Mmoja wa wanawake hao akitoa tamko rasmi kwa niaba ya wenzake huku baadhi ya mahakimu (hawako pichani) wakiwa wamepigwa butwaa!!!! |
Sehemu ya akina mama kutoka Lubaga Manispaa ya Shinyanga wakiwa nje ya viwanja vya mahakama wakisubiri kupaaza sauti zao kulaani kitendo cha kuachiwa huru kwa mshitakiwa katika kesi ya ubakaji. |
Sehemu ya mahakimu na mawakili wa kujitegemea wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. |
Hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Shinyanga, John Chaba akitoa salaam za Siku ya Sheria nchini kwenye maadhimisho yaliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya mkoa wa Shinyanga. |
Katika hali isiyokuwa ya kawaida kikundi
cha wanawake wapatao 20 kutoka eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga kimevamia
katika viwanja vya mahakama muda mfupi baada ya mgeni rasmi katika maadhimisho
ya Siku ya sheria nchini kumaliza hotuba yake.
Wanawake hao ambao nyuso zao
zilionesha dhahiri shahiri kuwa na machungu makubwa waliwaita waandishi wa
habari waliokuwa pia wamehudhuria maadhimisho hayo ya siku ya sheria na
kuwaeleza kuwa wamefika pale kwa lengo kupaaza sauti zao katika viwanja hivyo
vya mahakama baada ya kuzuia na dola maandamano ya amani kulaani vitendo vya
kubakwa kwa watoto wadogo.
Katika tamko lao akina mama hao
walidai wanapinga kitendo cha hivi karibuni kilichofanywa na mahakama ya wilaya
ya Shinyanga kumuachia huru mshitakiwa Eugen Mwaluko aliyekuwa ameshitakiwa kwa
kosa la kumbaka mtoto mdogo mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia maumivu
makali hukumu iliyowashangaza wakazi wengi wa mji huo.
Wanawake hao
walielezea kushangazwa kwao na uamuzi huo na kudai ndiyo unaochangia kuendelea
kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto mkoani Shinyanga na kuiomba serikali
iingilie kati kwa kufuatilia mwenendo mzima wa kesi hiyo ambayo wamedai rushwa
imetumika na kupindisha ushahidi halisi pamoja na mtoto kumtambua mahakamani
mshitakiwa.
Wakifafanua walisema
hukumu ya kesi iliyotolewa hivi karibuni na Hakimu mkazi Neema Gasabile
ikimuachia huru mshitakiwa kwa madai ya ushahidi uliotolewa na upande wa
mashitaka mbele ya mahakama haukutosheleza kumtia hatiani mshitakiwa imeonesha
wazi jinsi kesi hiyo ilivyotawaliwa na mianya ya rushwa tangu mwanzo.
“Sisi
akina mama tumeamua kuja hapa leo ikiwa ni siku ya sheria nchini kupaza sauti
zetu kupinga vikali kitendo cha kuachiwa huru mshitakiwa aliyembaka mtoto
mwenye umri wa miaka tisa ambaye pia ana matatizo ya moyo wake kuwa mkubwa,
tunaamini haki haikutendeka kabisa, ni wazi rushwa ilitumika kupindisha haki,”
“Pamoja na
mtoto huyo kuonesha wazi ameharibiwa katika sehemu zake za siri, bado mahakama
imedai ushahidi hautoshelezi, hata hivyo tunahoji kitendo cha fomu namba tatu
inayotolewa na polisi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo iliyojazwa awali kupotezwa
kwa makusudi ili kuharibu ushahidi,”
“Lakini
kilichotushangaza ni kesi kusikilizwa na mahakimu wawili tofauti, pia
wanasheria waliokuwa wakiisimamia walibadilishwa mara tatu ilipokuwa
ikiendelea, hata hivyo kuanzia polisi upande wa dawati la jinsia, ustawi wa
jamii na madaktari walionesha wazi kufanya mambo kinyume na taratibu zao za
kiutendaji kazi,” alieleza Kareny Kimambo mmoja wa wanawake hao.
Akina mama hao
walihitimisha kupaaza kwao sauti mahakamani hapo kwa kuiomba serikali, vyama
vya wanaharakati vinavyopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na vyombo vya
habari kusaidia ili haki ya mtoto aliyebakwa iweze kupatikana ambapo walidai
hata baba wa mtoto hivi sasa anazungushwa kupewa nakala ya hukumu ili aweze
kukata rufaa.
Hivi karibuni
mahakama ya Hakimu mkazi Shinyanga ilimuachia huru mshitakiwa Eugen Mwaluko
aliyekuwa ameshitakiwa kwa kosa la kumbaka na kumsababishia maumivu mtoto
mwenye umri wa miaka tisa anayesoma darasa la tatu baada ya mahakama hiyo kudai
ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka haukutosheleza
kumtia hatiani mshitakiwa huyo.
Hata hivyo kwa upande wake hakimu aliyesoma hukumu ya kesi hiyo, Neema Gasabile hivi karibuni alitoa ufafanuzi kwa kueleza hakuna eneo lolote ambalo mahakama hiyo imepindisha maamuzi yake na kwamba kuachiwa huru kwa mshitakiwa huyo kunatokana na upande wa mashitaka kushindwa kutoa ushahidi mahakamani hapo usioacha shaka.
“Ni kweli nimemuachia huru mshitakiwa aliyekuwa
akishitakiwa katika kesi ya jinai namba 1 ya mwaka 2015, Eugene Mwaluko, hii ni
baada ya kukosekana ushahidi unaomtia hatiani, hapakuwa na kesi ya kulawiti
bali ilikuwa ni kesi ya kawaida ya ubakaji,”
“Katika kesi hii ushahidi wa mhanga (mbakwaji) ambao
haukuwa wa kiapo kwa vile ni mtoto ulikosa ushahidi wa kuungwa mkono na hivyo
kuacha shaka kwa upande wa mahakama, lakini pia maelezo yaliyoandikwa katika
fomu namba tatu ya matibabu yalipingana na aliyotoa daktari mahakamani
hapa,” alieleza Gasabile.
Post a Comment