Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la AMSK Foundation, Lilian Kwofie (wa kwanza kulia) akikabidhi msaada wa televisheni kwa mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku (katikati) na mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nhobola wilayani Kishapu, Mohamed Shamte (mwenye kofia) kwa ajili ya matumizi ya wanakijiji hicho. (Picha na Suleiman Abeid)


KISHAPU:

MKUU wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Wilson Nkhambaku amelipongeza Shirika la AMSK Foundation lenye makao makuu yake mkoani humo kwa juhudi zake za kuboresha elimu na miradi mingine ya kijamii  katika kijiji cha Nhobola kata ya Talaga katika wilaya hiyo.

Nkhambaku alitoa pongezi hizo juzi baada ya kutembelea darasa la awali ambalo watoto wa kijiji hicho hufundishwa masomo ya awali ikiwemo somo la lugha ya kiingereza ambapo katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa darasa hilo watoto hao wameonesha hali ya uelewa mkubwa kwenye masomo wanayofundishwa.

Pia mkuu huyo alikabidhi televisheni moja yenye thamani ya shilingi 250,000 iliyotolewa na Shirika hilo la AMSK Foundation kwa wanakijiji itakayowawezesha wakazi wake kupata taarifa za habari ikiwemo kufuatilia mijadala ya bunge la bajeti linaloendelea na vikao vyake hivi sasa na bunge la katiba litakapoanza mwezi Agosti mwaka huu.

Mbali ya kukabidhi televisheni hiyo, Nkhambaku alipata fursa ya kukagua kikundi cha akinamama wanaopatiwa mafunzo ya ushonaji wa nguo mbalimbali ambapo vyerehani vitatu vinavyotumika katika mafunzo hayo vilitolewa na Shirika hilo la AMSK Foundation kwa lengo la kuwasaidia wanawake wa kijiji hicho cha Nhobola.

Akizungumza na uongozi wa serikali ya kijiji hicho mkuu huyo alisema serikali itaendelea kutoa msaada wake kila pale utakapohitajika ili kuwezesha mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo wilayani humo yaweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo wakazi wa Kishapu.

“Sina budi kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Shirika la AMSK Foundation kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika kijiji hiki, kuanzia upande wa darasa la awali kwa watoto wetu, nimefurahishwa na jinsi wanavyojifunza kiasi cha kuwazidi hata kaka zao wanaosoma madarasa ya juu, hongereni kwa kazi nzuri,”

“Lakini pia hawa nimeridhishwa na kitendo chenu cha kutoa msaada wa vyerehani vitatu, tumeona pale mama zetu wanajifundisha ushonaji, mmenieleza wanapohitimu baadhi yao wanajinunulia vyerehani na kuweza kujiajiri wenyewe, ni wazi mafunzo waliyoyapata yamewasaidia, hivyo kuweza kujiongezea kipato ndani ya familia,” alieleza Nkhambaku.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Shirika la AMSK Foundation, Dkt. Sam Kwofie akitoa shukrani zake kwa mkuu wa wilaya, alisema lengo la misaada wanayoitoa katika wilaya hiyo ni kutaka kusaidiana na serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya jamii ya watu wa Kishapu hususani kijiji cha Nhobola ambacho wamedharimia kuwekeza zaidi.

Hata hivyo Dkt. Kwofie alisema mafanikio yaliyokusudiwa yatategemea na jinsi jamii yenyewe itakavyojipanga katika kushughulikia miradi yao mbalimbali ya kimaendeleo na kwamba ikiwa itajiwekea mipango mibovu ni wazi kasi ya maendeleo itakuwa ni ya kusuasua.

“Sisi AMSK Foundation tumedhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika kjiji cha Nhombola, tunataka baada ya kipindi kifupi kiwe mojawapo ya vijiji bora nchini na mfano wa kuigwa na vijiji vingine, ndiyo maana tumeona tuanze na suala la uboreshaji wa elimu, wanafunzi hawa wa awali tutawasimamia hadi wafikie elimu ya juu,” alieleza Dkt. Kwofie.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top