Maofisa kutoka Rafiki SDO wakiwa katika maandalizi ya kuwasafirisha watoto 50 kutoka mgodi wa Mwabomba. |
Mmoja wa watoto wanaotumikishwa katika migodi midogo ya dhahabu wilayani Kahama. |
Sehemu ya watoto walioibuliwa kutoka kwenye ajira za migodini - Mwabomba Kahama. |
Mratibu wa mradi kutoka Shirika la Terre des Hommes Samson Kube akitoa nasaha zake kwa watoto. |
SHERIA ya
mtoto ya mwaka 2009 inaeleza wazi kati ya mambo yanayokatazwa kutendewa watoto
chini ya umri wa miaka 18 ni kuajiriwa katika kazi ngumu au zile zinazotajwa
kama ajira hatarishi kwa mtoto.
Hata hivyo
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la 2005 Sehemu ya
pili katika Ibara ya 11 vifungu vidogo vya (2) na (3) vinaeleza, nanukuu, (2)
Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu
katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo
wake,”
(3) Serikali
itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za
kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za
shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo,” mwisho wa kunukuu.
Kwa mujibu
wa vifungu hivyo vya katiba ni wazi kwamba mtu ye yote anayemzuia mtoto kupata
elimu kwa kadri ya uwezo wake anakuwa amevunja katiba ya nchi na ukipatikana ushahidi
wa kutosha juu ya kitendo hicho anastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pamoja na
katiba kueleza na kufafanua wazi kuhusu haki ya kupata elimu kwa kila mtu
ikiwemo watoto lakini hapa nchini watoto wengi wamebainika kunyimwa haki hiyo
kutokana na hali ya kimaisha ndani ya baadhi ya familia inayosababisha watoto
kugeuzwa vitega uchumi na watafutaji wa kipato ndani ya familia.
Maeneo
ambayo yamekithiri kwa ukiukwaji wa haki za watoto ni pamoja na yaliyoko
kandokando ya migodi midogo midogo na mikubwa hususani ile ya dhahabu na
Tanzanite, maeneo ya wavuvi, uchimbaji wa kokoto na mchanga, mashamba ya
tumbaku na kwenye shughuli za uchomaji wa mkaa.
Pamoja na
kwamba ndani ya sheria ya mtoto ya mwaka 2009 vifungu vya 77 na 86 kuruhusu
watoto wenye umri wa kuanzia miaka 14 kufanya kazi nyepesi na kupata malipo
stahiki lakini hata hivyo ieleweke kazi zinazoruhusiwa ni zile zisizoathiri
afya mtoto husika.
Hata hivyo
kifungu cha 78 cha sheria hiyo ya mtoto kinazuia mtu ye yote kumwajiri mtoto
katika kazi ye yote ile ya kinyonyaji au ya hatari kwa maisha yake ambapo
katika sehemu ya pili kifungu cha 12 kinazuia watoto kuajiriwa katika kazi
zitakazosababisha waathirike kiakili, kielimu, kiafya au kuathiri maendeleo yao
ya kiroho.
Katika
kuangalia uhalisia utabaini bado katika maeneo mengi hapa nchini haki za watoto
wengi zimekuwa zikikiukwa bila ya kuwepo mtu au mamlaka yo yote inayokemea hali
hiyo na hivyo mtu akitembelea katika miji mingi mikuu hatokosa kukutana na
makundi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Kutokana na
hali hiyo baadhi ya mashirika na asasi mbalimbali za kiraia zinazojishughulisha
na utetezi wa haki za mtoto hapa nchini hivi sasa yanaendesha harakati
mbalimbali za kuwasaidia watoto walioko katika makundi hatarishi kwa lengo la
kuwasaidia ili waweze kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadae.
Mashirika na
asasi hizo yanaendesha miradi mbalimbali yenye lengo la kuwanusuru watoto
walioko katika hatari ya kujiingiza katika makundi hatarishi kwa wale wa kiume
na kwa upande wa watoto wa kike kuwaepusha na mimba na ndoa za utotoni vitendo
ambavyo katika siku za hivi karibuni vimekithiri katika mkoa wa Shinyanga.
Shirika la
kimataifa la nchini Uholanzi liitwalo, Terre des Hommes (TdH) jina lenye maana
ya Dunia ya wenye huruma hivi sasa linafadhili miradi miwili mikubwa mkoani
Shinyanga inayolenga kuwasaidia watoto mmoja ukiwa ni ule wa kutokomeza ajira
za watoto migodini.
Mradi huu wa
mwaka mmoja hivi sasa unatekelezwa wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga katika
halmashauri mbili za Msalala na Ushetu kwenye kata nne ambazo ni kata ya Isaka,
Chela, Lunguya na Idahina katika vijiji vitano vilivyopo katika kata hizo
kupitia mashirika manne ya kiraia yaliyopo katika wilaya hiyo.
Moja ya
mashirika hayo ni Shirika la Rafiki Social Organization Development (Rafiki
SDO) ambalo tayari limeanza kutekeleza mradi huo wa Tokomeza ajira za watoto
migodini katika maeneo ya Kata ya Mwabomba kuanzia Julai, 2014.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi huo mkurugenzi mtendaji wa shirika la Rafiki SDO, Gerald
Ng’ong’a anasema moja ya kazi kubwa inayotekelezwa na shirika lake ni kufanya
utafiti na kuwatambua watoto wanaofanya kazi katika migodi hiyo na kuwarudisha
shule kulingana na umri wao.
Ng’ong’a
anasema, “….Mradi wa tokomeza ajira za watoto migodini ni mradi unaotekelezwa
na shirika letu kwa ushirikiano wa mashirika mengine yaliyopo wilayani Kahama
ambayo ni SHIREMA, SHIHABI na HUHESO wote tukifadhiliwa na Shirika la kutoka
nchini uholanzi la Terre des Hommes,”
“Mbali ya
lengo la kuwatambua watoto walioko katika maeneo ya migodi midogo, lakini kubwa
zaidi ni kuhakikisha tunatokomeza utumikishwaji wa watoto walio chini ya umri
wa miaka 18 kwenye migodi hiyo iliyopo wilayani Kahama.”
Mkurugenzi
huyo anasema shirika hilo linatekeleza mradi huo kwa kuzingatia malengo
mahususi ya uanzishwaji wake ambapo mbali ya kupiga vita ajira mbaya kwa watoto
lakini pia linajishughulisha na utetezi wa haki za watoto na vijana mkoani
Shinyanga.
Anasema hadi
kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba, 2014 tayari shirika lake lilikuwa
limewatambua watoto 4,200 walioko katika maeneo ya migodi wilayani Kahama ambao
miongoni mwao watoto 800 ilibainika wanafanya kazi katika migodi hiyo huku
wakiwa ni wanafunzi katika shule za msingi.
“Lengo la
mradi huu ilikuwa tuutekeleza ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu, lakini baada
ya kufanyika kwa utafiti wa kina tumebaini ukubwa wa tatizo, kuna watoto wengi
wameacha shule na kukimbilia migodini, na hii inatokana na hali ngumu ya maisha
miongoni mwa familia zinazoishi kandokando ya migodi hiyo,”
“Kwa hali
hiyo tayari tumeanza mazungumzo na mfadhili wetu Shirika la Terre des Hommes
ili kuangalia uwezekano wa kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi huu ili
angalao sasa ufanyike kwa kipindi cha miaka mitano tuweze kuwaibua na kuwaondoa
katika ajira hatarishi watoto wote walioko migodini,” anaeleza Ng’ong’a.
Anasema
lengo la hivi sasa ni kuwasaidia watoto 800 waliokwisha ibuliwa katika migodi
midogo ya Nhumbi, Nyangalata, Mwabomba na Nyamtengela ambao baadhi wanaobainika
kutoroka shule wanarudishwa ili waendelee na masomo yao na wengine wanapelekwa
katika vyuo vya ufundi kufundishwa ufundi wa fani mbalimbali.
“Mpaka hivi
sasa tumeishafanikisha kupeleka watoto 150 katika vyuo vya ufundi vya Malampaka
FDC wilayani Maswa mkoa wa Simiyu, Mwananla FDC na Nzega FDC wilayani Nzega
mkoa wa Tabora, na hivi karibuni tutapeleka watoto wengine 100 katika vyuo
hivyo,”
“Lakini pia
mradi unashughulika na kazi ya kuwajengea uwezo wazazi wa watoto wote
wanaotolewa katika ajira mbaya ambao kwa sehemu kubwa walikuwa wakitegemea
kipato kutoka kwa watoto hao, tunawafundisha elimu ya ujasiriamali na
kuwaanzishia vikundi vidogo vya uzalishaji mali,” anaeleza Ng’ong’a.
Anasema
lengo la kuwasaidia wazazi hao ni kuwawezesha waweze kujitegemea badala ya kuwa
tegemezi kwa watoto wao na kwamba wasipojengewa uwezo kuna hatari hata pale
watoto waliondolewa katika ajira mbaya watakapomaliza mafunzo yao wakajikuta
wanajerea walikotoka na hivyo kazi yote iliyofanyika kupoteza maana.
“Lakini pia
mradi huu umejikita katika kutoa elimu kwa kamati za ulinzi wa watoto na
viongozi wa serikali za vijiji juu ya jinsi ya kuwashawishi watoto kuachana na kazi
za migodini pamoja na kuandaa mpango wa utekelezaji wa mradi mzima,” anaeleza.
Hata hivyo
mkurugenzi huyo anasema pamoja na juhudi zinazotekelezwa na asasi mbalimbali za
kiraia katika kuwasaidia watoto hao bado halmashauri za wilaya kwa upande wake zinawajibika
kuanza kujipanga kuangalia jinsi gani zitaweza kuwasaidia mara baada ya
kumaliza mafunzo yao vyuoni.
“Ni muhimu
hivi sasa halmashauri zote ambako watoto hawa wameokolewa zianze mpango mahsusi
wa kutenga bajeti itakayowezesha kuwasaidia pale watakapohitimu mafunzo yao kwa
kuwapatia mitaji midogo itakayowawezesha waweze kujiajiri wenyewe badala ya
kuendelea kuwa tegemezi,”
“Lakini pia
kuna umuhimu wa halmashauri hizi kujitungia sheria ndogo katika maeneo yake ya
vijijini zitakazowabana wamiliki wa migodi watakaokutwa wakiendelea kuajiri
watoto wadogo kinyume cha sheria ya mtoto na kutoa elimu kwa serikali za vijiji
juu ya umuhimu wa kumlinda mtoto bila kutegemea watu wa nje,” anaeleza
Ng’ong’a.
Kwa upande
wake mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Terre des Hommes (TdH), Samson Kube
anasema kwa sasa shirika lake linatekeleza mradi huo kwa ushirikiano wa asasi
nne za kiraia zilizopo wilayani Kahama katika mkoa wa Shinyanga na kwamba lengo
kuu ni kupunguza tatizo la ajira mbaya kwa watoto chini ya umri wa miaka 18.
“Mradi huu
umepangwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, lakini hata hivyo kwa
hali ilivyo tumebaini tatizo ni kubwa, tunafanya mawasiliano ili kuangalia
uwezekano wa kuongeza muda badala ya mwaka mmoja iwe ni miaka mitano, maana
tumebaini kuna kundi kubwa la watoto chini ya umri wa miaka 18 waliozagaa
katika migodi iliyopo Kahama," anaeleza Kube.
Post a Comment