ASMK Foundation waguswa na hali ya usafi wa mazingira katika kituo cha kutunzia watoto wenye ulemavu wa ngozi (albinism) waliopo kituo cha Buhangija Shinyanga waamua kujitolea kufanya usafi na kupaka rangi baadhi ya majengo
SHIRIKA la ASMK Foundation lenye makazi yake mkoani Shinyanga limejitolea kutengeneza chumba maalumu kitakachotumika kwa ajili huduma za kliniki kwa watoto walemavu wa ngozi (albinism) waliopo katika kituo cha Buhangija Shinyanga kitakachogharimu shilingi milioni sita.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi mtendaji wa ASMK Foundation, Liliane Sykes Kwofie alisema mbali ya matengenezo ya chumba hicho pia wanachama wa shirika lake kwa kipindi cha wiki nzima watafanya usafi kwenye kituo hicho ikiwemo kupaka rangi katika majengo wanavyoishi watoto hao na kuwafulia nguo zao.

Liliane alisema gharama za ukarabati wa chumba cha kliniki zimetolewa kwa ushirikiano na wanafamilia wawili, Paul Singleton na Allice Singleton ambao ni mke na mume kutoka nchini Ireland kupitia kitengo chao cha Ireland Volunteers ambao pia wameshiriki katika shughuli za kufanya usafi.

Alisema baada ya ASMK kutembelea kituo hicho walibaini kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazowakabili watoto ikiwemo huduma za kiafya kutokana na kutokuwepo kituo cha huduma ya kwanza hivyo na kulazimika watoto wanaopatwa na tatizo kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa.

“Tumekuja hapa kufanya ukarabati wa moja ya vyumba vilivyopo ili kutengeneza kliniki itakayotoa huduma ya matibabu na kuchunguza afya za watoto hawa kila wakati, afya za watoto hawa zinahitajika kuchunguzwa kila wakati kutokana na miili yao ilivyo kuhitaji uangalizi wa kila mara,”

“Mbali ya kutengeneza chumba cha kliniki, pia sisi wana ASMK Foundation kwa wiki nzima hii tutafanya kazi ya usafi katika maeneo yote ya kituo ikiwemo kuwafulia nguo zao, kupulizia dawa za kuua wadudu katika vitanda na magodoro wanayolalia, maana hivi sasa tumebaini  hali ya mazingira hairidhishi sana,” alieleza Liliane.

Hata hivyo mkurugenzi huyo aliwaomba viongozi wa kiserikali mkoani Shinyanga kuangalia uwezekano wa kuteua muuguzi mmoja atakayetoa huduma za kuwahudumia watoto waliopo katika kituo hicho ambao mara nyingi huhitaji kupatiwa huduma za kiafya kutokana na mazingira ya miili yao ilivyo.

“Nafikiri ni wakati muafaka kwa uongozi wa Manispaa yetu kuiona hali hii, wateue muuguzi mmoja atakayekaa hapa muda wote, maana tayari kuna daktari aliyeteuliwa anayekuja kwa vipindi fulani kuangalia afya za vijana wetu hawa, wanahitaji uangalizi wa karibu muda wote kutokana na hali zao zilivyo,”

“Si vizuri kwa uongozi wa manispaa na serikali kwa ujumla kukaa pembeni katika kukishughulikia kituo hiki na kuliacha jukumu hilo kwa jamii yenyewe pamoja na wahisani mbalimbali, serikali ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto hawa wanaishi kwa amani huku wakiwa na afya njema,” alieleza Liliane.

Kwa upande wake mmoja wa wakurugenzi wa ASMK Foundation, Dkt. Sam Kwofie kutoka nchini Ghana na wafanyakazi wa kujitolea kutoka nchini Ireland Paul na Allice Singleton walisema walihamasika kufanya shughuli za usafi katika kituo hicho baada ya kuguswa na hali ya uchafu ilivyokuwa kituoni.

“Tumeona vyema tutoe mchango wetu kwa kufanya usafi na kuweka chumba cha kliniki ili kuwezesha watoto hawa waweze kuishi katika mazingira salama yenye afya nzuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ongezeko la watoto kituoni limechangia pia kuongezeka kwa hali ya uchafu, hivyo ni muhimu suala la usafi likazingatiwa,” alieleza Kwofie.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top