KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA SHINYANGA, JUSTUS KAMUGISHA |
MAMA
mdogo wa mwanafunzi anayesoma kidato cha kwanza (13) (jina
limehifadhiwa) aliyebakwa na askari wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU)
mkoani Shinyanga amelilalamikia jeshi la polisi kwa kitendo cha kumpora
mtoto wake hali ambayo imesababisha ashindwe kurudi shuleni kuendelea na
masomo yake.
Mbali
ya kulalamikia kuporwa kwa mtoto wake pia mama huyo Neema Elisha
ameelezea wasiwasi wake kutokana na mwenendo mzima wa kesi ya polisi
huyo mbakaji inavyoendeshwa ikionesha dalili zisizoacha shaka kwamba
inachezewa kwa lengo la kutaka kuharibu ushahidi ili kumnusuru mtuhumiwa
huyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Shinyanga, Neema alisema mara baada
ya mwanae kubakwa na mmoja wa askari wa kikosi cha FFU aliyemtaja kwa
jina moja la Alex mnamo Januari 4, mwaka huu na wao kufungua mashitaka
kituoni wamekuwa wakisumbuliwa kila mara pasipo sababu za msingi.
Akifafanua
alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida baada ya mtoto wake kutoa
maelezo ya jinsi alivyobakwa polisi walikula njama na kumpora kutoka
nyumbani kwake Ngokolo manispaa ya Shinyanga katika mazingira ya
kutatanisha ambapo walimlazimisha atoe upya maelezo yake huku
akishinikizwa aeleze hakubakwa bali polisi aliyemtendea kitendo hicho ni
mpenzi wake.
“Kinachotia
wasiwasi mpaka sasa sifahamu mwanangu anaishi wapi,
nilipokwenda kituoni kuulizia waliniambia eti anatunzwa na ustawi wa
jamii baada ya mtoto kulalamika kwamba ninampiga sana kushinikiza aseme
alibakwa wakati siyo kweli, lakini nashangaa polisi wao ndiyo watuhumiwa
wanakaaje na mlalamikaji? hapa kweli kuna haki itatendeka?” alihoji
Neema.
Alisema
pamoja na kwamba wao ndiyo walalamikaji mpaka sasa hawana taarifa
zozote iwapo kesi hiyo imefikishwa mahakamani au bado na hata juzi
walipofuatilia ofisini kwa mkuu wa kituo (OCS) kutaka kufahamu mtoto
alipo na kama kesi imefikishwa mahakamani walifukuzwa na kutakiwa
waondoke mara moja kituoni hapo kwa vile wao ni kichomi.
Kamanda
wa Polisi mkoani Shinyanga Justus Kamugisha alikanusha madai ya polisi
kumpora mtoto huyo na kufafanua kuwa baada ya kufuatilia alibaini mtoto
alikwenda mwenyewe kituoni akilalamika kupigwa sana na mama yake na
kwamba kutokana na majadiliano yaliyofanyika walikubaliana akatunzwe na
watu wa ustawi wa jamii mpaka pale kesi yake itakapoanza kusikilizwa.
“Polisi hatuwezi kufanya upuuzi huo, nashangaa ninyi waandishi na
watu wa Agape sijui kwa nini mnalifuatilia sana hili, nilipopewa
taarifa za kupotea kwake nilishituka, nilifuatilia mwenyewe na nilipewa
taarifa yupo kituoni amekimbia kwao baada ya kupigwa sana, tukaone vyema
atunzwe na watu wa ustawi, sasa vipi idaiwe tumempora?” alieleza
Kamugisha.
Akizungumzia
suala la mtoto huyo kulazimishwa kutoa maelezo zaidi ya mara tatu
Kamugisha alisema huo ni utaratibu wa polisi na kwamba wanaweza kuchukua
maelezo kutoka kwa mlalamikaji hata zaidi ya mara kumi iwapo wataona
yale ya awali bado hayajajitoshelezi na kufafanua kuwa utaratibu huo ni
wa kawaida katika masuala ya kiupelelezi.
“Tutahakikisha
haki inatendeka, huyu polisi iwapo atabainika amefanya kosa, kwanza
tutamvua upolisi wake na kumpeleka mahakamani kujibu shitaka lake,
binafsi nitatoa taarifa kamili mara baada ya kukamilika kwa upelelezi,
hakuna mtu anayetaka kumlinda mtuhumiwa iwapo atabainika ametenda kosa,”
alieleza Kamugisha.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Festo Kang’ombe
alikiri kupata taarifa za ofisa wake wa Ustawi wa Jamii, Emmanuel Nhabi
kukabidhiwa mtoto huyo japokuwa hakuwa na taarifa kamili ya tukio zima
lililosababisha akabidhiwe mikononi mwa ustawi wa jamii.
Akizungumza
mbele ya mkurugenzi wake Nhabi alikiri kukabidhiwa mtoto huyo na mkuu
wa kituo cha polisi (OCS) cha mjini Shinyanga baada ya kuelezwa alikuwa
akifanyiwa vitendo vya ukatili na kutakiwa akamkabidhi katika kituo cha
Buhangija Jumuishi wakati akisubiri kesi yake, hata hivyo alisema juzi
alilazimika kumrejesha tena mikononi mwa polisi wenyewe.
Akizungumzia
suala hilo Mwanasheria mkuu wa serikali mkoani Shinyanga, Seth Mkemwa
alikiri kupokea jalada la kesi ya polisi wa FFU anayetuhumiwa kubaka na
tayari kesi hiyo imefikishwa mahakamani kwa kutajwa mara ya kwanza
ambapo alisema kiutaratibu kwa mara ya kwanza siyo lazima mama wa mtoto
kupewa taarifa au kulazimika kuwepo mahakamani.
Post a Comment