BAADHI
ya wanachama wa Umoja wa wanawake wa CCM (UWT) mkoani Shinyanga wamelalamikia kitendo
cha baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Jumuiya hiyo kuanza kupanga safu za
viongozi wanaowataka ili waweze kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao kitendo kinachopingana na taratibu za chama.
Wakizungumza na
waandishi wa habari kwa nyakati tofauti mjini Shinyanga wanachama hao
walidai baadhi ya viongozi na watendaji wa UWT hivi sasa wameanza kupitapita
kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa wakiwanadi wagombea wanaowataka wakidai
ndiyo wanaostahili kuchaguliwa katika uchaguzi ujao mwakani.
Wanachama
hao
wamedai kitendo kinachofanywa na viongozi wao kinapingana na maelekezo
ya chama
yanayozuia watendaji na viongozi walioko madarakani hivi sasa kujiingiza
katika upangaji wa safu za
watu wanaowataka wao na badala yake kazi hiyo wawaachie wanachama
wenyewe ndiyo wanaofahamu watu gani wa kuchaguliwa badala ya
kuchaguliwa.
Kutokana
na hali hiyo wamekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo kuanza
kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini viongozi wote ndani ya jumuiya
hiyo ambao wameanza kampeni kabla ya wakati huku wengine wakiwachafua
wenzao kwa misingi ya kidini, ukabila na rangi kinyume na maelekezo ya
katiba ya chama.
Mmoja
wa wanachama hao (jina tunalo) ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa UWT Shinyanga vijijini alisema tayari kuna kampeni za
chini chini zinazoendeshwa na baadhi ya viongozi ndani ya Jumuiya hiyo (majina
tunayo) wanaowanadi watu wao wakidai ndiyo wanaotakiwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa viti maalumu.
“Viongozi wetu wanataka kutuchanganya, binafsi
nimeshangazwa na kitendo cha kiongozi mmoja ndani ya UWT aliyeanza mikakati ya
kuwanadi wagombea hivi sasa anawasaka wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa akiwaomba wahakikishe wakati wa
uchaguzi wanawachagua (anataja majina) kuwa ndiyo wabunge wa viti maalum
watakaowakilisha mkoa wa Shinyanga,”
“Kibaya
zaidi ni kauli anazozitoa kiongozi huyo maana anadai mmoja wa watu wake anao uwezo mzuri wa
kifedha ambazo atakazigawa kwa wajumbe wote kwa lengo la kuhakikisha
anachaguliwa kwenye uchaguzi wa kura za maoni kitu ambacho
kinapigwa vita kila siku na CCM,” anaeleza mwanachama huyo.
Kwa
upande wake Susan Mashindike mkazi wa kata ya Iselamagazi Shinyanga vijijini amewaomba viongozi wa ngazi ya
juu ndani ya CCM kusisitiza suala la wana CCM kuheshimu maelekezo ya chama kwa
kusubiri muda muafaka wa kuanza kampeni za udiwani na ubunge.
Mashindike
alisema
kitendo cha viongozi na watendaji ndani ya CCM kujihusisha na upangaji
wa safu za viongozi wanaowataka wao ni cha hatari kwa vile kinaweza
kusababisha
mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu ujao
mwakani na hivyo kutoa mwanya kwa wapinzani kushinda kwa urahisi.
“Ni
vizuri
viongozi wakuu wa CCM kupitia vikao vya chama wakakemea hali ambayo
imeanza kujitokeza kwa wanaotaka kuwania nafasi za udiwani na ubunge wa
viti maalumu mwakani kupitia UWT, hali hii inastahili kukemewa mapema,
wapo watu wanataka
kutuletea vurugu ndani ya Jumuiya maana wengine wanatuletea suala la
ukabila,”
“Suala
la mgombea yupi achaguliwe na yupi asichaguliwe si la viongozi ama watendaji
ndani ya Jumuiya, kazi hii waache ifanywe na wapiga kura wenyewe, kutuambia fulani
ndiye anayestahili kuchaguliwa na fulani hafai ni kukiuka maadili ya chama
chetu, viongozi wetu wawakemee na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika,”
alieleza Mashindike.
Kwa
upande
wao baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT Shinyanga mjini walikiri
kuwepo kwa kampeni za chini kwa chini zinazoendeshwa na baadhi ya
viongozi ambao hata hivyo hawakupenda kuwataja majina hali inayoashiria
wazi tayari kuna safu ya viongozi iliyoandaliwa na kampeni hizo
zikilenga kuhakikisha ndiyo watakaochaguliwa.
Kwa
upande
wake mwenyekiti wa UWT mkoani Shinyanga Angela Paulo, alipohojiwa
kuhusiana na malalamiko hayo alikanushwa kuwepo kwa viongozi walioanza
kuwafanyia kampeni baadhi ya wagombea na kwamba kipindi cha kampeni
hakichafika.
"Siyo
kweli kuna kiongozi ye yote wa UWT ambaye ameanza kampeni, hayo ni
mambo ya kisiasa maana kila kinapofika kipindi cha uchaguzi watu huamua
kuzusha maneno yasiyo na ukweli, na hawa ni wale wenye hofu ya
kutochaguliwa, sisi viongozi ni jalala, tunasingiziwa kila kitu, ukweli
hakuna anayefanya kampeni hivi sasa," alieleza Paulo.
Post a Comment