MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA.
Kifungo cha miezi 12 walichopewa makada sita wa CCM kwa kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho na kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati, kinamalizika ndani ya saa 24 na hatma yao kusubiri tathimini itakayofanywa na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo au la.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo unaelekea ukingoni  na kufafanua kuwa viongozi hao watafanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini kama walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo.

Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Vilevile baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.

Kutokana na adhabu ya onyo kali makada hao kwa mwaka mzima walikuwa katika hali ya kuchunguzwa ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.

Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe), kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.

Makada hao waliokuwa chini ya adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Chanzo cha Habari: Gazeti la Mwananchi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top