Mwenyekiti TCCIA mkoani Shinyanga, Dickson Musula akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake (hawapo pichani). |
Moja ya viwanda vilivyoathiriwa na ubabe wa maofisa vipimo mkoani Shinyanga, inadaiwa walibeba mikono mitatu ya kwenye mizani na hivyo kusababisha kiwanda kushindwa kufanya kazi. |
Mmoja wa watumishi wa kiwanda cha Gladi Oil & Food Co. Ltd. akitumia mzani mdogo kwa shida baada ya mizani ya kawaida kubebwa na maofisa vipimo. |
CHAMA
Cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Shinyanga kimetoa ufafanuzi
kuhusiana na taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Wakala wa vipimo mkoani humo
ikidaiwa kuwepo kwa wafanyabiashara wanaoharibu kwa makusudi mizani zao kwa
lengo la kuwapunja wateja.
Akitoa
tamko rasmi mbele ya waandishi wa habari, mwenyekiti wa TCCIA mkoani
Shinyanga, Dickson Musula alisema mgogoro uliopo kati ya wafanyabiashara na
maofisa vipimo mkoani humo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya maofisa
hao kutoza gharama kubwa za ukaguzi wa mizani kinyume na maelekezo ya sheria.
Alisema
TCCIA mkoani humo mara kwa mara imekuwa ikiwaelimisha wafanyabiashara ambao ni
wanachama wake juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kuzingatia
masharti ya biashara wanazoziendesha ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima
kati yao na mamlaka nyingine za nchi.
Hata
hivyo alisema tatizo lililopo mkoani Shinyanga linatokana na wakala wa vipimo
kuwatoza gharama kubwa wafanyabiashara pale wanapofanya ukaguzi wa mizani pia
hupenda kutumia ubabe wanapotekeleza majukumu yao hali inayosababisha
wafanyabiashara wengi waanze kuwakwepa.
“TCCIA
mkoani Shinyanga tumeshangazwa na taarifa zilizotolewa mwishoni mwa wiki
iliyopita na meneja wakala wa vipimo mkoani Shinyanga akidai kuna
wafanyabiashara wengi wanye tabia ya kuchezea vipimo vyao kwa lengo la
kuwapunja wateja wao, lakini ukweli halisi sivyo ulivyo,”
“Hatusemi
wafanyabiashara wote ni wasafi, bali tunachokipigia kelele ni suala la kutozwa
fedha nyingi kinyume na utaratibu, kila mwaka wakati wa ukaguzi tunatozwa
kuanzia shilingi 70,000 na kuendelea kulingana na ukubwa wa mizani badala ya
shilingi 40,000 za kisheria, hilo ndilo tunalolipinga kwa nguvu zote kila mwaka,”
alieleza Musula.
Akifafanua
alisema kisheria ada ya ukaguzi kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura namba 340
iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 mizani ya kawaida isiyozidi uzito wa kilogramu
300 hupaswa kulipiwa ada ya shilingi 40,000 pekee lakini hata hivyo hutozwa shilingi
30,000 nyingine ikiwa ni gharama za matengenezo iwapo mzani una matatizo.
“Sasa
ajabu ni kwamba maofisa vipimo wetu baada ya kufanya ukaguzi baadae hujigeuza ndiyo
wasemaji wa mafundi wanaorekebisha mizani unapokuwa na matatizo, wanatutoza shilingi
30,000 kwa kila mzani bila kujali ni mzima au mbovu wanalazimisha lazima zilipwe hapa ndiyo penye
tatizo, maana ulazimishaji huu ni sawa
na wizi,”
“Kibaya
zaidi angalia hizi stakabadhi zao (angalia picha juu) kuna hii ya shilingi
40,000 ni ya serikali, lakini hii ya pili ni ya kampuni inayofanya marekebisho
ya mizani zenye matatizo, ajabu mtu anayeandika stakabadhi hizi ni mmoja wa
maofisa vipimo badala ya mafundi wenyewe, utaratibu huu TCCIA tunaupinga na
kuupiga vita,” alieleza Musula.
Musula
alisema wafanyabiashara mkoani Shinyanga hawapingani na sheria zilizopo bali
wanachokipinga ni vitendo vya uonevu wanavyotendewa na maofisa vipimo mkoani
humo ambao mara nyingi hutumia vitisho wanapotekeleza majukumu yao na hata
wanapotoa taarifa zao kwa ajili ya kazi ya ukaguzi huwa hazioneshi tarehe na
eneo husika la kufanyia kazi hiyo.
Hivi karibuni wakala wa vipimo mkoani Shinyanga ulitoa taarifa ya
kuwatahadharisha
wafanyabiashara wenye tabia ya kuchezea mizani zao kwa lengo la
kuwapunja
wateja baada ya kufanya ukaguzi sehemu mbalimbali na kuwakamata baadhi
ya wafanyabiashara waliokutwa wameharibu mizani zao kwa makusudi.
Post a Comment