WAZIRI TITUS KAMANI AKIWA KATIKA KIJIWE CHA KAHAWA MJINI SHINYANGA.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Peter Bunyongoli aliyekuwa ameongozana na waziri Kamani akihudumiwa kahawa na mmiliki wa kijiwe cha kahawa mjini Shinyanga.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo nchini na mbunge wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu, Titus Kamani (mwenye shuka mabegani) akishiriki kunywa kahawa katika moja ya vijiwe vya kahawa mjini Shinyanga, mwenye birika la kahawa ni mmiliki wa kijiwe hicho, Bakari Rashidi.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo nchini na Mbunge wa Jimbo la Busega (CCM) mkoani Simiyu, Titus Kamani amelazimika kushiriki katika kijiwe cha Kahawa mjini Shinyanga kilichopo jirani na Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini humo baada ya wananchi kumzuia alipokuwa akitokea Dodoma kushiriki kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).


Tukio hilo lilitokea Jumatatu ya Mei 25, 2015 saa mbili asubuhi baada ya wananchi kuliona gari la waziri likiwa limeegeshwa jirani na Soko Kuu mjini Shinyanga likipeperusha bendera ya serikali huku likiwa na namba zinazoonesha ni gari la Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, ambapo wananchi hao walimtuma mmoja wao amfuate amuombe aende katika kijiwe hicho ili aweze kusalimiana nao.

Waziri Kamani bila kinyongo aliteremka katika gari lake na kuelekea katika kijiwe hicho cha Kahawa kitendo ambacho kiliwafurahisha wananchi waliokuwa wamekaa kijiweni hapo, ambapo baada ya kufika alikabidhiwa kikombe cha kahawa na kuanza kuinywa  bila ajizi na mmoja wa wananchi aliyekuwa akimfahamu alimtambulisha rasmi kwa wananchi wenzake kwamba, huyo bwana ni waziri wa maendeleo ya mifugo.

Utambulisho huo uliongeza furaha ya wana kijiwe hicho cha kahawa hali iliyosababisha wapita njia wengine kuamua kusogolea eneo hilo na kujumuika pamoja na waziri katika kunywa kinywaji hicho cha kahawa wakionesha kufurahishwa na kitendo cha waziri kukubali wito wa wananchi.

Kwa upande wake mmiliki wa kijiwe hicho, Bakari Rashidi, ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, aliwaeleza wateja wake kwamba kitendo kilichooneshwa na waziri Kamani kinatokana na CCM kuwa na hazina kubwa ya viongozi wanaowajali wananchi, ambapo alisema pamoja na kwamba ni waziri, lakini hakuwanyanyapaa wananchi hao pale walipomuomba asalimiane nao.

"CCM bwana tuna hazina kubwa ya viongozi, ni viongozi wa watu, ninyi wenyewe mmejionea leo hii, nani alikuwa anamfahamu waziri huyu, lakini bila kujali hadhi yake ya uwaziri amekubali kukaa na sisi hapa na tumekunywa naye pamoja kahawa, CCM ni chama dume bwana, kina viongozi wanaowajali wananchi, mwingine asingekubali kukaa kwenye benchi hizi na kunywa kahawa pamoja na sisi huku tukibadilishana naye mawazo,"  alieleza Bakari.

Kwa upande wake waziri Kamani aliwashukuru wananchi hao kwa kitendo chao cha kumwita kwa lengo la kusalamiana na kufahamiana ambapo pia alimtambulisha mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Maswa, Mheshimiwa Peter Bunyongoli na kwamba yeye mwenyewe mbali ya nafasi ya uwaziri na ubunge alionao pia ni mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Simiyu.


Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top