Hatimaye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametangaza rasmi kuwa Makao makuu ya
Mkoa Mpya wa Songwe uliopendekezwa kuundwa kutoka sehemu ya Mkoa wa
Mbeya sasa yatakuwa wilaya ya Mbozi.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara alioufanya katika
viwanja vya Vwawa Mbozi, Pinda amesema kinachoenda kufanyika sasa ni
kuigawa wilaya ya Chunya ili sehemu ya wilaya hiyo kubakia mkoa wa Mbeya
na sehemu nyingine kuunda wilaya mpya itakayoungana na wilaya za Mbozi,
Ileje na Momba ili kuunda mkoa wa Songwe.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na wananchi wa Mbozi kutokana na mvutano wa muda mrefu wa wapi mkoa huo utakuwa makao makuu, hatua ambayo wakati fulani baadhi ya wilaya zilitishia kupiga kura za maruhani katika chaguzi zijazo.
Ameagiza wilaya ya Mbozi kutenga eneo ambalo litakuwa makao makuu ya mkoa huo ili kurahisisha wakati wa kutekeleza hatua ya ujenzi wa mkoa, aidha ameitaka wilaya ya mbozi kuanza mchakato wa kuigawa halmashauri ya Mbozi ili kupata halmashauri nyingine kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wananchi ambayo inakaribia 500,000
Amesema wilaya hiyo ki eneo, ina kilometa za mraba 3400 ambazo hazitosherezi kuigawa wilaya kuwa mbili na badala yake idadi ya watu ndiyo inayoibeba wilaya hiyo hivyo ili kuruhusu ugawaji ni vyema wakaangalia uwezekano wa kuomba halmashauri nyingine kusogeza huduma kwa wananchi.
Post a Comment