesha wasiwasi, hata baada ya kumaliza kuwahutubia wengi
walinikubali, na wengine kusema wazi huyu ndiye Rais tunayemtaka, ni kutokana
na jinsi nilivyokuwa nikijieleza, walithibitisha ninafaa kwa nafasi hii
ninayoiomba, na kila sehemu tulikuwa tukiombewa dua,” alieleza Mpina.
Mpina aliiitaja
mikoa 17 aliyoitembelea kusaka wadhamini 450 ukiwemo mkoa wa Simiyu, na kwamba
maeneo mengi walipata wadhamini wengi na hata hivyo walizingatia hitaji na
maelekezo ya CCM makao makuu ya wadhamini 450, na kwamba katika mikoa yote
walipata wadhamini safi wenye sifa zote zilizoainishwa.
Aliitaja mikoa
mingine mbali ya Simiyu kuwa ni pamoja na Dodoma, Shinyanga, Singida, Tabora,
Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Tanga, Morogoro, Pwani, Iringa, Manyara,
Mjini Unguja, Mjini Magharibi na Kusini Unguja.
Hata hivyo Mpina
alisema kwa mujibu wa maelekezo ya sheria na kanuni yaliyotolewa na CCM makao
makuu asingeweza kuzungumzia mengi kuhusiana na adhima yake ya kutaka kuteuliwa
kugombea nafasi hiyo ya urais kwa vile kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuanza
kampeni na atakuwa amekwenda kinyume na maelekezo hayo.
“Baada ya kuchukua
fomu pale Dodoma, tulipewa nafasi ya kutangaza nia na nafasi ya kuongea kidogo
nini tunachofikiria kukifanyia Chama chetu cha Mapinduzi lakini pia utaifanyia
nini nchi yako, hayo yote yaliisha fanyika, sasa hivi haturuhusiwi tena kuanza kuzungumza kana kwamba unafanya
kampeni, ukifanya hivyo unakuwa tayari umepoteza,” alieleza.
Hata hivyo alisema
wengi walikuwa wakimpigia simu na kumuuliza kwa nini ameamua kugombea nafasi
hiyo ya urais, ambapo aliwajibu kuwa yeye ni mwana CCM na anayo haki ya
kugombea nafasi hiyo ambayo muda si mrefu itabaki wazi baada ya Rais aliyepo
madarakani kukamilisha kipindi chake cha miaka 10.
“Ndugu zangu kwa
kifupi tu niwathibitishie tena kwamba nafasi hii ninaimudu, na niwaeleze wazi
kati ya watia nia wengine wapatao 39, sioni atakayenishinda iwapo haki
itatendeka, maana muda mrefu nilikuwa nikiomba kwa mungu taifa letu liweze
kupata kiongozi mzuri atakayeliongoza taifa hili, lakini kila nilipoomba,
mwenyezi mungu alinijibu, ni wewe mwenyewe Mpina ndiyo unayefaa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza na kushangiliwa.
Mpina alitarajia
kwenda mkoani Dodoma siku ya Jumanne, Juni 30, mwaka huu kwa lengo la kukabidhi
rasmi fomu zake za kuomba kugombea nafasi hiyo ya urais ambazo zimeambatanishwa
pamoja na fomu zote za wadhamini wake 450.
Post a Comment