Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu, Damian Lubuva |
Zipo za kuandikisha watu milioni 24 ifikapo
Julai 30,
Pia zipo siku 60 za mchakato wa zabuni vifaa
vya uchaguzi,
Kuna kibarua cha kugawa majimbo kuanzia
30.05.2015,
Nyingine ni zaidi ya siku 70 za kampeni uchaguzi
mkuu,
Kibarua hicho hakihusishi kura ya maoni
Katiba mpya.
Wakati bado ikielemewa
na majukumu mazito matano, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imezidi kujiongezea
mzigo mwingine zaidi, ambayo utekelezaji wake hadi kukamilika ndani ya siku 160
kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu kuwa miujiza.
MGAWANYO WA MAJIMBO:
Nec imejiongezea jukumu
lingine zito ambalo ni la sita baada ya kutangaza kuanza mchakato wa kuchunguza
mipaka na kugawa majimbo kwa ajili ya uchaguzi huo, huku ikitaja tarehe ya
mwisho ya kuwasilisha maombi kwa wadau wenye nia ya kugawa jimbo/majimbo
yanayokidhi vigezo kuwa ni Mei 31, mwaka huu.
Mchakato huo
ulitangazwa kupitia taarifa ya Nec iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari juzi
iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, R.K. Kairima.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, uamuzi wa Nec wa kujiongezea jukumu hilo umezingatia Ibara ya 74 (6) (c)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, ambayo inaipa tume hiyo mamlaka
ya kuchunguza mipaka na kugawa maeneo kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.
Pia umezingatia Ibara
ya 75 (4) ya katiba hiyo, inayoipa Nec uwezo wa kugawa majimbo mara kwa mara na
angalau kila baada ya miaka 10.
“Hivyo, Tume inakusudia
kuanza mchakato wa kuchunguza mipaka na kugawa majimbo kwa ajili ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Miongoni mwa vigezo
vitakavyotumika katika kuchunguza mipaka na kugawa majimbo ni pamoja na
mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu katika jimbo inayopatikana kwa kuchukua
idadi ya watu wote nchi nzima na kugawanywa kwa idadi ya majimbo yaliyopo.
Vigezo vingine ni idadi
ya watu iliyotokana na makisio ya ongezeko la watu hadi Julai, mwaka huu na
kwamba, majimbo yenye watu wengi yatafikiriwa zaidi; pia upatikanaji wa
mawasiliano, hali ya kijiografia, kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika na
mipaka ya kiutawala.
Vingine ni jimbo moja
kutokuwa ndani ya wilaya/halmashauri mbili, kata moja kutokuwa ndani ya majimbo
mawili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya Muungano,
uwezo wa ukumbi wa Bunge na viti maalumu vya wanawake.
Utaratibu utakaofuatwa
kuwasilisha maombi umetajwa kuwa ni maombi/mapendekezo ya kugawa majimbo au
kurekebisha mipaka kuwasilishwa kwa mkurugenzi wa halmashauri husika, ambayo
yatajadiliwa katika vikao rasmi.
“Inashauriwa vikao
hivyo vishirikishe wadau mbalimbali,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia mkurugenzi wa
halmashauri atawasilisha maombi/mapendekezo kwa Katibu Tawala (RAS), Katibu
Tawala Mkoa atayawasilisha katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ili
kupata maoni zaidi na katibu huyo atawasilisha mapendekezo Nec.
Taarifa hiyo imewataka
wadau wote wenye nia ya kugawa jimbo/majimbo yanayokidhi vigezo hizo
kuwasilisha maombi yao Nec kwa kufuata utaratibu huo.
Hata hivyo, taarifa
hiyo ilieleza kuwa maombi yote yaliyo chini ya mgawanyo wa wastani wa idadi ya
watu hayatafanyiwa kazi.
ZABUNI VIFAA VYA
UCHAGUZI.
Nec pia imeanzisha
mchakato wa zabuni ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya uchaguzi kwa kutoa
siku 60 kwa miongozo ya vitu 23 vinavyohitaji kuombewa zabuni na
wazabuni.
Kwa mujibu wa tangazo
lillitolewa na Nec katika Gazeti la Daily News la Mei 14, mwaka huu zabuni hizo
zilitangazwa na tume hiyo Mei 13, mwaka huu.
Tangazo hilo
limeelekeza kuwa Nec itafunga upokeaji wa maombi ya wazabuni watakaotaka kutoa
huduma na vitu vilivyoorodheshwa Mei 16, mwaka huu.
Katika tangazo hilo,
zabuni hizo zitaanza kutolewa Mei 23 kwa wazabuni ambao watakuwa tayari
wamehakikiwa Mei 17, mwaka huu.
Zabuni zilizotangazwa
na Nec kwa ajili kuombwa ni pamoja na usambazaji wa fulana, kofia, mikoba
ya waangalizi wa uchaguzi, kuchapisha na kusambaza karatasi za uchaguzi,
usambazaji wa wino wa kupigia kura, usambazaji wa vifaa vya uchaguzi na
mabetri.
Baadhi ya vitu na
huduma zilizotangazwa kuombewa zabuni, ni usambazaji wa vifungio vya makasha ya
kupigia kura, magurudumu, mafuta ya dizeli, kompyuta mpakato, mashine za
kuchapisha karatasi, magari, huduma za usafiri wa ndege, huduma za marekebisho
ya tovuti ya Nec.
Nyingine ni utoaji wa
tiketi za ndege, sehemu za kufanyia mikutano, malazi, dawa za kupulizia kuua
wadudu, chakula na vinywaji, ulinzi na vifaa vya kujikinga na moto, usambazaji
wa vifaa vya kompyuta, usambazaji wa vifaa vya kutolea elimu kwa wapiga kura,
vifaa vya kujikinga pamoja na vifaa vya kufanyia usafi.
DAFTARI BVR:
Wakati ikijiongezea
majukuku mengine, hadi sasa Nec bado inaelemewa na majukumu mengine
matano, likiwamo linalohusu uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la
wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR).
Uandikishaji huo, ambao
umekuwa ukisuasua tangu kuanza kwake Februari 23, mwaka huu katika mkoa wa
Njombe na hivyo, kusababisha kukwama kwa kura ya maoni iliyokuwa imetangazwa na
Rais Jakaya Kikwete kuwa ingefanyika Aprili 30, mwaka huu.
Uandikishaji katika
Mkoa wa Njombe ulikamilika katikati ya Aprili.
Hadi sasa mchakato,
ambao umekwishakamilika katika mkoa huo pekee, unaendelea katika mikoa ya
Ruvuma, Lindi, Mtwara na Iringa.
Awali, Nec ilitangaza
kuwa uandikishaji katika mikoa ya Mbeya, Dodoma, Tabora na Katavi ungeanza Mei
2, mwaka huu, lakini kwa sababu zizizojulikana haujaanza huku Nec ikiahidi kuwa
utaanza kesho.
KAMPENI
Jukumu lingine zito
linaloikaba koo Nec ni maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu ambazo kisheria
zinatakiwa kuchukua siku 72.
UCHAGUZI MKUU
Baada ya kampenni za
uchaguzi, Nec itakabiliwa na jukumu la kusimamia na kuratibu upigaji kura za
udiwani, ubunge na urais utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu sambamba na
kutangaza matokeo.
KURA YA MAONI
Hadi sasa haijajulikana
ni lini kura ya Katiba inayopendekezwa itafanyika.
Awali, Nec ilitangaza
kwua ingefanyika Aprili 30, lakini ilishindikana kutokana na kutokukamilika kwa
Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Kufuatia ahli hiyo, Nec
ilitangaza kuwa itakamilisha Daftari kabla ya julai, mwaka huu na kwamba suala
la tarehe ya kura ya maoni litafuata, baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (Zec).
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment