Na Suleiman Abeid,
Shinyanga

ASKARI Polisi wawili wa kituo kidogo cha Polisi cha Manghu Salawe wilayani Shinyanga wanatuhumiwa kuwashambulia kwa kuwapiga risasi raia watatu na kumvunja mmoja wao miguu yake yote miwili pasipo sababu za msingi.

Tukio hilo lilitokea Agosti 10, mwaka huu saa 3.00 asubuhi huko katika kijiji cha Mwagiligili mpakani mwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga ambapo mwananchi aliyevunjwa miguu ametajwa kwa jina la Bw. Philipo Yusufu (25) mkazi wa kijiji cha Kakola wilayani Shinyanga.

Mbali ya shambulio hilo dhidi ya raia pia polisi hao wanatuhumiwa kumbambikizia mashitaka ya uongo majeruhi huyo baada ya kubaini kuwa wamemjeruhi ambapo walimlazimisha kuweka sahihi katika maelezo ambayo yaliandikwa na polisi wenyewe huku akiwa hoi kitandani hospitalini Bugando.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza wodi namba 805, Bw. Yusufu alisema wakati anapatwa na mkasa huo alikuwa na nduguze wengine wawili, Bw. Nicholas Titus mkazi wa Ngokolo Shinyanga na Bw. Selemani Malosha mkazi wa Kakola.

Bw. Yusufu alisema siku hiyo ya tukio walikuwa katika gari lenye namba T. 825 AME Mitsubishi Canter lililokuwa likiendeshwa na Bw. Titus wakitokea wilayani Kahama kuelekea katika machimbo ya dhahabu yaliyoko katika kijiji cha Ishokelahela wilayani Misungwi ambako ndiko wanakofanyia shughuli zao.

Alisema wakiwa njiani wakiendelea na safari katikati ya vijiji vya Solwa na Ikonongo Salawe walisikia sauti ya kishindo kikubwa nyuma ya gari lao na wakahisi huenda tairi moja la gari lao limepasuka.

“Dereva alitaka kupunguza mwendo ili kuweza kubaini kilichotokea, lakini alipochunguza kwa kupitia kioo kinachomsaidia kuona nyuma, aliona nyuma yetu kuna watu wawili waliokuwa wamepakizana katika pikipiki wakitufuata kwa kasi huku mmoja akiwa na bunduki aina ya SMG,” alieleza Bw. Yusufu na kuongeza,

“Baada ya kubaini hali hiyo, Bw. Titus alitueleza kuwa kuna watu ambao anahisi ni majambazi yakitufuata, na hivyo aliongeza mwendo wa gari katika kujaribu kuwaacha watu hao umbali mrefu,” alieleza.

Alisema wakiwa kilometa chache kabla ya kufika katika kijiji cha Manghu Salawe ilipigwa risasi nyingine iliyopasua tairi moja la nyuma hali iliyosababisha gari liache njia lakini dereva aliendelea kuliongoza kwa kutumia njia za pembeni na baadae kwa mbele walikwenda kuunga katika barabara iliyokuwa ikielekea katika kijiji cha Ishokelahela.

Aliendelea kueleza kuwa wakati huo watu wale wa pikipiki walikuwa wakiendelea kuwafukuza bila ya kujali vumbi walilokuwa wamelipata ambapo walifyatua risasi nyingine mbili na moja ilipiga upande wa kulia wa gari na kuingia sehemu aliyokuwa amekaa yeye.

Bw. Yusufu alisema risasi hiyo ilitoboa mguu wake wa kulia na kutokea upande wa pili ambapo pia ilipiga mguu wa kushoto ikatoka na kuikosa mikono ya dereva (Bw. Titus) na ikitoboa upande wa pili wa bodi la gari lao.

“Kwa kweli nilipiga kelele za uchungu na kumuomba dereva asimamishe gari kwa vile nimeumizwa na risasi, lakini hata hivyo gari lilisamama lenyewe kutokana na kugonga jiwe mbele, na papo hapo wenzangu walitoka ndani ya gari na kukimbia kutafuta msaada mimi sikuweza kwa vile tayari nilikuwa nimejeruhiwa,” alieleza Bw. Yusufu.

Alisema baada ya gari kusimama wale watu wawili walifika na kudai kuwa ni polisi huku wakimuuliza kwa nini walikuwa wanawasimamisha lakini wanakataa kusimama na kuhoji walikokimbilia wenzake, ambapo yeye aliwajibu kuwa hawakuona kama kuna sehemu yoyote waliyosimamishwa.

Hata hivyo alisema pamoja na polisi wale waliokuwa wamevaa mavazi ya kiraia kubaini kuwa wamemjeruhi lakini hawakuchukua hatua zozote za kuweza kumuwahisha hospitali mpaka pale alipopita msamaria mwema baada ya kusikia kilio chake cha kuomba msaada ambaye alipiga simu kuagiza gari lililofika na kumpeleka katika kituo cha afya cha Ikonongo.

Hata hivyo alisema kituoni hapo hakuweza kupatiwa huduma zozote za matibabu baada ya kushauriwa awahishwe katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza ambako alipokelewa saa 11 jioni na kupatiwa matibabu mnamo saa sita usiku.

Akizungumzia suala la kubambikizwa kesi, alisema siku ya pili akiwa hospitalini hapo, polisi aliyempiga risasi aliyemtambua kwa jina la Edson, alifika akiwa na mpelelezi kutoka kituo cha polisi Shinyanga wakidai walikwenda kumjulia hali.

Bw. Yusufu alisema wakati akiongea kwa shida na polisi hao kutokana na maumivu aliyokuwa nayo wakati huo polisi walikuwa wakiandika vitu ambavyo hakufahamu lakini baadae walimuomba aweke sahihi na alipojaribu kukataa walimsihi afanye hivyo kwa madai kuwa walichoandika ni kile walichoongea pale.

“Kwa vile nilikuwa nahisi maumivu makali nilikubali kuweka sahihi, lakini baadae wagonjwa wenzangu walinilaumu kuwa nimekosea ningeomba kwanza nisomewe kile kilichoandikwa, basi sikuwa na jinsi, lakini ndugu yangu anayenisaidia hapa yeye alikataa kuweka sahihi yake katika karatasi aliyopewa,” alieleza Bw. Yusufu.

Alisema katika karatasi ya pili aliyopewa ndugu yake pia aweke sahihi alipoisoma (nduguye) alibaini ilikuwa ni fomu ya dhamana akitakiwa kumdhamini Bw. Yusufu kwa shilingi milioni mbili kwa vile anatuhumiwa kupatikana na mali inahohisiwa kuwa ni ya wizi kitu ambacho nduguye alikanusha kwa kudai pale hapakuwa na mtuhumiwa yeyote waliyemkamata.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Daudi Siasi alikiri kupata taarifa kwa ufupi juu ya tukio hilo ambapo alisema alikuwa ameelezwa kuna watu walikamatwa na mali inayohisiwa kuwa ni ya wizi.

“Ni kweli nimepata taarifa fupi juu ya kuwepo kwa tukio hilo, lakini siyo kama mnavyonieleza ninyi (waandishi) nilimwambia OCD alifuatilie, lakini sasa naona nitalifuatilia mwenyewe, kama kweli polisi wamefanya kitendo hizo wamefanya kosa, na ninaomba waelezeni ndugu za majeruhi waje ofisini kwangu jumatatu waweze kunipa picha halisi,” alieleza Bw. Siasi.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top