MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA KATIKA MOJA YA MIKUTANO YAKE YA HADHARA MKOANI SHINYANGA

 
Maelfu ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga wakiwasikiliza viongozi wa CHADEMA katika mkutano wa hadhara.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kusisitiza msimamo wake wa kususia zoezi la upigiaji kura katiba inayopendekezwa huku kikiwahimiza watanzania wasipoteze muda wao kwenda katika vituo vya kupigia kura ifikapo Aprili 30 mwaka huu badala yake waendelee na shughuli zao kama kawaida.
 
Msisitizo huo umetolewa na mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini humo ukiwa na lengo la kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.
 
Hata hivyo wakati mwenyekiti huyo akiwaomba wananchi kususia  upigiaji kura katiba inayopendekezwa amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba kupitia sanduku la kura pekee ndiko watakapoweza kufanya maamuzi sahihi ifikapo Oktoba 25, mwaka huu.
 
Mbowe alisema CHADEMA kwa ushirikiano wa vyama vingine vya siasa vinavyotetea katiba ya wananchi (UKAWA) wametangaza rasmi kususia upigiaji kura ya maoni katiba inayopendekezwa kwa vile upatikanaji wake haukuzingatia sheria wala kanuni na badala yake imepindishwa kwa nguvu na Chama cha Mapinduzi (CCM).
 
Alisema viongozi wote wa UKAWA baada ya kubaini ukiukwaji wa makusudi uliofanyika ndani ya bunge la katiba (BMK) wakati wa kuijadili rasimu ya katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba waliamua kutoka nje na kuacha kushiriki katika mchakato mzima kwa vile kilichokuwa kikijadiliwa hakikutokana na maoni ya watanzania.
 
“Baada ya kubaini maoni ya wananchi mengi yanakataliwa na kutupiliwa mbali tuliona tusishiriki katika kulinajisi taifa, tukaamua kutoka nje, wao waliamini tungerudi kwa ajili ya kufuata fedha, hapana tuliona heri tufe maskini kulikoni kushiriki katika kulichakachua taifa letu,”
 
“Ndugu zangu wa Shinyanga katiba inayotungwa siyo ya CHADEMA wala CUF bali ni katiba itakayoongoza maisha ya taifa letu, kwetu sisi leo, kwa watoto wetu na watoto wa watoto wetu, hivyo haistahili kufanyiwa mzaha, tulikubaliana bunge hili lisitishwe baada ya kubainika limekiuka kanuni, sheria na taratibu, lakini wenzetu waligoma,”
 
“Sasa leo wanatangaza kura ya maoni, wanataka tukashiriki kura ya maoni, tumeseme hatuendi, maana UKAWA tukishiriki ni sawasawa na kwenda kubariki mchakato uliokuwa haramu, japokuwa wapo wanaolaumu kwamba kususia kwetu kutasababisha CCM wapige kura ya ndiyo kupitisha katiba hiyo, si kweli,” alieleza Mbowe.
 
Akifafanua juu ya sababu za kuwashauri wananchi kususia upigaji kura huo mwenyekiti huyo alisema hata kama wasioitaka katiba hiyo watakwenda na kupiga kura ya hapana, bado watakuwa wamehalalisha kuendelea kutumika kwa katiba iliyopo hivi sasa ambayo pia ina mapungufu mengi na inatokana na CCM.
 
“Upigaji wa kura hii una sehemu mbili, ukipiga kura ya ndiyo utakuwa unaikubali ile iliyoandikwa na Chenge (Andrew) na ukiikataa hiyo ukapiga kura ya hapana, maana yake unakubali kuendelea na katiba iliyopo ambayo tunasema ni mbovu, hivyo basi ni vizuri tuwaache wafu wazike wafu wao, msipoteze muda,” alieleza.
 
Mbowe alisema mara baada ya serikali itakayoongozwa na UKAWA kuingia madarakani Oktoba 25, mwaka huu wataharakisha kurejesha mchakato wa katiba ya Jaji Warioba bungeni ili kuwezesha Taifa kupata katiba ambayo wananchi wameiridhia na siyo lazima katiba ipatikane sasa chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
 
Katika hatua nyingine Mbowe amewaomba wakazi wa mkoa wa Shinyanga wasaidie katika kuimarisha umoja wa UKAWA pamoja na vyama vya upinzani na kuwataka wananchi wachache ambao bado wako CCM wasome alama za nyakati na wajiunge na vyama vya upinzani ili kujenga nchi yao.
 
“Hiki kilio na msiba wa watanzania hatuwezi kuumaliza kwa kuiacha CCM madarakani, nawaomba muimarishe UKAWA na kila mmoja muda ukifika ahakikishe anakwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, na niwapongeze vijana waliozindua kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha nchi nzima, kila mmoja awe wakala wa kuhamasisha watu kujiandikisha,” alieleza Mbowe.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top