Mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaitwa: Ridhiwan Kikwete.
MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan Kikwete, amesema mzee wake (Kikwete) hana ugomvi wala uhusiano mbaya na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa; na kwamba kama kungekuwa na ugomvi, basi yeye angekuwa anajua hilo.


Ridhiwan alitoa kauli hiyo alipohojiwa na Televisheni ya Star TV kupitia kipindi chake cha Changamoto za Kisiasa kwa Watoto wa Viongozi. “Wanaosema uhusiano wa mzee (Rais Kikwete) na Lowassa ni mbaya ni waongo, si mbaya... tatizo baadhi ya Watanzania wana tabia ya kupika vitu ili wafanikiwe,” alisema Ridhiwan na kusisitiza;

“Sijawahi kumwona mzee akiwa na ugomvi na huyu bwana (Lowassa) na hili lazima nilisema, mimi nimeenda Ikulu zaidi ya mara tatu na kumkuta mzee (Rais Kikwete) akiwa na Lowassa.”

Alisema baba yake hapendi ugomvi na
wala hapendelei kuingia kwenye ugomvi na
mtu.

Alipoulizwa na mwongozaji wa kipindi
kuwa kuna taarifa za kuvutana kisiasa kati ya Rais Kikwete na Lowassa na kwamba kuna wakati upande wa Rais Kikwete, umekuwa ukivutana na upande wa Lowassa kisiasa na wa Lowassa kuibuka mshindi, Ridhiwan alisema;

“Hakuna siasa za kuvutana kati ya mzee na Lowassa, bali wanaosema hivyo wanataka kutengeneza mpasuko,” alisema na kusisitiza kuwa Rais Kikwete hana ugomvi na Lowassa.

Alisema; “Rais Kikwete ana vyombo vyote..nyie mnaona marais wengine wanayofanya... kama angekuwa na jambo na Edward mimi ningejua.” Alisema tatizo lipo kwenye media hawataki kueleza ukweli...hawataki kuweka vitu ambavyo watu wangependa kusikia.

Alipoulizwa kuhusu kinyang’anyiro cha urais ni mtu gani yeye anamuona anafaa kuwania nafasi hiyo, Ridhiwan alisema CCM ina watu wengi wanaofaa kuwa viongozi, akitaja hawawezi kuwamaliza hivyo wale ambao hatawataja atakuwa hajawatendea haki.
“CCM ina watu wengi sana nikitaja wengine sitawatendea haki kwa kutowataja, wapo wengine wenye sifa waliopo nje tutaangalia kati ya hao nani mwenye sifa ya kupeperusha bendera yetu,” alisema Ridhiwan na kutolea mfano mwaka 2005
akisema kati ya wagombea tatu waliokuwa
wamebaki, ungesema nani anafaa angekuwa
Salim Ahamed Salim.

Wagombea hao alikuwa Salim Ahamed Salim, Profesa Mark Mwandosya na Rais Jakaya Kikwete. Alisema Salim alikuwa na uzoefu wa uongozi kimtandao na ndani ya nchi, huku Profesa Mwandosya akiwa msomi mzuri na Rais akiwa na uzoefu wa uongozi Serikalini na ndani ya chama.

“Lakini Mzee Mkapa (Benjamin) hakuwa na uwezo wa kuwachagulia wanachama mtu anayemtaka, wanachama waliamua wenyewe na kumpitisha Rais Kikwete, hivyo ndivyo ilivyo kwenye chama chetu,” alisema.

Alipoulizwa ni kitu gani atakumbukwa nacho Rais Kikwete, endapo ataondoka madarakani; Ridhiwan, alisema; “Akiondoka madarakani Watanzania watamkumbuka kwa kuimarisha demokrasia...anastahili kupewa cheo cha baba wa demokrasia.”

Alisema asingekuwa mtu wa demokrasia angekuwa amefuta vyama vya siasa na hata
kuwaondoa nchini baadhi ya watu. “Watu wanakaa kwenye televisheni wanasema rais
legelege, dhaifu...huwezi kumuita mzazi au baba wa mtu dhaifu, lakini tukimuuliza mzee huwa anajisikia vipi akiitwa hivyo, anasema huo ndio uongozi.”

Ridhiwan alisema maendeleo si barabara peke yake, bali ni pamoja na kuwapa watu uhuru wa kuzungumza. Ridhiwan alipoulizwa taarifa kwamba ana utajiri kupindukia, alisema taarifa hizo si za kweli.

“Unaposema Ridhiwan ana majumba, basi yatajwe yapo wapi, sema nina nyumba ipo Dodoma karibu na CCM, lakini hawasemi.
Unaposema ninamiliki vituo vya mafuta, basi vitaje sema ninamiliki Oil com,” alisema na
kuongeza kwamba yeye anamiliki nyumba moja jijini Dar es Salaam ambayo alikuta
imeanzishwa ujenzi na mzee wake (Rais Kikwete) aliyompa wakati anataka kuoa.

Alisema hataki kujilimbikizia mali, maana
akijilimbikizia mali hiyo haitakuwa sehemu
ya mali za ndugu zake.

Source:  Majira News
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top