Kaburi la marehemu Bernadetha Stephen likiwa limefukuliwa na watu wasiojulikana kama jinsi linavyoonekana kwa kutoka juu. |
Mkuu wa Upelelezi Polisi Mkoani Shinyanga, Kamanda Mussa Taibu (aliyeinama kushoto) akiangalia jinsi kaburi lilivyofukuliwa. |
KATIKA hali isiyokuwa
ya kawaida kaburi la marehemu Bernadetha Stephen (35) ambaye mwili wake
ulizikwa na kifaranga cha kuku tumboni hivi karibuni katika kile kilichodaiwa
kutekeleza mila za kikurya limefukuliwa
usiku na watu wasiojulikana.
Hali hiyo imezua
sintofahamu miongoni mwa wakazi wa kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga
akiwemo mume wa marehemu huyo Maulidi Njunju ambaye hata hivyo hakutaka
kuzungumza lolote mbele ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa mashuhuda
wa tukio hilo kaburi hilo lilifukuliwa usiku wa kuamkia Januari 13, mwaka huu ambapo baadhi ya
wananchi walitoa taarifa juu ya kitendo hicho na kusababisha umati wa wananchi
kufurika katika makaburi hayo kwa lengo la kujionea kilichotokea.
Mbali ya kufukuliwa kwa
kaburi hilo baadhi ya watu walivumisha uvumi mjini humo kwamba mwili wa
marehemu Bernadetha ulionekana ukiwa umesimama juu ya kaburi hilo hali iliyowashitua
baadhi ya watu hata hivyo hakuna hata mmoja aliyethibitisha kuonekana kwa mwili
huo kama ilivyokuwa ikivumishwa.
Kwa upande wake mjumbe
mwingine wa serikali ya mtaa wa Mapinduzi Deogratius Masanja alisema mume wa
marehemu Bernadetha awali alimpa taarifa kwamba siku tatu zilizopita ndugu
wawili wa marehemu huyo walionekana katika mtaa huo katika mazingira ya
kutatanisha.
Hata
hivyo alisema
alihisi huenda walikuja kumalizia mambo yao ya kimila baada ya mazishi
yaliyofanyika mnamo Januari 3, mwaka huu lakini pia baadhi ya wakazi wa
maeneo jirani na makaburi hayo walidai juzi usiku waliliona gari moja
likiranda randa katika maeneo
hayo japokuwa hawakuweza kubaini iwapo ni ndugu wa marehemu au watu
wengine.
Marehemu Bernadetha Stephen
alifariki dunia Januari mosi mwaka huu katika hospitali ya
serikali mkoani Shinyanga alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na uvimbe tumboni, alizikwa Januari 3, hata hivyo wakati wa
mazishi yake ndugu walizua tafrani kubwa baada ya kulazimisha kufanyika
kwa mitambiko ya kimila na hivyo kumzika akiwa na kifaranga cha kuku tumboni.
Post a Comment