SPIKA WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR, PANDU AMEIR KIFICHO |
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana wamepitisha Sheria ya Kura ya
Maoni ya Katiba Pendekezwa kwa mvutano na vurugu baada ya wajumbe kutoka Chama
cha Wananchi (CUF) kuhoji uhalali wa sheria hiyo kutumika Zanzibar,
wakati kuna sheria yake ya kura ya maoni inayojitegemea.
Mvutano wa sheria hiyo ulianza kujitokeza mapema asubuhi kuhusu utaratibu
uliotumika kuwasilishwa kwake ikiwemo kuwemo katika orodha ya shughuli za
baraza na kukosekana katika taarifa za shughuli za Serikali.Hata hivyo wakati wa kujadili hoja hiyo, wajumbe wa pande ya upinzani walisimama na kuanza kuimba wimbo wa “Hatutaki udalali, hatutaki udalali.” Wakati huo pia wawakilishi CCM nao walisimama na kuanza kuimba; "CCM, CCM, CCM."
Hali hiyo ilisababisha vurungu ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, hivyo kumlazimisha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kuwaita askari wa baraza kunyanyua siwa na kuashiria kuahirishwa kwa kikao hicho cha Baraza la Wawakilishi.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya mjumbe wa Jimbo la Mjimkongwe, Ismail Jusa Ladhu, kulitaka baraza lisiridhie sheria hiyo na badala yake itumike sheria ya kura ya maoni ya Zanzibar.
Alisema hatua ya kuridhia sheria hiyo ikitumike Zanzibar ni sawa na kuifanyia udalali nchi na kuwataka wajumbe wasikubali kuwasilishwa sheria hiyo na kutumika.
“Zanzibar tunasheria yetu, kwanini tupitishe sheria nyingine hatua hii ni sawa na udalali dhidi ya nchi, jambo ambalo haliwezekani”, alisema.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said walilazimika kusimama na kutetea hoja ya sheria hiyo kuridhiwa na baraza hilo.
Hassan Said alisimama na kusema kuwa hoja ya Jusa imepitwa na wakati pamoja na Zanzibar kuwa na sheria yake, sheria hiyo imetungwa kwa ajili ya matumizi ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 66, Zanzibar ina wajumbe watano wanaowakilisha maslahi ya baraza ndani ya Bunge na kama kutetea wazo hilo ilitakiwa kujitokeza wakati wa kujadili na kupitisha sheria hiyo bungeni.
Alisema kwamba Baraza la wawakilishi halina mamlaka ya kujadili sheria zilizopitishwa na Bunge na kazi yake kubwa ni kuridhia kwa sheria ambayo imetungwa kwa jambo ambalo halimo katika orodha ya mambo ya Muungano.
Hata hivyo waziri Mwinyihaji alisema kauli ya Jusa haikuwa ya kiungwana na kumtaka afute kauli yake hiyo kwa kuliomba radhi baraza, ambapo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alisema suala hilo litafanyiwa utaratibu baadae.
Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi baada ya kura za wajumbe walioridhia kuwa nyingi.
Post a Comment