Serikali
imesema matunda yanayolimwa katika Mkoa wa Tanga licha ya kuwa ni mengi lakini
bado hayana sifa ya kutengeneza juisi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyetaka kujua ni
lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kiwanda cha matunda Mkoa wa
Tanga.
Mbunge
huyo alihoji kitendo cha Serikali kubadilisha eneo la kujenga kiwanda na sasa
imetangaza kujenga kiwanda hicho eneo la Msoga wilayani Bagomoyo.
Mbunge
huyo alitaka kuelewa sababu ya Serikali kuwa na kigugumizi cha kujenga kiwanda
hicho sehemu yenye matunda mengi kuliko Bagamoyo.
Pia
katika swali lake la nyongeza awali, mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina
mpango gani wa kutafuta mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kutengeneza juisi ya
machungwa mkoani Tanga.
“Wakulima
wa Machungwa Tanga hawana soko la machungwa na kusababisha kuoza, je Serikali
ina mpango gani wa kumtafuta mwekezaji,” alihoji mbunge huyo.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alisema machungwa
ambayo yanazalishwa mkoani Tanga hayana ubora wa kutengeneza juisi.
Mbali
na hilo alisema bado hakuna matunda ya kutosha ambayo yanaweza kukifanya
kiwanda kuwa na mwendelezo wa kuzalisha juisi kwani matunda yanayozalishwa
Tanga ni ya msimu.
Kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza juisi katika Mkoa wa Bagamoyo na Msoga, Naibu
Waziri huyo alisema limetokana na mapendekezo ya mwekezaji mwenyewe
aliyependelea eneo hilo zaidi kuliko eneo lenye matunda mengi.
Source: Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment