Naibu Katibu mkuu wa CCM - Bara na Naibu waziri wa Fedha nchini, Mwigulu Nchemba akihutubia maelfu ya wana CCM na wananchi wengine mjini Shinyanga. |
WATANZANIA
wametahadharishwa kuacha tabia ya kuishinikiza serikali kuchukua hatua za
kuwawajibisha viongozi na watendaji wake bila ya kufanya uchunguzi wa kina dhidi
ya tuhuma mbalimbali zinazoibuliwa nchini kwa vile hatua hiyo imechangia
kutotendewa haki kwa baadhi ya watuhumiwa.
Tahadhari
hiyo imetolewa mjini Shinyanga na Naibu Katibu Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba alipokuwa akizundua rasmi kampeni za
CCM kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mkoani Shinyanga sambamba na
kuwaapisha makamanda wa Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) mkoani humo.
Nchemba
ambaye pia ni Naibu waziri wa fedha nchini alisema madhara ya kuishinikiza serikali
kuchukua hatua bila ya kufanya uchunguzi wa kina yamechangia serikali kuwapoteza
watendaji wake wazuri ambapo alitoa mfano wa ilivyotokea kwa aliyekuwa waziri wa
maliasili na utalii nchini, Ezekiel Maige.
Alisema
katika bunge lililopitisha azimio la kuwawajibisha mawaziri watano na manaibu
wawili Mei 4, 2012 watuhumiwa wote hawakupewa nafasi ya kujitetea kama
ilivyotokea hivi karibuni kwa watuhumiwa wa kashfa ya fedha za Tegeta
Escrow.
Naibu
katibu mkuu huyo alikiri katika kashfa hiyo Maige hakuwa na kosa lolote
kwa vile hata taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haikuzungumzia
wizara yake ya maliasili na utalii na kwamba iwapo angekuwa na kosa leo hii asingekuwa
huru maana angeishafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zake.
“Katika
maamuzi ya bunge yaliyowawajibisha mawaziri sita mwaka 2012 miongoni mwa watu
ambao hawakutendewa haki ni mbunge wenu wa jimbo la Msalala ambaye wakati huo
alikuwa waziri wa maliasili na utalii, Maige (Ezekiel), ukweli ni kwamba hakuwa
na kosa, ndiyo maana leo hii mnamuona tunaye hapa,” alieleza Nchemba na kuongeza,
“Ndugu zangu ninachopenda kuwaeleza leo hii ni kwamba serikali sasa
imechoka kuchukua maamuzi yake kwa kukurupuka au kwa kufuata upepo wa wananchi
wanavyotaka, tutahakikisha tunakuwa makini kwa kabla ya kuchukua hatua za kuwajibishana lazima tuchunguze kwa kina
kashfa yoyote ile itakayoibuliwa, vinginevyo tutakuwa hatuwatendei haki watendaji wetu."
Mbali
ya Maige mawaziri wengine waliowajibishwa pamoja naye mwaka 2012 ni aliyekuwa waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, Waziri wa Afya, Dk. Haji
Mponda na naibu wake Ruth Nkya na Naibu waziri wa uchukuzi, Athumani Mfutakamba.
Katika
hatua nyingine Nchemba alisema serikali hivi sasa inafanya jitihada
zitakazowezesha nchi kujitegemea kwa asilimia 100 badala ya kutegemea misaada
kutoka kwa nchi wahisani na kwamba hatua ya kutegemea misaada ya wafadhili
imechangia kukwama kwa shughuli nyingi za kimaendeleo pale wanapozuia misaada
yao.
Alitoa
mfano wa hivi karibuni ambapo nchi hizo wahisani zimezuia kutoa misaada waliyokuwa wameahidi kuchangia katika
bajeti ya mwaka 2014/2015 baada ya kuibuliwa kwa kashfa ya fedha za Escrow
ambayo mpaka sasa fedha zilizoahidiwa hazijatolewa.
Naibu waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele na mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini aliyeponea tundu la sindano katika kashfa ya fedha za TEGETA ESCROW. |
“Ndugu
zangu serikali hivi sasa inafikiria kuanza kujitegemea yenyewe kwa asilimia 100
badala ya kutegemea misaada ya wafadhili katika utekelezaji wa bajeti zake
za kila mwaka, tumeona misaada hii ya masharti ina matatizo, na hii ndiyo
ilichangia hata kushutumiwa kwa mbunge wenu Stephen Masele alipowalalamikia baadhi ya
mabalozi,”
“Ukweli
ni kwamba Masele hakuwa na kosa lolote, kwani alichokieleza bungeni kilihusiana na kitendo cha baadhi ya
mabalozi kuendesha kampeni za chini chini kutaka nchi yetu isipatiwe misaada
iliyoahidiwa, japokuwa alilaumiwa lakini madai yake yalikuwa na ukweli, sasa
lazima taifa kama taifa tuhakikishe tunajitegemea wenyewe,” alieleza.
Post a Comment