Moja ya Nyumba zilizoezuliwa na upepo katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama. |
Mbuzi hawa ni miongoni mwa mifugo iliyokufa kutokana na mvua hiyo iliyoambatana na upepo na mawe makubwa ya saruji. |
WATU 42
wakazi wa kijiji cha Mwakata kata ya Mwakata wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga
wamekufa huku wengine 89 wakijeruhiwa vibaya baada ya nyumba zao kubomolewa na
mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 4, mwaka huu ikiambatana na upepo mkali na mawe
makubwa ya saruji.
Mbali ya
kupoteza maisha ya watu pia mifugo kadhaa ikiwemo ng’ombe, mbuzi na punda
imekufa kufuatia mvua hiyo iliyonyesha kijijini hapo kwa zaidi ya saa moja huku
ikiharibu mazao mbalimbali ya chakula mashambani na kuacha familia kadhaa
zikiwa hazina makazi.
Baadhi ya
wakazi wa kijiji hicho walionusurika katika tukio hilo wamelieleza Majira
kwamba mvua hiyo ilianza kunyesha mnamo saa 4.00 usiku hadi saa 5.02 usiku wa
kuamkia Machi 4, 2014 ikiambatana na upepo mkali na mawe makubwa ya saruji yenye ukubwa
wa ndoo ndogo za plastiki zenye ujazo wa lita 10.
Wanakijiji
hao walisema maeneo yaliyoathiriwa vibaya na mvua hiyo ni pamoja na kijiji cha
Mwakata, Nhumbi na Mangung’humwa katika kata hiyo ya Mwakata na kwamba mpaka
sasa familia kadhaa hazina makazi baada ya nyumba zao kubomoka.
“Mimi
binafsi nyumba zangu mbili zimebomolewa na baadhi ya wateja wangu waliokuwa
katika matibabu (tiba za jadi) wawili wamejeruhiwa na wamepelekwa hospitali ya
serikali mjini Kahama kupatiwa matibabu, mvua hii imetushangaza sana, maana
ilikuwa inateremsha mawe makubwa mfano wa ndoo ndogo,”
“Watu wengi
wamepoteza maisha, hali hii haijawahi kutokea hapa kwetu hata wakati wa mvua
zile za El-nino haikuwa hivi, ni hatari sana maana watu wengi wameangukiwa
nyumba wakiwa ndani na wengine kujeruhiwa na mawe ya mvua, maana yalikuwa
makubwa sana,” alieleza Machimu Ndalo ambaye ni mganga wa jadi kijijini hapo.
Akizungumzia
tukio hilo mkuu wa wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema watu 35 walifia
katika eneo la tukio huku wengine watatu wakifia katika hospitali ya wilaya
mjini Kahama walikopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Ni kweli
kumetokea maafa makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa
kuamkia leo (jana), na hapa ninapozungumza na wewe tayari tumeopoa miili ya watu
35 iliyokuwa imefunikwa na nyumba zilizoanguka, hali ni mbaya sana, wengine
watatu wamefia hospitali mjini Kahama mida hii,” alieleza Mpesya.
Hata hivyo
mkuu huyo alisema mpaka hiyo jana mchana walikuwa bado wanaendelea na ukaguzi
zaidi katika kila kaya ili kuweza kubaini idadi halisi ya watu waliopoteza
maisha kutokana na mvua hiyo na ukubwa wa hasara iliyopatikana ikiwemo mifugo
na mazao yaliyoharibika.
Naye Kamanda
wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Elisa Mugisha alisema baada
ya kupata taarifa za kuwepo kwa tukio hilo kikosi cha Zimamoto kilikwenda
katika kijiji hicho kwa ajili ya shughuli za uokoaji sambamba na kuwawahisha
katika hospitali ya wilaya majeruhi waliojeruhiwa na mvua hiyo.
Kwa upande
wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga alithibitisha kutokea kwa vifo vya
watu 42 na majeruhi 89 waliopatikana na kukimbizwa katika hospitali ya serikali
mjini Kahama kupatiwa matibabu na kwamba idadi kubwa ya waliokufa ni watoto
wadogo.
Post a Comment