Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec), imesema vifaa BVR kits 2,098 zitatumika katika uandikishaji wa
wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura katika mikoa minne.
Mikoa hiyo ni Iringa,
Ruvuma, Mtwara na Lindi ambayo kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu
(NBS), itakuwa na jumla
ya watu wenye sifa za kupiga kura hadi siku ya Uchaguzi Mkuu ni 2,599,205.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva (pichani),
alisema vifaa hivyo ni 250 vinavyotumika kwenye uandikishaji mkoani
Njombe, 248 vilivyowasili hivi karibuni na 1,600 vinavyotarajiwa kuwasili
wakati wowote.
“Vifaa hivyo kwa pamoja
vitawezesha uandikishaji kwenye mikoa hiyo kufanyika kwa haraka na kadri
tutakavyoendelea kupokea vifaa ambavyo serikali imeshavilipia vitakwenda
kwenye mikoa hiyo.
Alisema kwa sasa BVR
kits 250 zinatumika kwenye mkoa wa Njombe na uandikishaji utamalizika Aprili
18, mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema
wakati wowote kuanzia leo Nec itatoa ratiba kamili ya uandikishaji kwenye mikoa
hiyo, ili kuwarahisishia wananchi kufika kwenye vituo kulingana na ratiba.
Hivi karibuni, Nec
ilitangaza kusongezwa mbele kwa tarehe ya kura ya maoni kwa Katiba
inayopendekezwa kutokana na kile kinachoonekana ni kushindwa kuandikishwa
kwa wapiga kura kwenye daftari la wapiga kura kutokana na kukosekana kwa
vifaa hivyo.
Nec ilisema tarehe ya
Kura ya maoni itatangazwa baadaye baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec)
Source: Nipashe
Post a Comment