Dkt. Hamisi Kigwangala akiwa na mwenyekiti wa CCM wilayani Nzega, mkoa wa Tabora, Amos Kanuda wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Parking mjini Nzega. |
Dkt. Kigwangala akielekea meza kuu baada ya kupokelewa na vijana wa Green Guard. |
Akipokea salaam kutoka kwa Green Guard. |
Akishiri kucheza ngoma ya utamaduni na kikundi cha Walumba cha mjini Nzega. |
Dkt. Kigwangala akihutubia maelfu ya wakazi wa Nzega katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Parking. |
MBUNGE
wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora, Dkt. Khamis Kigwangala amekitahadharisha Chama
cha Mapinduzi (CCM) kihakikishe hakiteui mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu atakayebainika kuusaka uongozi kwa kutumia fedha vinginevyo
kitaanguka vibaya kwenye uchaguzi huo.
Dkt.
Kigwangala ambaye ni mmoja wa wana CCM walioonesha nia ya kugombea urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM alitoa tahadhari hiyo juzi
alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Nzega na vitongoji vyake katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Parking mjini humo.
Alisema
wakati Taifa likijipanga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ni muhimu kwa CCM
ikajipanga vizuri katika kupanga safu ya wagombea wake kuanzia ngazi zote za
udiwani, ubunge na urais kwa kuhakikisha haisimamishi wale wote walioanza
kusaka uongozi huo kwa kutumia fedha.
Alisema
baadhi ya walioonesha nia ya kutaka kuteuliwa kugombea nafasi ya urais hivi
sasa wanapitapita maeneo mbalimbali wakigawa fedha kwa wajumbe watakaohusika na
vikao vya uteuzi ili waweze kuteuliwa hali ambayo alisema inapingana na
tararibu na kanuni za CCM.
“Ndugu
zangu binafsi naendelea kuwathibitishia kwamba nia yangu ya kutaka kugombea
urais wa nchi ipo pale pale, na niwaeleze wazi kwamba sijatoa uamuzi kuhusu
kugombea kwangu tena ubunge katika jimbo hili la Nzega, kwanza nimejikita
kwenye urais, iwapo nitashindwa huko ndipo nitatoa uamuzi kama nitagombea
ubunge au laa,”
“Hata
hivyo napenda nitumie nafasi hii kukitahadharisha Chama changu cha CCM kiwe makini
katika uteuzi wa mgombea wake katika nafasi hii nyeti ya urais wa Jamhuri ya
Muungano, isifanye kosa hata kidogo kwa kumteua mtu ye yote ambaye tayari
ameonesha dhahiri kuusaka urais kwa kutumia fedha,”
“Tunataka
CCM isimamishe mgombea aliye safi asiye na doa lolote au kashifa yoyote ya
ufisadi katika nchi hii, bali izingatie mtu mwenye agenda na anayeeleza iwapo
atachaguliwa kuwa rais atawatendea kitu gani watanzania, siyo sifa ya kuwa na
fedha nyingi, nyingine tunajua zimeibwa kutoka serikalini, hii hatukubali,” alieleza
Dkt. Kigwangala.
Alisema
yeye
binafsi anaamini CCM itahakikisha hakuna mgombea ye yote ambaye
amebainika tayari anakwenda kinyume cha kanuni na maadili ya chama na
ambao hivi sasa wanapitapita kwa
wajumbe wa vikao vya uteuzi wakimwaga fedha atakayeteuliwa bali majina
yao yote yatakatwa mapema.
Akifafanua Dkt.
Kigwangala alisema iwapo CCM itamsimamisha mgombea ye yote mwenye
dosari na aliyebainika kutumia fedha katika kuusaka uongozi ni wazi watanzania
watahoji maana wengi sasa ni wajanja na wana akili, ni vigezo vipi vilivyotumika kumteua maana CCM daima inaimba rushwa
ni adui wa haki, sasa lazima ioneshe kwa vitendo jinsi inavyoichukia rushwa.
“Hawa
wanaotumia fedha mpaka hivi sasa hawajaweza kuwaeleza wananchi iwapo
watachaguliwa watawafanyia nini, binafsi mimi nina agenda na hoja ya kwa nini nataka
kugombea urais, na nimeandikika kitabu kueleza nitakayoyafanya, naamini wengine walioonesha nia ni dhaifu sana, hawana agenda
yoyote ya maana mbali ya kuegemea kwenye uwezo wao wa kifedha,”
“Hata chama changu cha CCM hakiamini katika watu wanaotumia fedha, kanuni zetu
zikiheshimiwa katika vikao vya awali, majina ya wengi wao yatakatwa hata kabla ya kufikishwa kwenye vikao
vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri kuu ya Taifa (NEC), na wengi mtashangaa maana
majina yatakayojitokeza ni ya wagombea vijana,” alieleza Dkt. Kigwangala.
Aidha
mbunge huyo alisema itakuwa ni ajabu kwa vikao vya uteuzi ndani ya CCM kuteua
mgombea ambaye atasababisha wananchi kuwa na maswali mengi juu yake wakati wa kipindi cha kampeni mfano wa
wale ambao awali walitakiwa kuvuliwa magamba lakini baadae yaliishia mabegani
na wakasafishwa kwa kusamehewa.
“Wapo
waliotakiwa kuvuliwa magamba, wanafahamika, leo hii itokee CCM iwasimamishe
kama wagombea itakuwa ajabu kubwa, sijui mtu atasimamaje jukwaani kuwanadi,
lazima wananchi watahoji hawa wamekuwa wasafi lini? baadhi yao fedha walizonazo
walizipata kupitia madaraka waliyokuwa nayo serikalini, leo tena waletwe kwenu
eti ndiyo wagombea urais wa CCM, hapana litakuwa ni jambo la kushangaza sana,”
alieleza.
Post a Comment