Mapigano bado yanaendelea
nchini Ukraine na yamejikita zaidi katika mji wa Debaltseve, Mashariki mwa
nchi. Hata hivyo mamia ya wanajeshi wanasemekana kusalimu amri na kuondoka
mjini humo.
Waasi
wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine wamedai kuteka asilimia 80 ya mji wa
Debaltseve, mji wenye kituo cha reli chenye umuhimu mkubwa. Hata hivyo serikali
ya Ukraine imekanusha taarifa hizo.
Kwa
mujibu wa wizara ya ulinzi ya Ukraine, baadhi ya wanajeshi wametekwa nyara
mjini Debaltseve. Nalo shirika habari la kundi la waasi linasema mamia ya
wanajeshi wamesalimu amri na kujitoa kwenye eneo la mapigano. Wakati huo huo,
waasi wanaondoa silaha nzito kwenye maeneo ambapo amani imerejea.
Umoja
wa Mataifa umelaani kuendelea kwa mgogoro nchini Ukraine. Nalo baraza la
usalama la Umoja huo limepitisha azimio ambalo linataka pande zote mbili
ziheshimu makubaliano ya amani yaliyosainiwa wiki iliyopita. Urusi,
iliyopendekeza azimio hilo, imesisitiza kwamba inatamani kuona amani ikirejea
Ukraine.
Vitali
Churkin ambaye ni balozi wa Urusi kwa Umoja wa Mataifa alisema: "Tangu
kuanza kwa mgogoro huu, Urusi imetaka pawe na suluhu itakayoletwa kwa njia ya
amani. Tumefanya kila tuwezalo kutoa nafasi ya mazungumzo kuhusu masuala ya
siasa na katiba na tutaendelea kufanya hivyo siku zijazo."
Putin akanusha kuhusika
Lakini
Ukraine pamoja na nchi za Magharibi, kama vile Marekani na Ujerumani,
zinainyooshea kidole Urusi zikisema nchi hiyo imejihusisha moja kwa moja katika
mgogoro wa Ukraine kwa kutuma wanajeshi kuwaunga mkono waasi na pia kuwapatia
waasi hao silaha.
Makamu
wa rais wa Marekani Joe Biden amekemea kukiukwa kwa makubaliano ya amani na
amesema Urusi isipochukua hatua italipa gharama kubwa.
Akizungumza
katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa balozi wa Ukraine kwa Umoja huo,
Yuriy Sergeyev, amesema madai ya Urusi kwamba inachangia mchakato wa amani
hayatoshi. "Kama Urusi kweli inataka kuchangia juhudi za kuleta amani
Ukraine, lazima iondoe wanajeshi wake wote kwenye ardhi ya Ukraine na
iwalazimishe waasi wafuate masharti ya makubaliano ya amani ya Minsk,"
alisema Sergeyev.
Serikali
ya Ukraine imeyataka mataifa ya Magharibi yaongeze shinikizo kwa Urusi. Lakini
rais Vladimir Putin, anayekanusha kupeleka wanajeshi Ukraine, amesema mzozo
hautakomeshwa kwa nguvu za kijeshi. Badala yake amewaasa wanajeshi wa Ukraine
waweke silaha zao chini. Mpaka sasa mgogoro wa Ukraine umegharimu maisha ya
watu wapatao 5,600.
Post a Comment